Kiungo wa timu ya taifa ya England, Jordan Henderson alizomewa na mashabiki wa England aliporejea Wembley baada ya kutimkia Saudi Arabia, huku Kocha Gareth Southgate alishangazwa na kitendo hicho.
Kocha Southgate alimpa kitambaa cha unahodha kiungo huyo anayekipiga Al-Ettifaq katika ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Australia kwenye Uwanja wa Wembley.
Lakini mashabiki wa England walimzomea nahodha wao ambaye analipwa mshahara wa Pauni 700,000 kwa wiki katika klabu yake ya Al-Ettifaq.
Henderson alizomewa baada ya jina lake kutajwa katika kikosi cha England kabla ya mechi kuanza na wakati alipogusa mpira, hata hivyo alifanyiwa mabadiliko kipindi cha pili dakika ya 62.
Mwezi uliopita Henderson alianza kikosi cha kwanza dhidi ya Ukraine, kisha akaanzia benchi dhidi ya Scotland lakini mashabiki walimdhihaki katika mechi yake ya kwanza akiwa kwenye ardhi ya nyumbani na Ollie Watkins alifunga bao la ushindi dakika ya 57.
Southgate alisema: “Kwa kweli sielewi, yeye ni mchezaji wa England na ameichezea mechi 79 mpaka sasa. Kujitolea kwake kwa ajili ya timu ya taifa ni kitu cha kipekee. Jukumu lake ndani na nje ya uwanja ni muhimu sana. Watu waliamua kuzomea lakini sielewi kwa nini. Tuna wachezaji waliovalia jezi za England. Jumanne tutacheza dhidi ya Italia, tuwe nyuma ya timu na kuipa sapoti. Najua hatukuwa katika ubora wetu dhidi ya Australia lakini hiyo ni kutokana na mabadiliko mengi yaliyofanywa na kuwapa wachezaji kazi ngumu sana.
Kesho England itacheza mechi ya kufuzu Euro 2024 dhidi ya Italia katika uwanja wa Wembley huku Southgate akiwa na matumaini ya kushinda mchezo huo muhimu.