Klabu ya Simba ipo kwenye mipango mizito ya kusuka kikosi chake cha msimu ujao kitakachoshiriki michuano ya ndani na kimataifa, huku mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Amri Said ‘Jaap Stam’ akiamini hiki ni kipindi sahihi kwa Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kufanya vizuri na kuipa mafanikio.
Simba tayari imesafisha kikosi chake kwa kuwapa mkono wa kwaheri watu wanne wa benchi la ufundi na mastaa wao Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Nelson Okwa, Mohamed Outtara, Victor Akpan, Beno Kakolanya na Gadiel Michael kupisha majembe mapya yatakayoshushwa.
Stam aliyetwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2009/10 bila kupoteza mchezo akiwa msaidizi wa Kocha Mkuu, Patrick Phiri aliliambia Mwanaspoti kuwa kwa muda ambao Mbrazili huyo amekaa Msimbazi ameshaijua timu yake penye uimara na mapungufu huku akiamini atafanya uamuzi sahihi kwenye dirisha la usajili kupata kikosi bora.
Kocha huyo ambaye kwa sasa anainoa KVZ ya Zanzibar, alisema kutokana na kilichotokea msimu uliopita kwa timu hiyo kuambulia patupu katika mashindano yote iliyoshiriki, anaamini uongozi wa Simba utampa ushirikiano wa kutosha Robertinho kupata majembe bora msimu ujao.
“Kwa muda aliokaa na timu ameshaijua kiufundi nafikiri muda alioupata umetosha kujua changamoto zilizopo ndani ya kikosi chake na benchi lake kwa ajili ya maboresho ya msimu ujao, kuendeleza mazuri aliyoyaona na kuongeza ili mwakani aweze kufika malengo kama klabu ya Simba ilivyojiwekea,”
“Nafikiri mwalimu na benchi watakaa na kupanga nini kifanyike ni jukumu lao kuanzia usajili, kuandaa na kujenga timu imara nina imani na uongozi wa Simba upo imara na bodi na Rais wa heshima Mo (Mohammed Dewji) watampa ushirikiano wa kutosha,” alisema Said
Akiwa na KVZ msimu uliopita aliisaidia kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Zanzibar