BAADA ya Alhamisi Machi 25 kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Guinea ya Ikweta na kupoteza matumaini ya kufuzu fainali za mataifa ya Afrika 'Afcon' leo Jumapili saa 10:00 jioni timu ya Taifa ya Tanzania itaingia uwanjani kucheza mechi ya mwisho dhidi ya Libya.
Stars wenye alama nne watakuwa nyumbani kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa watahitaji kushinda mchezo huo ili kuweka heshima na kuongeza rekodi japo hawawezi kufuzu kwani tayari Guinea ya Ikweta na Tunisia wana alama nyingi ambazo hawawezi kuzifikia.
Hivyo hivyo kwa Libya wenye alama tatu nao watakuwa wanakamilisha ratiba tu kwani wanaburuza mkia kwenye kundi hilo (J) na matokeo yeyote hayatawasaidia zaidi ya kuwaongezea wasifu na rekodi tu kama ilivyo kwa Stars.
Wakati huo huo vinara wa kundi hilo Tunisia wenye alama 13 watakuwa nyumbani kuwakaribisha Guinea ya Ikweta wenye alama tisa mchezo ambao pia ni wa kuhitimisha ratiba ya kundi kwani timu hizo mbili tayari zimefuzu kucheza Afcon Mwakani.
Michezo mingine ya leo itakua kati ya Namibia na Guinea kutoka kundi A, na Ghana na Sao Tome kutoka kundi C ambapo mechi hii itachezwa saa 1:00 usiku huku nyingine zote zikianza saa 10:00.