Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stars yapewa mbinu Chan

C3d4f31d5a53057ba2582469c8337f5d Stars yapewa mbinu Chan

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

BAADA ya timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kurejesha matumaini ya kufuzu robo fainali michuano ya Mataifa ya Afrika ya Chan, wadau mbalimbali wamehimiza wachezaji kutambua umuhimu wa mchezo ujao na kujipanga kwa utulivu na umakini ili kuibuka na ushindi.

Stars ilirejesha matumaini hayo juzi baada ya kushinda mchezo dhidi ya Namibia kwa bao 1-0 na kushika nafasi ya tatu katika Kundi D, huku Guinea na Zambia zikiongoza kwa pointi nne baada ya kupata sare ya bao 1-1.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana, baadhi ya wadau wakiwemo kocha wa zamani wa Stars, Charles Mkwasa, mchezaji wa zamani wa Simba, Mussa Mgosi, mchezaji wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua na Msemaji wa Ruvu, Masau Bwire walisema Stars ina nafasi ya kwenda hatua inayofuata endapo itaongeza umakini.

Mkwasa ambaye ni Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting alisema kikosi kilichocheza juzi kilionesha wazi kiko makini kutafuta matokeo ila mapungufu yaliyoonekana ni kukosa utulivu na umakini ambao katika mchezo dhidi ya Guinea wanahitajika kurekebisha yasijirudie.

"Mechi inayokuja ni ngumu, Guinea ni wazuri katika umaliziaji kinachohitajika kwetu ni kuacha kucheza mipira mirefu kama ilivyotokea ule uliopita, bali wacheze mipira ya chini tutaimudu kirahisi na kuhakikisha tunakuwa watulivu tutafanikiwa," alisema.

Kwa upande wake, Mgosi ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya wanawake ya Simba Queens, alisema wachezaji wanapaswa kujitambua na kujitoa kwa ajili ya taifa katika mchezo ujao wakijua Watanzania wana imani kwao.

Alisema benchi la ufundi linaweza kuongeza mbinu kulingana na mpinzani ajaye na kwa kutazama umuhimu wa mchezo huo wanatakiwa wajipange vizuri kupambana kwa jasho na damu ili kupata matokeo mazuri.

Naye Chambua alisema aliona mabadiliko kidogo kwenye kikosi na yameleta matokeo ila anaona bado kuna mapungufu yanayohitaji kufanyiwa kazi katika safu ya ushambuliaji na ulinzi ili Stars iweze kufanya vizuri zaidi.

“Nafasi ya kufuzu inawezekana ni jitihada tu zinahitajika, wachezaji wajiamini na kutulia wanaposhambuliwa, waache papara kwani inawezekana ikawagharimu,” alisema.

Bwire alisema ushindi uliopita dhidi ya Namibia ni ishara nzuri ya kurudi na kikombe na kuhimiza Watanzania kuiunga mkono na kushikamana na kufuta tofauti za usimba na uyanga zinazoweza kuchochea timu kufanya vibaya.

"Naipongeza Stars kwa ushindi ila kocha arekebishe mapungufu kwenye safu ya ulinzi na ushambuliaji, suala la kukosa utulivu na umakini liangaliwe lisijirudie. Lakini kingine, mashabiki wa Simba na Yanga waache kubaguana tutasababisha timu isifanye vizuri," alisema.

Bwire alitolea mfano mechi ya juzi kitendo cha mashabiki wa Yanga kutamba mtandaoni eti Yanga imefunga bao 1 na pointi tatu kisa mchezaji Farid Mussa anayetoka klabu hiyo alifunga, alisema haifai kwa timu ya taifa.

Chanzo: habarileo.co.tz