Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Story ya Eriksson inasikitisha

Sven Goran Eriksson.jpeg Kocha mzoefu wa soka duniani, Sven-Goran Eriksson

Sun, 18 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha mzoefu wa soka duniani, Sven-Goran Eriksson amerejea kuutangazia ulimwengu kuwa anaweza kuishi mwaka mmoja tangu sasa.

Sven mmoja kati ya makocha wenye heshima kubwa amesema anasumbuliwa na saratani ya kongosho na tayari madaktari wameshamwambia kuwa hawana uhakika kama ataweza kuishi zaidi ya mwaka mmoja.

Eriksson, 76, alitangaza mwezi uliopita kuwa aligundua alikuwa na saratani baada ya kuanguka ghafla na kupelekwa hospitali alipofika alielezwa kuwa ana ugonjwa huo usioweza kutibika.

Kocha huyo mwenye rekodi kubwa kwenye soka amesema hana hofu pamoja na kwamba kila siku muda wake wa kufa unasogea karibu.

“Najua kwamba muda mrefu zaidi wa kuishi utakuwa mwaka mmoja, lakini unaweza kuwa chini ya hapo. Kizuri zaidi unaweza kuwa zaidi ya hapo. Sina uhakika kama madaktari watakuwa wanafahamu siku kamili, wangenitajia.

“Unatakiwa kuiheshimu kila siku unayoishi hapa duniani. Daktari ameshanimbia kuwa nitaishi kama mwaka mmoja tu kuanzia sasa,” alisema.

Kocha huyo raia wa Sweden, alikuwa kocha wa kigeni wa kwanza kupata nafasi ya kuifundisha England na kuifikisha robo fainali ya Kombe la Dunia 2002 na 2006 pamoja na michuano ya Euro 2004.

“Nitaendelea kupambana kila iitwapo leo kuhakikisha naishi maisha mazuri kwa kipindi kifupi kilichobaki,” Eriksson aliiambia Swedish Radio P1.

“Ni ngumu kusema moja kwa moja, lakini ukweli ndiyo huo. Kwangu sasa siyo jambo linalonisumbua sana.”

Eriksson, ambaye alikaa kwenye kazi ya ukocha kwa miaka 42, mwaka jana mwishoni aliachana na timu ya Karlstad 11 ambayo alikuwa mkurugenzi wa ufundi kutokana na afya yake kuzidi kudhoofika.

“Sipo hospitali. Nakwenda mara chache na kurudi nyumbani. Nini? Marafiki wengi wanakuja kunitembelea muda wote na familia yangu ipo karibu.”

“Nimekuwa nikitoka nje mara moja moja kwenda kufanya mazoezi, pamoja na kwamba nina mwaka kwenye huu ulimwengu kama nilivyoelezwa, lakini namwamini Mungu lazima mambo mengine yaendelee kwa kuwa bado naishi.

“Ukiwa na ujumbe kama huu kichwani kwako, unatakiwa kuwa na furaha ukiona umeamka asubuhi salama, hilo ndiyo jambo ninalofanya kila siku.

“Nilikuwa kawaida sana nikiwa na afya njema, ghafla nikapata kiharusi watoto wangu wakanichukua na kunipeleka hospitali.

“Baada ya siku moja nilifanyiwa vipimo na kuelezwa kuwa kiharusi nilichopata nitapona kwa asilimia 100, lakini daktari akaendelea kusema, nina kansa ambayo hawawezi kuitibu kwa uwezo wao.

“Alianiambia atanipa dawa ambazo zinaweza kunisaidia kuendelea kuishi kwa kuwa wao hawawezi kufanya zaidi ya hapo,” alisema kocha huyo aliyeanza kufundisha soka kwenye klabu ya Degerfors mwaka 1977.

Kwa sasa afya ya kocha huyo imeendelea kudhoofu, lakini madaktari mbalimbali kwenye mitandao wamekuwa wakisema kuwa anaweza kuendelea kuishi kwa muda mrefu hata kama madaktari wamesema.

NDOTO YAKE:

Kwa kipindi chote ambacho, Sven alikuwa akifundisha soka, alikuwa anatamani kuiongoza Liverpool na amewahi kutamka hivyo mara kadhaa.

Ndoto yake imetimia baada ya klabu hiyo, kumtangaza kuwa kocha wa timu ya wakongwe wa Liverpool, itakayocheza mchezo wa hisani dhidi ya Ajax Machi 23 kwenye Uwanja wa Anfield.

Kocha wa Liverpool, Juggen Klopp, amesema anamruhusu kocha huyo akae kwenye kiti chake, ana mheshima na hata akitaka kuendelea kubaki klabuni hapo, anaruhusiwa kufanya hivyo. Sven atakuwa akisaidiana na Ian Rush, John Barnes na John Aldridge.

MAFANIKIO YAKE:

Kocha huyo amefanikiwa kuzifundisha timu nyingi kubwa Benfica, Roma, Fiorentina, Sampdoria na Lazio sehemu aliyopata mafanikio makubwa baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Italia Serie A, makombe mawili ya Italia na Uefa

Super Cup.

Eriksson alikuwa kocha wa England kwenye fainali mbili za Kombe la Dunia 2002 na 2006 na zote ilitolewa hatua ya robo fainali, kumbuka shuti kali la kiungo Ronaldinho ambalo liisaidia Brazil kuichapa England mabao 2-1.

lakini fainali zilizofuata, England ilitolewa na Ureno kwa mikwaju ya penalti, mechi ambayo Wayne Rooney alipewa kadi nyekundu.

Baada ya kukaa kwenye timu hiyo kwa miaka mitano, aliondoka pamoja na kwmaba alikuwa amebakiza mkataba wa miaka miwili.

Baada ya hapo, Eriksson alifundisha timu za Manchester City na Leicester City, pamoja na timu za Taifa za Mexico, Ivory Coast na Philippines.

KASHFA:

Miaka yake akiwa na England, alikumbana na skendo kadhaa ikiwa ni pamoja na gazeti moja kuandika kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi na mtangazaji wa televisheni Ulrika Jonsson mwaka 2002 nyingine ni kuwa na uhusiano wa kimapenzi na sekretari wake Faria Alam mwaka 2004.

MASTAA WASIKITIKA:

Mtandao wa X wa timu ya taifa ya England umeandika “Tunakupenda Sven,” Nahodha wa zamani wa England, Wayne Rooney baada ya taarifa ya kuumwa kwa Sven aliandika kwenye mitandao yake: “Hii ni habari ya kusikitisha, hakika tupo na Sven na familia yake, kocha bora na mtu muhimu sana, tupo pamoja na nawe, endelea kupambana.

Chanzo: Mwanaspoti