Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stars mbele ni Samatta, Msuva

Msuva Samatta Rg Stars mbele ni Samatta, Msuva

Fri, 17 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kimeondoka asubuhi ya jana kwenda Morocco kuwahi pambano la Kundi E la kuwania kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Niger linalopigwa kesho kwenye Uwanja wa Marrakech litakalochezeshwa na waamuzi wote kutoka Algeria.

Stars na Niger zilizopo kundi moja na nchi za Morocco, Zambia na Congo, huku Eritrea iliyokuwa imepangwa kundi hilo ikijiondoa, zitacheza kesho kuanzia saa 4 usiku kabla ya timu hiyo ya Tanzania kurejea nyumbani mapema wiki ijayo kuikaribisha Morocco iliyomaliza ya nne kwenye fainali za Kombe la Dunia za Qatar 2022.

Kama tulivyoona kwenye safu ya makipa kisha jana kuchungulia eneo la mabeki na viungo, Stars imeondoka na majembe ya maana kwenye eneo la ushambuliaji.

Kocha Adel Amrouche amewaita jumla ya wachezaji tisa wanaocheza eneo la ushambuliaji waliobeba matumaini ya timu hiyo kwenye ufungaji mabao katika mchezo huo wa kwanza kabla ya mechi ya nyumbani dhidi ya Morocco.

Kocha Adel amewachukua washambuliaji hao wenye mchanganyiko tofauti kwa maana ya wale wazoefu na vijana huku ndani yao kukiwa na nahodha mkuu Mbwana Samatta.

Mbali na Mbwana anayekipiga klabu ya PAOK FC ya Ugiriki, wengine walioitwa ni; Saimon Msuva (JS Kabylie, Algeria), John Bocco na Kibu Denis (wote Simba), Abdul Suleiman (Azam FC), Ben Starkie (Basford United, England), Matteo Athony (Mtibwa Sugar), Charles M’mombwa (Macarthur, Australia) na Clement Mzize (Yanga).

NI SAMATTA NA MSUVA

Kocha Adel kama tulivyoeleza mwanzoni anapenda kutumia mfumo wa 3-5-2 ambao unampa nafasi au kuhitajika kuchagua washambuliaji wawili tu wa kuanza nao kwenye kikosi hicho kwa eneo la mbele na katika hilo hakuna namna nafasi kubwa itaweza kuangukia kwa Samatta na Msuva ambao mara nyingi ndio amekuwa akianza nao kwenye kikosi cha kwanza.

Samatta ameanza kurudi kwenye ubora wake akiwa na klabu ya PAOK ya Ugiriki akifunga kwenye mchezo wa mwisho wa klabu yake dhidi ya Panetolikos.

Msuva naye ni ngumu kuanzia nje akiwa na Stars kutokana na rekodi yake ya kufunga akiwa na kikosi hicho cha Stars, pia ubora wao katika kucheza kwa kutumia mfumo huo pia inawabeba.

BENCHI WATU WAPO

Hata kama washambuliaji hao wataanza na kushindwa kufanya vizuri bado, kocha Adel ana nafasi nyingine ya kuchagua watu wengine bora wa kuja kuwasaidia wawili hao wakiwemo John Bocco, Kibu Denis, Abdul Seleman ‘Sopu’, Matteo Antony na Clement Mzize.

MGENI ATAAMUA

Safu hiyo ina mtu mmoja mpya Charles M’Mombwa anayecheza soka Australia kwenye klabu ya Macarthur ambaye Adel ataamua kutokana na ubora wake huku kinda Ben Starkie anayeichezea Basford United ya England akiendelea kuvuna uzoefu.

Bado Adel ana nafasi ya kuamua kubadilika kutoka mfumo wa 3-5-2 na kutumia ule wa 4-3-3 ambao anaweza kuja kuwatumia Kibu, Sopu na Mzize kutengeneza ubora wa eneo hilo la mwisho kwa kuwa ni mifumo ambayo hata klabuni kwao wamekuwa wakiitumia.

Kwa kurejea matokeo ya mechi zilizopita baina ya timu hizo, kuna uwezekano mkubwa wa Stars kuanza mechi za makundi vyema kama wachezaji wataamua kuliamsha mwanzo mwisho ili kujitengenezea morali na mazingira mazuri kwa mchezo wa Novemba 21 itakapoikarisha Morocco kwenye Uwanja wa Mkapa.

Chanzo: Mwanaspoti