Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siwa aishauri Yanga  kucheza kwa mipango

B5ce69d740ee5505aa0f40682455f109.jpeg Siwa aishauri Yanga  kucheza kwa mipango

Fri, 21 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KOCHA wa makipa wa Yanga, Razack Siwa amesema ili kuendelea kufanya vizuri katika michezo iliyobaki ya kumaliza msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanahitaji kucheza kwa mipango.

Akizungumza Dodoma baada ya mechi dhidi ya JKT Tanzania juzi, Siwa alisema wachezaji hawatakiwi kuwa na haraka bali kucheza kwa mipango ambayo ni njia pekee itakayowasaidia kufikia malengo waliojiwekea.

Katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya maafande hao uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, matokeo yaliyowafanya kufikisha pointi 61 sawa na vinara Simba ingawa wekundu wa Msimbazi wako nyuma michezo minne.

“Tusiwe na haraka kwasababu tukiwa na haraka kila kitu kinaharibika,” alisema Siwa na kuongeza kuwa kila kitu kinahitaji mipango na utulivu katika kufanya vizuri.

Kocha huyo kutoka Kenya alisema timu imeanza kuelewana ndio maana walicheza vizuri, hivyo ana amini kwa kile walichokionesha mipango yao ni kupambana mpaka mchezo wa mwisho kushinda.

Alijipa moyo kuwa bado wako kwenye mbio za ubingwa na kwamba ni lazima waendelee kupambana na kushinda michezo iliyobaki.

“Nashukuru Mungu kwa kuwa tulichopanga kimetimia, lengo lilikuwa kushinda na kuondoka na pointi tatu nategemea tutafanya hivyo pia katika michezo mingine minne iliyobaki,” alisema.

Naye Kocha wa JKT Tanzania, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ alisema makosa waliyofanya kipindi cha kwanza cha mchezo huo yaliwagharimu na kuwapa nafasi Yanga kufunga mabao mawili.

Alisema kipindi cha pili walifanya marekebisho na kucheza vizuri ila hawakuweza kutumia nafasi walizokuwa wanapata.

Kocha huyo aliwapongeza Yanga kwa ushindi na kwamba wanakwenda kujipanga kufanya vizuri katika michezo mingine iliyoko mbele yao.

“Mpira ni mchezo wa makosa kwa hiyo wametumia nafasi walizopata wakashinda, kipindi cha kwanza hatukutulia wachezaji wangu walifanya makosa ya kibinadamu tukafungwa, hakuna wa kumlaumu tutajirekebisha na kujipanga kwa mchezo ujao,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz