Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stars ijipime na timu zenye uwezo Afrika

Fa58cc43bed650e305f964b5bd2e88af Stars ijipime na timu zenye uwezo Afrika

Sat, 19 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TIMU ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) wiki iliyopita ilicheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Malawi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kushinda kwa mabao 2-0.

Mchezo huo na mingine itakayokuja ni muhimu kwa Taifa Stars kwani kwa sasa iko katika mbio za kutafuta nafasi ya kufuzu kwa mashindano ya Kombe la Dunia, ambalo fainali zake zijazo zitafanyika Qatar 2022.

Tanzania imeshiriki mara mbili fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ikiwa ni mwaka 1980 nchini Nigeria na 2019 huko Misri, lakini hatujawahi kucheza fainali za Kombe la Dunia hata mara moja.

Timu yetu hiyo inahitaji mechi nyingi za majaribio zile za nyumbani na ugenini na tena timu zenye uwezo mzuri katika soka la Afrika ili kuipa uzoefu na uwezo wa kukabiliana na timu zenye uwezo mkubwa kama Misri, Ghana, Zambia na Algeria na zingine.

Pamoja na Malawi kuwa katika nafasi ya 115 katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikishi la Kimataifa la Soka (Fifa) na Tanzania iko katika nafasi ya 137 kwa mwezi uliopita, lakini bado timu hiyo sio kipimo kizuri sana kwa Taifa Stars.

Tanzania ni miongoni mwa timu zilizopo katika makundi ya kusaka nafasi ya kucheza hatua ya mwisho ya kusaka kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia Qatar 2022, hivyo inahitaji majaribio zaidi tena kutoka timu bora barani Afrika.

Timu kama Ghana, Cameroon, Ivory Coast, Senegal, Mali, Nigeria na zinhgine zinaweza kuwa kipimo tosha kwa kuifanya timu yetu kupata uzoefu na kuzoea mechi za kimataifa.

Taifa Stars inaweza kufanya vizuri na wengi wakaishangaa endapo itajiandaa vizuri kwa ajili ya mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Duniana maandalizi yanatakiwa kuanza sasa.

Timu hiyo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani naugenini dhidi ya Burudi, ilishinda kwa penalti 3-0 na kutinga hatua ya makundi, hivyo sasa inasubiri kuanza kampeni zake Septemba mwaka huu ili kusaka nafasi hiyo ya kwenda Qatar.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatakiwa kuiandaa vizuri Taifa Stars kwa ajili ya mechi hizo za hatua ya makundi, ambapo kila kunsdi litatoa timu moja itakayocheza hatua ya mwisho ya kufuzu kabla ya kukata tiketi ya Kombe la Dunia.

Ni matarajio yetu kuwa TFF itakuwa makini kutumia kalenda ya Fifa kwa kuchagua timu zenye uwezo wa kufanya vizuri dhidi ya timu bora katika soka la Afrika na sio kuchagua timu rahisi, ambazo hazitaisaidia timu yetu kufanya vizuri.

Chanzo: www.habarileo.co.tz