Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stars yamaliza kwa ushindi

B8f9631c398aea7fd73cf183f9d195d6 Stars yamaliza kwa ushindi

Mon, 29 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TIMU ya soka ya taifa, Taifa Stars, imekamilisha ratiba ya kuwania kufuzu michuano ya Afrika kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi Libya jana.

Libya imemaliza michezo yote ikiwa inaburuza mkia katika kundi J ikiwa na pointi tatu.

Mchezo huo wa kukamilisha ratiba uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa ulikuwa wa kutafuta heshima kwa timu hizo mbili baada ya Tunisia na Equatorial Guinea kufuzu kutoka hilo.

Katika mechi ya jana, Libya ilikuwa ya kwanza kulifikia lango la Stars katika dakika ya nne kupitia kwa mlinzi wa kulia Rabia Abubakar ambaye alikosa bao la wazi akiwa na Aishi Manula, wenyeji walijibu mapigo dakika ya 16 kwa mpira wa adhabu kupitia kwa Mbwana Samatta lakini hawakufanikiwa kupata bao.

Wenyeji walikosa bao la wazi katika dakika ya 25 baada ya Simon Msuva kushindwa kukwamisha mpira wavuni akiwa yeye na nyavu baada ya kipa kupigwa chenga na Samatta ambaye shuti lake liligonga mwamba dakika ya 38, Samatta tena alishindwa kuwapa uongozi Stars baada ya shuti lake kugonga mwamba na kwenda nje ya uwanja.

Taifa Stars ilipata bao lake la pekee kupitia kwa mshambuliaji Msuva katika dakika ya 46 akiunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa na kiungo Deus Kaseke kutoka upande wa kushoto wa uwanja.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Libya ikiliandama lango la Stars lakini uimara wa Manula ulikuwa kikwazo ambapo aliokoa michomo hatari katika dakika ya 51 shuti la Mohamed Rabia na dakika ya 64 shuti la Rabia Abubakar.

Stars ilijibu shambulizi katika dakika ya 86 kupitia kwa Ayoub Lyanga aliyepokea pasi ndefu ya mshambuliaji Shaaban Idd lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa wa Libya, katika dakika ya 90 Erasto Nyoni alioneshwa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Rabia Hassan.

Kikosi cha Tanzania: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Nickson Kibabage, Kennedy Juma, Erasto Nyoni, Jonas Mkude/Bakari Nondo dk 55 , Deus Kaseke/ Shaaban Idd dk 55, Hassan Dilunga/ Abdul Suleiman dk 72, Feisal Salum/ Himid Mao dk 72 , Mbwana Samata na Saimon Msuva/ Ayoub Lyanga dk 55.

Chanzo: www.habarileo.co.tz