Dakika 45 za kipindi cha kwanza za mchezo wa kufuzu fainali za mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zimemalizika kwa Stars kutoka suluhu ya 0-0 dhidi ya Uganda.
Mchezo huu wa kwanza wa hatua ya mtoano unaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salam umeshuhudia timu zote zikishambuliana kwa zamu na tahadhari kubwa.
Uganda chini ya kocha wake mkuu, Milutin Sredojevic 'Micho' ilianza kwa kasi mchezo huu huku ikitengeneza mshambulizi kadhaa ambayo hayakuleta changamoto kwa Stars.
Dakika ya 10, Stars ilipata nafasi nzuri ya kuandika bao la utangulizi baada ya mshambuliaji, Kibu Denis kupiga mpira kichwa ambao haukuwa na madhara kufuatia krosi zuri iliyopigwa upande wa kushoto na Farid Mussa.
Licha ya Stars kuonekana kutawala mchezo ila eneo la katikati mwa uwanja ndilo ambalo limekuwa tishio kwa timu zote mbili kutokana na upinzani ulioonyesha hadi dakika hizi 45 za kwanza.
Stars ambayo imezungukwa na viungo wawili wakabaji, Jonas Mkude na Salum Abubakar 'Sure Boy' wameonyesha kustahimili vishindo vya, Siraje Sentamu anayekipiga kwenye klabu ya Vipers na Marvin Youngman ambao wamekuwa muhimili kwenye kikosi cha 'The Crane'.
Hadi kufikia dakika 45 za kipindi cha kwanza zinatamatika sio Stars wala Uganda iliyoona lango la mwenzake, huku makocha wa pande zote mbili wakiwa na jukumu nzito la kufanya kipindi cha pili.