MSHAMBULIAJI wa Yanga, raia wa Burkinafaso, Yacouba Songne, amesema atautumia mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, kuendeleza kasi ya ufungaji ili kusaka kiatu cha ufungaji bora kinachoshikiliwa na Meddie Kagere wa Simba.
Hadi sasa Songne amepachika mabao sita huku Kagere akiwa na mabao 11.
Akizungumza na gazeti hili jana Songne alisema, licha ya kuwa huu ni msimu wake wa kwanza katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara atapambana kuhakikisha anaisaidia timu yake kuibuka na ushindi katika mchezo ujao dhidi ya Azam FC wakati yeye akifukuzia kiatu cha ufungaji bora.
“Tunaendelea vizuri na mazoezi kwaajili ya mchezo ujao, nipo fiti kwaajili ya kuipambania timu yangu pamoja na kutimiza malengo yangu ya kutwaa kiatu cha ufungaji bora ambacho naamini inawezekana kutokana na ushirikiano ninaoupata kutoka kwa wachezaji wenzangu,” alisema Songne.
Yanga wanaingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya Azam FC baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza bao lililofungwa na Deus Kaseke.