Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Southgate majaribuni England

Southgate Uingereza Kocha wa England, Gareth Southgate

Wed, 12 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ngoma ni ngumu. Gareth Southgate kijasho kinamtoka juu ya ufiti wa mastaa wake watano kwenye kikosi cha England kama watakuwa tayari kucheza kwenye mechi yao ya kwanza dhidi ya Serbia kwenye Euro 2024, imeelezwa.

Kikosi hicho cha England maarufu kama Three Lions kitarusha kete yake ya kwanza kwenye michuano hiyo Jumapili hii, ikiwa ni siku tisa tangu ilipochapwa 1-0 na Iceland katika mchezo wa kirafiki uliofanyika uwanjani Wembley.

Kocha Southgate aliwaduwaza mashabiki baada ya kuchagua kikosi chenye wachezaji wasiokuwa na uzoefu mkubwa na kuwaacha mastaa wenye ujuzi wa kucheza michuano mikubwa kama Jack Grealish, James Maddison na Harry Maguire.

Na sasa, atawapanga makinda kama Anthony Gordon, Cole Palmer na Eberechi Eze na sasa timu hiyo inakabilkiwa na majeruhi watano yanayohusu wachezaji wenye uzoefu wa kucheza mechi kubwa na zenye presha kwenye mchezo huo wa soka.

Ripoti zinafichua kwamba Jude Bellingham, Phil Foden, Bukayo Saka, John Stones na Luke Shaw wote watahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina wa afya zao kabla ya mchezo huo wa kuwakabili Serbia.

Kwenye orodha hiyo, wachezaji wote hao ni muhimu katika kikosi cha kwanza cha Southgate wanapokuwa fiti. Na kukosekana kwao kutakuwa pigo kubwa kwa England katika mpango wao wa kuanza kwa kishindo katika mchakamchaka wa kusaka ubingwa wa Ulaya.

Bellingham hakucheza kwenye mechi za kirafiki dhidi ya Iceland na Bosnia & Herzegovina baada ya kuisaidia Real Madrid kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuichapa Borussia Dortmund 2-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika Wembley mwanzoni mwa mwezi huu.

Foden alicheza kwa dakika zote 90 katika mechi hiyo iliyofanyika Ijumaa iliyopita huko Wembley, huku Saka alicheza kwa nusu saa tu, akiwa ametokea benchi baada ya kuwa majeruhi, alipoumizwa mwezi uliopita.

Na beki Stones alitolewa wakati wa mapumziko baada ya kuumia enka. Shaw, amekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu, ambapo aliitumikia timu yake ya Manchester United mechi 15 tu msimu uliopita, kuna uwezekano mkubwa hatakuwapo pia kwenye kipute cha Serbia.

Hiyo ina maana Kieran Tripper ataanza kwenye beki ya kushoto katika mechi hiyo ya Jumapili.

Na wachezaji wengine wanne nao wanaweza kukosa mechi hiyo, jambo linalomwaacha Southgate njiapanda kwenye ishu ya kuchagua kikosi.

Lewis Dunk, Ezri Konsa na Joe Gomez watagombea nafasi ya kuanza sambamba na Marc Guehi kwenye beki ya kati.

Wakati huo, staa wa Chelsea, Palmer atakuwa chaguo muhimu kwenye nafasi ya Bellingham, ambapo atatumika kwenye Namba 10.

Anthony Gordon na Eberechi Eze wameonekana kuwa vizuri kwenye upande wa kushoto, huku Jarrad Bowen atavaa viatu vya Saka kwenye wingi ya kulia. Na Trent Alexander-Arnold anatarajia kuanza kwenye sehemu ya kiungo sambamba na Declan Rice.

Hilo litafanyika bila ya kujali uwepo wa Conor Gallagher, sambamba na viungo makinda matata kabisa, Kobbie Mainoo na Adam Wharton.

Alexander-Arnold amebadili mambo kwenye kikosi hicho na taarifa zikisema: “Mambo mengi yamebadilika, lakini Trent amepewa jezi Namba 8 kwa sababu.”

Chanzo: Mwanaspoti