Kocha, Arne Slot amefichua kwamba ataachana na Feyenoord mwishoni mwa msimu huu na kwenda kuinoa Liverpool yenye maskani yake Anfield.
Kocha, anayemaliza muda wake Liverpool, Jurgen Klopp kwa sasa yupo kwenye maandalizi ya mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu England, ambapo kikosi chake kitacheza na Wolves huko Anfield, Jumapili.
Na hakuna siri ikiwa imefichuka siku nyingi kwamba Mdachi Slot atakwenda kurithi mikoba yake huko Liverpool.
Licha ya Slot kuwahi kusema huko nyuma kuhusu uwezekano wa kwenda kujiunga na miamba hiyo ya Ligi Kuu England, bado hakukuwa na taarifa rasmi kutoka kwa mabosi wa Liverpool kuhusu dili hilo.
Lakini, Ijumaa kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 alithibitsha mwenyewe kwamba amefikia makubaliano na Liverpool kwa ajili ya kwenda kuchukua mikoba ya Mjerumani, Klopp.
Klabu ya Feyenoord iliposti video kwenye mtandao wa X iliyosema; "Arne Slot zama zake zinakwenda mwisho."
Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari jioni ya Ijumaa, Slot alisema kwamba hana muda atakwenda kutambulishwa kuwa kocha mpya wa Liverpool.
Alisema: "Naweza kuthibitisha nitakuwa kocha wa Liverpool msimu ujao."
Liverpool bado haijatangaza na haijawekwa wazi kama wanasubiri Klopp afikisha mechi yake ya 491, ambayo itakuwa ya mwisho kwenye kikosi hicho cha Anfield.
Ripoti zinafichua kwamba Liverpool imekubali kuilipa Feyenoord, Euro 9 milioni na bonasi ya Euro 2 milioni ili kupata huduma ya kocha Slot.