Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Soko la usajili 'halimhusu' Nkane na wenzake

Skudu Moloko Kibabage Sure Boy Kibwana Yanga Soko la usajili 'halimhusu' Nkane na wenzake

Mon, 1 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga iko sokoni nje ya nchi ikisaka mshambuliaji wa kariba ya Fiston Mayele na kiungo mchezeshaji, wakati Simba bado inasaka nje mshambuliaji wa kati baada ya kukosa mtu anayeweza kuvaa viatu vya Meddie Kagere aliyeachwa msimu uliopita na John Bocco, ambaye amekuwa nguzo ya mafanikio kwa muda mrefu, akiitoa kwenye njaa ya miaka mitano bila ubingwa.

Sio Simba na Yanga tu zilizo sokoni nje ya nchi. Azam imeshamleta mshambuliaji kutoka Colombia, Franklin Navarro (24), akiwa ni wa kwanza kutoka taifa hilo la Amerika Kusini kuja kusakata soka hapa Tanzania.

Wako wengine wengi kutoka Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Burundi na hata Afrika Kusini wanaohusishwa na mipango ya kusajiliwa Tanzania. Kwa kifupi karibu klabu zote zinahaha kusajili wachezaji nyota kutoka nje ili ziweze kukabili ushindani unaozidi kunogeshwa na wachezaji kutoka nje.

Na umaarufu wa ligi yetu unazidi kukua kutokana na kuvutia nyota wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia, huku ikishika nafasi ya tano kwa ubora Afrika. Katika ligi kama hiyo huwezi kuwa na wachezaji wasio na viwango vya ubora vya kimataifa.

Hapa ni fedha nyingi zinatumika kusajili nyota hawa wa kigeni ambao nchini kwao hawana ushujaa huo tunaowavisha hapa Tanzania. Wapo waliokuja na wasifu mkubwa lakini wakaondoka kwa dhihaka na kejeli.

Na viongozi wana kila sababu ya kutumia mamilioni ya fedha wanayotengewa na wamiliki au bodi za wakurugenzi kununua wachezaji kwa bei mbaya na kuwapa mikataba ambayo huwakimbizia Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) mara wanapoachwa.

Biashara hii kubwa haihusishi chipukizi wetu wanaopikwa Rungwe mkoani Mbeya, au Kyerwa mkoani Kagera, Urambo mkoani Tabora au pale Kirumba mkoani Mwanza palipozaa nyota kadhaa wa soka Tanzania.

Hawahusishwi kwa sababu wanaonekana hawana viwango vya ubora huo wa kushindana na Mayele, Prince Dube, Luis Miquissone, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Stephane Aziz Ki, Fabrice Ngoma, Gjibril Sillah au Kipre Junior. Kila timu inasaka wachezaji wanaoweza kufikia viwango vya nyota hao, na wasipopata basi angalau wasubiri wawapate kwa mkopo au waachwe.

Kwa hiyo, kwenye klabu zenye misuli ya kifedha kuna wachezaji wanaokuja Tanzania kwa mara ya kwanza, wakati kule ambako ni ahueni kidogo kuna wachezaji ambao wameonekana hawawezi kupambana kwenye klabu zenye fedha lakini bado wana uwezo wa kucheza nchini.

Soko hili letu liko radhi limchukue mchezaji mtumba kutoka klabu zenye fedha, kuliko kuhangaika na vijana wetu. Vijana wetu hawana wa kuwakuza. Wanaposajiliwa na klabu zenye misuli ya kifedha, hutakiwa kuonyesha uwezo wao na wasipoweza huondolewa kwa mkopo usio na vipengele vya kuwarudisha kama watapata soka la kikosi cha kwanza.

Hawasajiliwi kwa sababu wameonekana wana kitu ambacho kinaweza kunakshiwa kikawa kizuri zaidi, bali hichohicho walichonacho wahangaike nacho kupata matokeo mazuri.

Ndivyo wanavyofanya kina Idd Seleman 'Nado', Sospeter Bajana, Feisal Salum 'Fei Toto', Dickson Job, Abdul Suleiman Sopu, Clement Mzize, Lusajo Mwaikenda, Israel Mwenda, Yahya Zayd na Kibu Dennis, wachezaji wazawa ambao wamepambana kiasi cha kuwa sura za kawaida katika vikosi vinavyoanza.

Lakini hali si hiyo kwa wachezaji kama Dennis Nkane, ambaye ameshaanza kuzungumziwa kuwa anatakiwa atolewe kwa mkopo, Crispin Ngushi, Hussein Abel, David Kameta 'Duchu' na wengine ambao wanaonekana wanaweza kufuata njia ya Said Ndemla, ambaye alivundikwa Simba na akaja kuachiwa wakati hanogi tena.

Nyota wengi wazawa tunawavundika. Tunaogopa kuwatoa kwa mkopo kwa kudhani watatudhuru na hatuwezi kukuza vipaji vyao kwa sababu hatuna program za vijana zinazoweza kuwakuza.

Leo hii kuna mashindano ya wachezaji walio na umri chini ya miaka 20, lakini husikii wale walio kwenye vikosi vya klabu za Ligi Kuu wakishiriki. Kwanini? Kwa sababu hilo ni kundi tofauti na lile linalojumuisha wachezaji wanaoelezewa wana umri huo lakini hawajahi kuitwa timu zao za vijana ili angalau waendelee kukua kimpira.

Hadi Edward Kedar Nketiah, maarufu kwa jina la Eddie Nketiah, anapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha Arsenal, alikuwa ameshaonyesha uwezo wake katika timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 18, na baadaye chini ya miaka 23 na ndipo Arsene Wenger alipomuita kikosi cha kwanza kwa ajili ya safari ya Australia na China kujiandaa kwa msimu.

Akawa akiitwa mara kwa mara kwa ajili ya mechi za michuano ya mtoano hadi alipoanza kuaminiwa na Michel Arteta.

Hapo unaona program zinazoweza kumkuza mchezaji. Arsenal na klabu nyingine kubwa zina vikosi tofauti vya umri kuanzia watoto wenye umri chini ya miaka 12. Kadri mchezaji anavyokua ndivyo anavyopata nafasi katika vikosi vya umri wa juu hadi anapofikia kikosi cha kwanza. Hiki kitu hatunacho na tunadhani kunahitajika mikakati ya ulimwengu mwingine kuweza kuwa navyo.

Kwa timu nyingi zinazoshiriki ligi ya U-20, wachezaji wamekutana kabla ya ligi kuanza na pengine uwanjani wanaitana “father, father” kwa kuwa hawajuani. Nkane hawezi kupelekwa kwenye vikosi kama hivi kwa kuwa havina utaratibu wa kisayansi wa uendeshaji.

Mpaka lini tutakuwa hivyo. Ni kweli tumetoka huko kusiko na utaratibu wowote, lakini tutaendelea hivyo kwa sababu tiumekuta hali hiyo?

Ni lazima pawepo na pa kuanzia ili wachezaji wetu wapate sehemu ya kuwakuza hadi wafikie viwango vya kushindana na hao wageni tunaowasajili kwa mamilioni ya fedha. Ni lazima kanuni ziwekwe za kuzibana hizi klabu ziwe na program za kukuza vijana na si program za kuwafanya eti waonyeshe kwamba wana timu za vijana. Hii haisaidii.

Kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo linapitisha kanuni za uendeshaji mashindano, limekubali kuruhusu klabu kusajili wachezaji 12 wageni, huku 11 wakiruhusiwa kuingia uwanjani, basi halina budi kuzibebesha hizi klabu wajibu wa kulea watoto na vijana. Ndio. Nipe, nikupe.

Kama unataka wachezaji wageni 12, basi uwe na wajibu wa kulea na kukuza vijana na watoto. Tunatamani sehemu ya mabilioni ya fedha yanayotumika kusajili wageni, ibaki humu ndani kukuza na kuneemesha vijana na jamii.

Nchi zilizo kusini mwa Afrika zinazounganishwa na shirikisho la Cosafa, zimefanikiwa katika hili. Wachezaji wengi nyota ni wazawa wa nchi hizo na taratibu klabu na mataifa yao yanaanza kutikisa soka Afrika, wakati Cecafa ambayo ndiyo ya muda mrefu kama shirikisho, inarudi nyuma na mafanikio yake yanategemea wageni kutoka nje ya ukanda wake.

Cosafa wamefanya nini ambacho, Cecafa hatuwezi? Kuwa waaminifu kwenye program zao za maendeleo na ndio maana leo Lesotho kulazimisha sare na Nigeria ugenini imekuwa si ajabu na hatushangai kuona klabu kama Jwaneng Galaxy ikishinda ugenini dhidi ya Wydad Athletic bila ya kuwa na nyota kutoka Cameroon, Nigeria wala Ivory Coast.

Tunahitaji kutoka huko. Kuondoa utegemezi kwa nyota wa kigeni ni kukuza vijana wetu, ni kubakiza rasilimali humu ndani, ni kuongeza ubora wa timu ya taifa na ni kuboresha pia maisha ya Watanzania.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live