Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stars, DR Congo vita ya kujuana

Fei Toto Stars Stars, DR Congo vita ya kujuana

Tue, 23 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa sasa ni mwendo wa kuhesabu vidole juu ya hatma ya timu yataifa ‘Taifa Stars’ kutinga hatua ya 16 bora kwenye michuano ya Afcon inayoendelea nchini Ivory Coast.

Tanzania iliyopo kundi ‘F’ ikishika nafasi ya nne kwenye mechi mbili, tayari imepoteza dhidi ya Morocco na juzi ilitoka sare na Zambia.

Kesho, Jumatano, Stars itacheza na DR Congo yenye pointi mbili na ili kusonga hatua ya 16 itahitaji kushinda mchezo huku ikiombea Zambia ifungwe na Morocco. Lakini kuna vita za kujuana:

MAYELE VS MWAMNYETO, BACCA

Hii ni vita ya wachezaji wanaofahamiana vizuri kwani msimu uliopita wote walicheza wote Yanga iliyobeba ubingwa wa Ligi na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa Stars Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca ndio mabeki wa kati ambao wamecheza dakika 180 kwenye mechi mbili za Afcon wakiruhusu mabao manne na straika wa Pyramids, Fiston Mayele amecheza dakika 39.

Kama atacheza mechi hiyo mabeki wa Stars wanapaswa kumchunga nyota huyo wa zamani wa Yanga kwani anawafahamu vizuri akiwa amewahi kucheza Tanzania kwa misimu miwili mfululizo.

INONGA VS FEITOTO, KIBU

Hii ni vita nyingine kwa beki wa Simba na DR Congo, Henock Inonga na mastaa wa Stars, Feitoto na Kibu Denis ambao anacheza nao Ligi Kuu Bara. Kama wote watacheza mechi hiyo huenda ikashuhudiwa vita kutokana na kujuana vyema kwenye Ligi Kuu.

MAKOCHA WAFUNGUKA

Nyota wa zamani wa Yanga na Stars, Charles Mkwasa alisema timu zote nne katika kundi F bado zina nafasi ya kwenda hatua inayofuata akiwataka wachezaji kutoridhika na bao kama watakalolipata dhidi ya Zambia.

“Kikubwa timu iongeze usahihi. Congo tunajuana nao vizuri haitakuwa mechi ya kitoto na nimeona kuna tofauti na kiuchezaji kuanzia mechi ya kwanza na hii ya juzi,” alisema Mkwasa ambaye aliwahi kuinoa Ruvu Shooting.

Beki wa zamani wa Yanga na Stars, Wiliam Mtendawema alisema kuna nafasi moja tu ili kwenda hatua ya 16 bora ambayo ni ushindi wa pointi tatu huku akiombea Zambia ifungwe na Morocco.

“Nikitazama wenzetu Congo wanavyocheza inabidi tubadilike sana la sivyo tutaishia kujifunza tu. Kikubwa wachezaji wetu wachangamke wakijua hii ni fainali,” alisema Mtendawema.

Mitandaoni mashabiki wanaamini kwamba Stars ikiongeza juhudi zaidi ya ilivyofanya dhidi ya Zambia itapata matokeo ya kuivusha na kuijengea heshima.

Chanzo: Mwanaspoti