Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Staili hizi tatu zitambeba Ten Hag

Ten Hag Majeruhi.png Staili hizi tatu zitambeba Ten Hag

Sun, 22 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Manchester United ipo namba 10 katika msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kuanza vibaya wa 2023-2024.

Kulikuwa na matarajio mengi klabuni hapo wakati msimu unaanza, hasa ukizingatia Man United ilikuwa inarejea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kikosi chao kilifanya maboresho kadhaa ya kuleta wakali wapya kwenye timu.

Hata hiyo, kiwango cha hovyo kwenye ligi, sambamba na vipigo mfululizo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kutoka kwa Bayern Munich na Galatasaray vimeacha maswali mengi kwa kocha Erik ten Hag.

Kwa klabu kama Man United, ambayo inapewa nafasi kubwa ya kushindana kwenye kila mashindano inayoshiriki, presha inakuwa kubwa kwa makocha pindi mambo yanapokwama kwenda.

Hata hivyo, bado kuna matumaini makubwa ya kuifanya Man United kurudi kwenye makali yake kama tu, kocha Ten Hag atafanya mabadiliko kadhaa ya kimbinu na uchezaji kwenye mechi.

Makala haya yanahusu staili tatu za kiuchezaji ambazo kama Ten Hag ataanza kuzifanya basi kikosi chake kitakuwa kwenye makali na kurudisha utamu katika timu hiyo ya Old Trafford.

Staili ya kwanza: Kukaba kuanzia juu

Wakati Ten Hag alipopewa mikoba Old Trafford, kulikuwa na mshawasha mkubwa sna kwamba kocha huyo ataleta utamaduni wa soka la kuanza kukabia juu kwenye eneo la mpinzani.

Kuna mambo machache, nje ya kumiliki mpira, mashabiki walianza kushuhudia jinsi timu yake ilivyokuwa ikipambana kuurudisha mpira kwenye umiliki wao kila ilipoupoteza.

Staili hiyo ya kiuchezaji wa kukabia juu mara zote imekuwa ikileta matunda chanya kwa sababu inakufanya kuwa kwenye mazingira rahisi ya kufunga bao kwa kuwa utamnyang’anya mpinzani mpira ukiwa kwenye eneo lake la hatari.

Hata hivyo, staili hiyo inahitaji nidhamu ya kutosha, kwamba timu ihakikisha inakaba na kuhakikisha inachukua mpira ili wasiadhibiwe kwa mipira kupitishwa nyuma yao na kufungwa kirahisi mabao ya kushtukiza. Kwa Man United staili ya kukabia juu inaweza kuwatoa. Man United ina wachezaji wanaofahamu namna ya kutumia nafasi kufunga mabao, hivyo kama watakaba kwa juu na kisha ikapora mpira kwenye eneo la hatari la wapinzani, wataweza kufunga. Staili yao ya kucheza 4-2-3-1, inawafanya kuwa na watu wanne kwenye eneo la kushambulia, hivyo idadi yao inatosha kumbana mpinzani na kufanya jambo.

Staili ya pili: Kucheza zaidi counterattack

Soka la kiwango cha juu, hasa kwenye Ligi Kuu England, kinachoonekana timu zinahitaji zaidi kumiliki mpira kwenye mechi zake na hicho ndicho kinachopewa kipaumbele.

Msimu huu kocha Ten Hag anaonekana kutaka soka la kumiliki mpira kwa kuanzia nyuma kwa kipa, mpira unapanda taratibu hadi kufikia kwenye goli la wapinzani, kitu ambacho kimewagharimu kwa kiasi kikubwa wanaponyang’anywa mpira.

Staili hiyo ya kuanza mpira nyuma inaonekana haiendani na aina ya wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Man United kwa sasa. Mchezaji wao Bruno Fernandes ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi, hivyo kufanya mashambulizi ya kushtukiza (counterattack) kutamaliza tatizo lao, hasa wanamiliki pia wachezaji wenye kasi kubwa kama Rasmus Hojlund na Marcus Rashford. Timu kama Manchester City na Arsenal zinapenda kuutawala mchezo mwanzo mwisho, lakini Man United inaweza kuchagua njia tofauti ya kushambulia kwa kushtukia na kutoboa.

Kucheza kasi, kushambulia kwa haraka na soka la kufanya mashabulizi ya kushtukiza, huo ndio utamaduni wa Man United. Mashabiki wanahitaji kuona hilo ili timu ishinde mechi.

Staili ya tatu: Kuacha kucheza nyuma

Uamuzi wa kusitisha mpango wa kumsainisha mkataba mpya kipa David de Gea na kumsaini Andre Onana hiyo ilikuwa ishara kwamba Man United imepanga kucheza soka lake kuanzia nyuma. Kipa De Gea ni mzuri sana kwa kudaka na kunusa hatari, hana uwezo mzuri wa kucheza kwa miguu. Lakini, Onana, kwa upande mwingine ni mzuri kwenye kuucheza mpira kwa miguu na Ten Hag alimleta kwenye timu yake ili afanane na Ederson wa Manchester City.

Lakini, sasa Onana tangu atue Man United anachofanya ni makosa tu, akiruhusu timu kufungwa mabao ya kutosha na kujikuta akipoteza mpira kwenye eneo lake na kuadhibiwa.

Hii haina maana kwamba Onana ni kipa mbaya, la ila kinachoonekana ni kwamba Man United haikuwa imejiandaa kucheza kwa staili hiyo. Hivyo, kujiweka salama na kuepuka kupoteza mengi zaidi, Man United inapaswa kubadilisha staili ya uchezaji kwa muda kwa kuacha kuanzia nyuma hadi hapo watakapoelewa vyema mfumo huo. Wachezaji wa Man United, Raphael Varane, Victor Lindelof, Casemiro na Christian Eriksen hawana utulivu wa kutosha wa kupokea mpira karibu na goli lao, hivyo jambo hilo limeigharimu sana timu hiyo.

Kipa Onana ana uwezo wa kupiga mipira ya kufika kwenye eneo la kiungo, hivyo anapaswa kuanza kufanya hivyo kuliko kuchezacheza kwenye eneo la nyumba ambalo limewagharimu.

Shida ya Man United ni nini?

Man United inaonekana kushindwa kutambua jambo moja, ifanye nini ndani ya uwanja icheze soka la kumiliki mpira au irudi kwenye mtindo wake kucheza soka la moja kwa moja kwa kushambulia kwa kasi. Ili kurudi kwenye ubora wake na kuvuna pointi zitakazowaweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu England, Man United inapaswa kuchagua kucheza soka lao la miaka yote, kwenda mbele na kutumia kasi, kuliko kutaka kumiliki mpira. Kutaka kucheza soka la kuanzia nyuma na kumiliki mpira muda wote ndipo shida ya Man United. Bado ina kasoro nyingi kwenye kikosi chake, haina wachezaji wenye viwango vya kukaa na mpira muda mrefu kwenye miguu yao. Warudi kwenye staili yao, watatoboa.

Chanzo: Mwanaspoti