Mshambuliaji wa Azam FC, Abdul Sopu amesema kwa sasa wao kama wachezaji wanafanya maandalizi ya kumaliza msimu kwa kushinda mechi zilizosalia huku akimweka kiporo kipa wa Yanga, Djigui Diarra.
Sopu ambaye kwa msimu uliopita aling'ara kwenye fainali ya Kombe la Azam Sport Federation Cup ilipowakutanisha Yanga na Coastal Union kwa kuweka rekodi ya mshambuliaji wa kwanza kumfunga kipa huyo mabao matatu kwenye mchezo mmoja, lakini pia alifanikiwa pia kumfunga mabao mawili kwenye ligi.
Huyu ndiye mshambuliaji ambaye amefanikiwa kumfunga Diarra mabao mengi kuanzia alipotua hapa nchini na wanakutana tena kwenye fainali mkoani Tanga.
Mshambuliaji huyo amesema nje ya maandalizi ya michezo ya Ligi lakini fainali hiyo ataibeba kwa uzito na kuandika historia nyingine akiwa na Azam.
"Sasa hivi tunazingatia sana kushinda mechi mbili za ligi ili tumalize bila ya kufungwa bada ya hapo ndiyo nitaanza kuwaza fainali kwa kuwa kila kitu ni mipango," alisema Sopu ambaye alipoulizwa kama ana mpango wa kumfunga tena Diarra alisema hilo analiweka kiporom kwanza.
Hii inakuwa fainali ya pili kwa Sopu kucheza dhidi ya Yanga baada ya ile ya msimu uliopita ambapo walivaana akiwa anaitumikia Coastal na wakalala kwa mabao 4-3.