Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stam: Fei Toto? Huku wapo kibao!

Fei Toto Final Ligi Feisal Salum

Fri, 30 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa KVZ, Amri Said amesema kama zipo timu za Ligi Kuu Bara zina uhitaji wa viungo na washambuliaji wenye vipaji vikubwa basi amezishauri zifike Zanzibar ambako vimejaa tele.

Tangu atue Zanzibar kukinoa kikosi hicho, alisema ameviona vipaji vikubwa ambavyo kama kuna timu ya Bara inahitaji itume maskauti wa kuvifuatilia na anaamini itafaidika hata kwa kuviuza kwa bei ya juu.

“Viungo kama kina Feisal Salum ‘Fei Toto’ vipo kibao shida timu nyingi hazina uvumilivu wa kuvifuatilia vikianza kujulikana ndio wanaanza kung’ang’aniana, jambo ambalo halisaidii mpira wetu.

“Kama watatokea viongozi watakaoamua kujenga timu yao kwa muda mrefu na yenye ushindani, nawashauri wawe na watalamu watakaotenga muda wao kwa ajili ya kufuatilia vipaji sehemu mbalimbali.”

Alisema kinachotakiwa kwa vipaji vilivyopo Zanzibar hasa viungo na washambuliaji aliowataja ni motisha kutokana na wachezaji hao kucheza kwa kujifurahisha kutokana na maslahi madogo wanayoyapata.

“Kiukweli Ligi Kuu Bara ina sapoti kubwa sana, ndio maana wachezaji wengi wanapata morali ya kucheza kwa bidii, tofauti na huku licha ya vipaji vikubwa ila naona kama maslahi yake yapo chini, jambo ambalo linawafanya wacheze kwa mapenzi na siyo kazi,” alisema.

Amri ambaye timu yake ni kinara wa ligi hiyo ya Zanzibar alisema yapo mambo aliyojifunza baada ya kufundisha Bara na Visiwani anayotamani kuyafanyia kazi ili kutoa mchango wake kuhakikisha soka linasonga mbele.

“Moja ya vitu vikubwa nilivyojifunza ni kufuatilia na kuwa na misingi ya kuwajenga wachezaji kwa sababu soka kwa nyakati hizi lina pesa kwa wachezaji ambao watajituma na kuliona hilo,” alisema.

Chanzo: Mwanaspoti