Benchi la ufundi la Taifa Stars litautumia mchezo wa leo wa kirafiki dhidi ya Sudan kuanzia saa 1:00 usiku huko Riyadh, Saudi Arabia kwa mambo mawili makubwa ambayo ni kuwatazama nyota wapya waliojumuishwa kikosini lakini pia kama kipimo cha mwisho cha kujiandaa na mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwezi ujao dhidi ya Niger na Morocco.
Mchezo huo utakaochezwa katika Uwanja wa Kimataifa wa King Fahd ni wa kwanza kwa Taifa Stars baada ya kukaa mwaka mmoja bila kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki tangu ilipocheza mechi ya mwisho dhidi ya Libya, Septemba 27 mwaka jana.
Sura mpya zinazoweza kupata nafasi ya kuonyesha makali leo ambazo zimeitwa kwa mara ya kwanza tangu kocha Adel Amrouche aanze kuinoa timu hiyo ni Kipa Ally Salim, Baraka Majogoro, George Mpole, Nassor Saadun na Abdulrazack Hamza.
Ukiondoa hao, wengine walioitwa wameshawahi kufanya kazi na Amrouche ambaye hivi karibuni ametoka kuiongoza timu hiyo kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zitakazofanyika mwakani huko Ivory Coast.
Kwa upande mwingine mchezo huo ni muhimu kwa mastaa wa Taifa Stars kujiweka tayari na harakati za kuwania tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia katika fainali zitakazofanyika 2026 katika nchi za Canada, Marekani na Mexico ambapo mechi zake za kuwania kufuzu zitaanza mwezi ujao.
Katika mashindano hayo ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia, Taifa Stars iliyopangwa kundi E la kuwania kufuzu Kombe la Dunia, itaanza kukabiliana na Niger, Novemba 13 na baada ya hapo itarudi nyumbani kucheza na Morocco, Novemba 20.
Lakini pia mchezo huo unaweza kutumika kama sehemu ya mwanzo ya maandalizi ya kushiriki fainali za Afcon mwaka ambapo wamepangwa katika kundi F pamoja na timu za Morocco, Zambia na DR Congo.
Kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco alisema wanaupa uzito mkubwa mchezo wa leo.
"Sudan ni timu nzuri na tunaamini itatupa kipimo kizuri katika maandalizi yetu ya kujiandaa na mashindano yaliyo mbele yetu. Kupata mechi kama hizi ni jambo zuri ambalo linatupa fursa ya kuona mambo tofauti ya kiufundi.
"Mechi itakuwa ngumu lakini hilo ndilo tunahitaji ili tuweze kuona wapi pa kurekebisha," alisema Morocco.