Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SportPesa yaipongeza Yanga kutinga makundi

Hersi Tarimbaa.jfif SportPesa yaipongeza Yanga kutinga makundi

Wed, 4 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kampuni ya burudani na michezo ya SportPesa imetoa salamu za pongezi kwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga kwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kusota kwa miaka 25 iliyopita na kuitakia kila la kheri kwenye hatua hiyo ili iweze kufanya makubwa zaidi msimu huu.

Yanga ilitinga hatua hiyo ikiwa ni mara ya pili tangu ilipocheza kwa mara ya kwanza mwaka 1998 baada ya kuing'oa Al Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0. Awali iliifunga mabao 2-0 katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili iliyopigwa Uwanja wa Pele Kigali (Nyamirambo), jijini Kigali kisha wikiendi iliyopita ikashinda tena 1-0 ziliporudiana kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Kwa sasa Yanga inasubiri kujua wapinzani watakaocheza nao makundi mara wakati droo ya hatua hiyo itakayofanyika keshokutwa Ijumaa ambapo inaungana na watani zao, Simba walioitoa Power Dynamos ya Zambia kwa kanuni ya bao la ugenini kutokana na matokeo ya jumla kuwa sare ya 3-3.

Kutokana na kitendo hicho cha kutinga hatua hiyo baada ya miaka 25, SportPesa ambayo ndio Wadhamini Wakuu wa klabu hiyo leo imetoa salamu za pongezi na kuitaka kukomaa kwenye mechi zilizopo mbele yao ili kurejea ilichokifanya msimu uliopita ilipofika Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kulikosa taji kwa kanuini ya bao la ugenini kwani matokeo ya jumla ilikuwa ni sare ya 2-2, ikifungwa nyumbani 2-1 na kushinda ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria kwa bao 1-0.

Akizungumza akiwa makao makuu ya ofisi za kampuni hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi SportPesa Abbas Tarimba amewapongeza wachezaji na viongozi wa Yanga kwa kufanikiwa kuingia hatua ya makundi kwenye michuano ya kombe la mabingwa barani Afrika.

“Sisi tukiwa wadhamini wakuu tunafarijika kuona mafanikio ya timu ya Yanga kwa jinsi inavyopiga hatua kubwa katika soka la Tanzania na kimataifa,” amesema Tarimba na kuongeza;

"Tunawatakia kila la heri kwenye mechi zijazo za makundi katika kuipeperusha bendera ya Tanzania. Tunawapongeza Viongozi wakiongozwa na Rais Injinia Hersi Saidi na pia wachezaji wote. SportPesa itaendeleza juhudi zake katika kuunga mkono,kuipa thamini na kuinua sekta ya michezo nchini Tanzania."

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: