Gumzo kubwa kwenye soka Tanzania ni kitendo cha mshambuliaji wa Azam, Abdul Suleiman ‘Sopu kuwa kinara wa kumfunga kipa bora wa Yanga, Djigui Diarra.
Sopu ambaye ni kati ya washambuliaji ambao hawatajwi sana ameshamtungua Diarra mabao matano katika mechi tatu. Alimfunga hat-trick msimu uliopita katika fainali ya Kombe la ASFC wakati akiitumikia Coastal Union katika mechi ambayo dakika 120 ziliisha kwa sare ya mabao 3-3 kabla ya Yanga kutwaa taji hilo kwa penalti 4-1, huku katika ligi mzunguko wa kwanza msimu huu akiitumikia Azam FC hakufunga bao katika sare ya 2-2 kabla ya kumtungua tena kipa huyo katika mechi ya marudiano ya ligi ambayo Yanga iliwalaza Wanalambalamba mabao 3-2.
Mashabiki wamekuwa wakisema Sopu ndiye kiboko ya kipa huyo anayetajwa kuwa bora zaidi hapa nchini kwa sasa kutokana na uwezo wake ambao amekuwa akiuonyesha uwanjani.
Mwanaspoti lilimtafuta Sopu kumuuliza siri ya mateso anayompa kipa huyo raia wa Mali, tofauti na washambuliaji wengine Bongo.
DIARRA NI BORA
Sopu anasema yeye ni mshambuliaji mkubwa ndiyo maana anamfunga kipa bora, lakini hiyo haimaanishi kuwa Diarra ni mzembe ila yeye hujiandaa vyema kufanya makubwa kila anapokutana naye.
Sopu anasema yeye hufanya maandalizi makubwa kwa ajili ya mechi zote bila ya kujali anakutana na timu gani hivyo kumfunga Diarra katika kila mechi wanayokutana tangu akiwa Coastal ni kutokana na maandalizi mazuri anayofanya.
“Hakuna kitu kizuri kama kumfunga kipa bora, hivyo mimi ninamshukuru Mungu nimeweza kufanikisha moja ya ndoto zangu, kila mara nilikuwa naomba Mungu siku moja nipate nafasi ya kuwafunga makipa bora hapa nchini.
“Maandalizi yangu sio kwa ajili ya kucheza na Yanga tu, bali kila mechi najitahidi kufanya kitu kikubwa kwa kufunga kadri niwezavyo, nimepata nafasi ya kumfunga Diarra tangu nikiwa Coastal Union lakini kwangu haijalishi kama nitakutana na Yanga ama Simba, au timu nyingine yoyote huwa natamani kufunga ndiyo maana najiandaa vyema na kwa Diarra labda maandalizi yamekuwa yakilipa zaidi jambo ambalo limekuwa likinipa furaha zaidi,” anasema Sopu.
AWATAJA JOB, KIBWANA
Akizungumzia mabeki wanaompa taabu awapo uwanjani, Sopu anasema kuwa mabeki wote ni bora, ingawa Dickson Job na Kibwana Shomari wa Yanga ni mabeki anaowaheshimu zaidi maana anawafahamu vyema tangu wakiwa Serengeti Boys wamekuwa wakimpa shida kuwapita.
“Mabeki wote ni bora, ila kwangu mimi mechi huwa ngumu nikikutana na Job na Kibwana, kwani tunafahamiana vema tangu tukiwa Serengeti Boys pamoja hivyo nawaheshimu sana ubora wao wakiwa uwanjani.” anasema Sopu.
KIKOSI KINAMFANYA AWE BORA
“Namshukuru Mungu nimerudi uwanjani na kuingia moja kwa moja kikosini, haikuwa rahisi. Nimepambana kuhakikisha naingia kikosini, hii ni kutokana na usajili mkubwa uliofanyika,” anasema.
“Pia nilimisi sana kucheza mpira na kuisaidia timu yangu kutimiza malengo ikiwa ni sambamba na mimi mwenyewe kufikia malengo niliyojiwekea kabla ya msimu kuanza. Mungu ni mwema nimerudi uwanjani na kiwango changu kinarejea kama awali,” anasema Sopu na kuongeza kuwa:
“Nilipokuwa nje ya uwanja kutokana na majeraha sikuwa na wasiwasi wa namba yangu kwani kila mtu ana nafasi yake ya kuonyesha alichonacho, hivyo nilijua wakati utafika na nitaonyesha nilichonacho licha ya timu yangu kuwa na wachezaji wengi wazuri kama Kipre Junior na wengineo.
“Ndoto zangu nilizojiwekea bado zipo kwani mechi bado zipo nyingi, nitapambana kuhakikisha kuwa natimiza kile nilichokipanga ingawa siwezi kusema wazi nilipanga nifunge mabao mangapi maana hayo ni malengo binafsi.”
MAPINDUZI IMEMPA SOMO
Akizungumzia ushiriki wake kwa mara ya kwanza katika Kombe la Mapinduzi na kufunga mabao manne anasema kila timu ilijiandaa vema ndiyo maana walikutana na changamoto iliyowafanya washindwe kufikia lengo la kutwaa taji lakini anamshukuru Mungu ushiriki wake kwa mara ya kwanza umempa funzo fulani.
“Kila timu ilijiandaa vyema mfano ni zile za Zanzibar ambazo zina wachezaji wazuri sana ambao wamezipambania timu zao na mojawapo imetwaa taji hilo la Mapinduzi baada ya miaka mingi kupita lakini kwa upande wangu nashukuru Mungu nimefunga mabao matatu,” anasema Sopu na kuongeza;
“Sisi kama wachezaji tuliumia sana kutolewa katika hatua ya nusu fainali (baada ya kipigo cha mabao 4-1 dhidi ya Singida Big Stars), malengo hayakutimia kwani tulitamani tuchukue ubingwa wa kombe hili kwa mara ya sita ingawa kocha alituambia tusahau yaliyopita tugange yajayo kwani bado Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho vinatusubiri,” anasema Sopu.
MSOSI BUANA
Sopu anasema kuna utofauti mkubwa akiwa katika timu ndogo na kubwa hususani kwenye ishu ya vyakula, kwani alizoea kula wali maharage tofauti na sasa anakula aina yoyote ya chakula anachotaka.
“Uwapo kwenye timu ndogo unakula kinachopatikana tofauti na huku sasa unakula chakula chochote unachokitaka ingawa kwangu mimi chakula changu ninachokipenda zaidi ni ugali nyama choma,” anasema Sopu.
ANGEKUWA MVUVI
“Nisingekuwa mchezaji huenda ningekuwa mvuvi, nyumbani kwetu Kilwa kazi kubwa inayofanywa ni uvuvi wa samaki, vijana wengi nyumbani kwetu shughuli kubwa ya kuwaingizia kipato ni uvuvi,” anasema Sopu.