Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stars kusaka rekondi mpya AFCON 2023

Taifa Stars Link Taifa Stars yapewa mbinu AFCON 2023

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo inakabiliwa na kibarua kigumu ikicheza mechi ya kwanza katika fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka huu dhidi ya Morocco katika Uwanja wa Laurent Pokou, San Pedro kuanzia saa 2:00 usiku.

Ugumu wa mchezo huo unachangiwa na ubora wa Morocco ambayo ndio timu inayoongoza kwa viwango Afrika, hilo likichangizwa kwa kiasi kikubwa na mafanikio ambayo iliyapata katika fainali za Kombe la Dunia 2022, ambapo iliandika historia ya kuwa timu ya kwanza Afrika kufika nusu fainali.

Mbali na hayo, pia ubora wa mchezaji mmojammoja na ule wa kitimu ambao Morocco imekuwa nao, unailazimisha Taifa Stars kufanya kazi ya ziada ili kupata matokeo mazuri katika mechi hiyo ambayo yataiweka katika uwezekano mzuri wa kutinga hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii.

Taifa Stars inaingia katika mchezo huo ikiwa inaitegemea zaidi safu ya ulinzi ambayo ilifanya kazi nzuri katika mechi za kuwania kufuzu fainali hizo, ambapo iliruhusu mabao manne katika mechi sita huku ikicheza mechi tatu kati ya hizo bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.

Udhaifu ambao Taifa Stars inapaswa kuuepuka katika mechi hiyo ni ule wa safu ya ushambuliaji kutokana na ubutu katika kufumania nyavu kwenye mechi ambazo ilicheza hivi karibuni hasa zile za mashindano.

Katika harakati za kuwania kufuzu Afcon, Taifa Stars ilifunga mabao matatu katika mechi sita ikiwa ni wastani wa bao 0.5 kwa mchezo, takwimu ambazo zinaonyesha kwamba washambuliaji wa deni kubwa kwa timu hiyo kwenye Afcon, mwaka huu.

Katika mchezo wa leo, matumaini makubwa ya Taifa Stars yapo kwa mabeki Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Novatus Miroshi na Haji Mnoga ambao wameonekana kufanya kazi nzuri na kuzoeana vilivyo pindi wakicheza pamoja, lakini wote wakiwa na uzoefu wa kutosha wa michuano mikubwa ya kimataifa.

Uwepo wa winga msumbufu Tarryn Allarakhia unaonekana unaweza kuichangamsha safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars kutokana na uwezo wa kupiga chenga na kutengeneza nafasi pamoja na kasi kwa nyota huyo wa Wealdstone ya England.

Taifa Stars katika mechi hiyo itapaswa kuwachunga zaidi viungo wa Morocco, Azzadine Ouna na Bilal Elkhannouss ambao wamekuwa moto wa kuotea mbali katika kutengeneza nafasi za mabao kwa timu hiyo na kufungua safu za ulinzi za timu pinzani, huku ikiwa na wachezaji wengi ambao iliwatumia kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizopita hivyo wana uzoefu wa kupambana uwanjani.

Historia ya mechi baina ya timu hizo mbili inaonyesha kwamba Taifa Stars imekuwa na unyonge mbele ya Morocco kwani katika mechi tano zilizowahi kukutana, imepata ushindi mara moja huku ikipoteza michezo minne.

Ushindi dhidi ya Morocco sio tu utakuwa ni jambo la kushtua, bali utakuwa wa kwanza kwa Taifa Stars kuupata kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika kwani katika awamu mbili tofauti ilizowahi kushiriki haikuonja ladha ya ushindi ikitoka sare moja na kupoteza mechi tano.

Katika fainali za mwaka 2019, Stars ilipewa matumaini makubwa ya kufanya mambo ya kushangaza, lakini ilishindwa kufurukuta na kuambulia mabao mawili ilipochapwa na Kenya 3-2 mchezo wa mwisho wa kundi.

Jana Stars ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa San Pedro na wachezaji walionekana kuwa na morali ya hali ya juu ambapo kwa mujibu wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro nyota wote wa Tanzania wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo.

“Nimezungumza na wachezaji kila mmoja yupo tayari. Hakuna shaka kuwa tunaweza kufanya vizuri. Hapa hali ya hewa inaturuhusu, endeleeni kutuombea,” alisema Dk Ndumbaro ambaye ameandamana na timu hiyo.

Hata hivyo, kuna uwezekano staa wa Morocco anayeichezea Bayern Munich, Noussair Mazraoui akakosekana kwenye mchezo huo kutokana na kusumbuliwa na majeraha, lakini timu hiyo inatarajiwa kuongozwa na Hakim Ziyech ambaye alifunga bao moja wakati Stats ilipovaana na Morocco, Novemba, mwaka jana, ambaye atasaidiana na kiungo wa Manchester United Sofyan Amrabat.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live