Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stars haikuwa bahati Afcon 2023

Taifa Stars Link Stars haikuwa bahati Afcon 2023

Sat, 27 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Taifa Stars imeaga michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023. Ndio, Mashujaa wa timu hiyo ya taifa, sasa wanarudi baada ya kazi kubwa ya kulipigania taifa katika fainali hizo za 34 zinazoendelea Ivory Coast baada ya juzi usiku kulazimishwa sare isiyo na mabao na DR Congo.

Hizo zilikuwa fainali za tatu kwa Tanzania baada ya zile za mwaka 1980 zilizofanyika Nigeria na 2019 zilizopigwa Misri, fainali ilizofanya vibaya kuliko nyingine zote. Katika fainali hizo za Misri, Stars ilitoka kapa ikifunga mabao mawili tu na kufungwa manane, lakini bila kuambulia pointi hata moja, kwani ilipoteza mechi zote, tofauti na zile za 1980 ilipotoka na pointi moja baada ya sare dhidi ya Ivory Coast.

Stars katika fainali za Nigeria, ilifungwa mabao 3-1 na Nigeria kisha kulala 2-1 mbele ya Misri na hivyo kutoka na mabao matatu, huku ikifungwa sita na kuambulia pointi moja.

Katika fainali za mwaka huu, Stars ikiwa Kundi F, japokuwa imetolewa lakini sio kinyonge sana, kwani imevuna pointi mbili baada ya sare mbili mfululizo dhidi ya Zambia (1-1) na suluhu mbele ya DR Congo, lakini ikifungwa mabao machache zaidi, manne na kufunga pia machache (moja tu) kwani ililala 3-0 kwa Morocco.

Kama ilivyomaliza kwenye fainali mbili za nyuma kwa kuburuza mkia, hata safari hii Stars imemaliza ikiwa eneo hilo baada ya Morocco kuongoza kundi ikiwa na pointi saba, ikifuatiwa na DR Congo (3), huku Zambia ikilingana nayo pointi mbili kila moja, lakini uwiano wa mabao umeibeba timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu.

Wakati hesabu kwa sasa zikiwa fainali zijazo za 2025 ambazo zitafanyika huko Morocco kabla ya michuano hiyo kuja Tanzania, haya ni mambo manne ambayo yameikwamisha Taifa Stars kuweka historia huko Ivory Coast.

Ikumbukwe kuwa katika awamu zote ambazo Taifa Stars imeshiriki fainali hizo haijawahi kuvuka hatua ya makundi.

UZOEFU

Japo yapo mataifa ambayo vikosi vyake ni vichanga wala sio wazoefu kwenye fainali hizo na yamefanya vizuri lakini uzoefu ni miongoni mwa mambo ambayo yanaweza kuibeba timu na kufanya vizuri kwenye mashindano yoyote yale.

Tuitazame Senegal kama mfano mzuri wa kuigwa imemaliza hatua ya makundi ikiweka rekodi ya kuvuna pointi tisa mbele ya Cameroon, Guinea na Gambia ambazo ilikuwa nazo kundi moja (C), kikosi chake kimeundwa na wachezaji wengi wenye uzoefu na michuano hiyo ambayo wao ndio mabingwa watetezi.

Licha ya Misri kutotinga kwa kishindo kama ilivyozoeleka nalo ni taifa lenye uzoefu wa kutosha kwenye michuano hiyo hata ukikitazama kikosi chake unaweza kukuta idadi kubwa ya wachezaji ambao hii ni mara yao ya tatu hadi nne kucheza fainali hizo ambazo hufanyika kila baada ya miaka miwili.

Vipi kuhusu Morocco na mataifa mengine makubwa? mbali na ubora wa vikosi vyao, uzoefu ni miongoni mwa silaha ambazo zimekuwa zikiibeba. Kwenye kikosi cha Taifa Stars unaweza kuona ni wachezaji wachache mno wenye uzoefu na mashindano hayo ambao ni Mbwana Samatta, Simon Msuva, Himid Mao na Aishi Manula wote hao walikuwepo kwenye fainali za 2019 ambazo zilifanyika Misri.

Stars inatakiwa kuendelea kukomaa na kupata nafasi ya kushiriki fainali hizo mara kwa mara kwanza kabla ya kuwa na hesabu za kufanya makubwa.

UBORA

Hili ni eneo muhimu mno, ubora upo na nafasi kubwa sana ya kuifanya timu kufanya vizuri kwenye mashindano yoyote yale hata kama haina uzoefu wa kutosha ikiwa bora ni wazi kuwa inaweza kuwa tishio, mfano mzuri kwenye hili ni Mauritania na Namibia ambazo zimetinga hatua ya 16 bora.

Nani ambaye alizipigia hesabu timu hizo kuwa zingevuka hatua ya makundi? Anaweza kuwepo mmoja kati ya 100, vikosi vyao vinaonekana kuwa na ubora wa aina yake na sio ajabu wakaendelea kutushangaza kwenye mashindano pamoja na kwamba wanavibarua vigumu mbele yao.

Kimsingi ni kwamba Stars inatakiwa kuendelea kupiga hatua kufika kule ambako wenzetu wapo, yapo mataifa ambayo yalikuwa ya kawaida mbele yetu kama vile Cape Verde na hata Burkinafaso lakini kwa sasa yanaonekana kutuacha mbali sana, wenzetu wamekuwa wakikua kwa kasi sana.

Wapo wachezaji mmoja mmoja kwenye kikosi cha Taifa Stars wenye ubora lakini idadi ni ndogo mno ukilinganisha na wenzetu, tukifika hatua ya kuwa na akina Samatta wa kutosha ambao watakuwa wanacheza ligi kubwa huko Ulaya inaweza kusaidia kuongeza ubora kwenye kikosi cha timu ya taifa.

HESABU

Inawezekana kama Stars ingekuwa na hesabu nzuri kwenye mchezo dhidi ya Zambia ingeweka historia ya kutinga hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza maana kwa matokeo ya mechi dhidi ya DR Congo ingeshika nafasi ya pili kwenye kundi ikiwa na pointi nne lakini ndio hivyo mipango sio matumizi.

Stars ikiwa na nafasi ya kushinda dhidi ya Zambia ambayo ilikuwa pungufu haikuwa kwenye ubora wake katika kipindi cha pili kwenye mchezo huo, ilionekana kukaa nyuma na kujilinda jambo ambalo liliwapa nguvu wapinzani na kupata bao la kusawazisha ambalo liliifanya timu kuwa na kazi kubwa ya kufanya kwenye mchezo wake wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya DR Congo.

UFUNDI

Stars imekuwa chini ya makocha wawili tofauti kwenye fainali moja ya Afcon, hili halina afya katika mahesabu ya timu kimbinu yote hiyo imetokana na kusimamishwa kwa Adel Amrouche ambaye ndiye aliyekiandaa kikosi na kukisimamia kwenye mchezo mmoja tu dhidi ya Morocco.

Amrouche ambaye anaonekana kukalia kuti kavu, alifungiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) mechi nane kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Morocco (RMFF) dhidi yake.

RMFF ilimlalamikia kocha huyo kwa kauli zake kuwa Morocco inaushawishi ndani ya CAF katika kupanga mechi pamoja na waamuzi lakini hata hivyo, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilimsimamisha kocha huyo na nafasi yake ikachukuliwa na Hemed Suleiman ‘Morocco’ kama kaimu huku akisaidiwa na Juma Mgunda. Makocha hao wazawa wameisaidia Taifa Stars kuvuna pointi mbili.

MASTAA WAFUNGUKA

Baada ya mchezo dhidi ya DR Congo, kiungo wa Azam FC, Feisal Salum alisema.

“Namshukuru Mungu tumemaliza mchezo salama, mashindano yalikuwa mazuri kundi letu lilikuwa gumu halikuwa rahisi tunamshukuru Mungu kwa kutujaalia tulichokipata tunajipanga siku nyingine,” anasema.

Mshambuliaji, Simon Msuva ambaye alifunga kwenye mchezo dhidi ya Zambia, alisema wanatakiwa kurejea kwenye fainali zijazo wakiwa bora zaidi ili kutoa changamoto lakini pia nyota huyo amefichua kuwa Afcon imempa Ulaya huko Saudia.

“Tumeshindwa kuingia hatua inayofuata lakini kuna mabadiliko na tutajipanga katika mashindano yajayo, kingine ni kwamba michuano hii imesaidia kupata timu, sikutaka kukata tamaa na unajua nimetoka kwenye matatizo kwenye timu yangu (JS Kabalie) ya Algeria lakini nilijua tu siwezi kukosa timu,” anasema.

Nyota wa DR Congo, Fiston Mayele ambaye aliwahi kucheza soka la kulipwa Tanzania, anasema;

“Stars ina wachezaji wazuri tumeona Afcon imekuwa na maajabu mengi sana, tulikuwa na mpango mzuri na kujua kama hatuwezi kufunga hatuwezi kufuzu, ulikuwa mchezo mzuri nilikuwa nacheza na rafiki zangu nilicheza nao Yanga (Nondo na Baka).”

Chanzo: Mwanaspoti