USISTAAJABU ya Musa unaambiwa. Tottenham Hotspur imempa ajira kocha Antonio Conte kwa mkataba unaofika tamati 2023, lakini mkataba kama huo wamepewa makocha wanne tofauti klabuni hapo.
Conte alithibitishwa kuwa kocha mpya wa Spurs, Jumanne iliyopita na alitarajia kuwa kwenye benchi la ufundi kwa usiku wa jana Alhamisi kwenye mchezo dhidi ya Vitesse katika michuano ya Ulaya.
Kabla ya Conte, Spurs ilikuwa chini ya kocha Nuno Espirito Santo, ambaye pia alisaini mkataba wa miaka miwili unaofika tamati 2023, kabla ya kufutwa kazi Jumatatu iliyopita baada ya kuiongoza timu hiyo katika mechi 10 za Ligi Kuu England.
Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy alimchukua Nuno kuja kuchukua mikoba ya Mreno, Jose Mourinho - ambaye pia alikuwa na mkataba unaofika mwisho 2023. Mourinho alitua Spurs mwaka 2019 na kusaini mkataba wa miaka minne ungemfanya kuwa na timu hiyo hadi 2023, lakini amefutwa kazi na sasa yupo AS Roma.
Kabla ya makocha wote hao, Spurs ilikuwa chini ya Muargentina Mauricio Pochettino. Baada ya kuonyesha kiwango bora kabisa kwenye kuinoa timu hiyo, Pochettino alisainishwa mkataba wa miaka mitano mwishoni mwa msimu wa 2017-18, ambao ungekwenda kufika tamati 2023.
Licha ya kuifikisha Spurs kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Pochettino alifutwa kazi na sasa ni kocha wa Paris Saint-Germain yenye mastaa kibao akiwamo Lionel Messi.