Siku kama ya leo lakini ikiwa ni mwaka 2008, aliyekuwa kocha wa Simba, Krasimir Bezinski alisema katika kikosi chake ana wachezaji sita ambao anaweza kuwatengeza kwa muda mfupi na wakacheza soka katika klabu yoyote ya Ulaya.
"Nina wachezaji sita ambao wanaweza kucheza Arsenal, Lyon, Manchester United na Barcelona," alisema Bezinski ambaye ni shabiki wa Liverpool.
Bezinsiki licha ya kukataa kuwataja majina wachezaji hao ila Mwanaspoti linatambua kuwa nyota hao ni Mussa Hassan Mgosi, David Naftali, Henry Joseph, Moses Odhiambo, Ramadhan Chombo 'Redondo' na Emeh Izechukwu.
Tangu kuwasili kwa kocha huyo wakati huo walikuwa na namba za uhakika katika kikosi chake na maajabu zaidi ni kwa David Naftali kumweka benchi Kelvin Yondani 'Vidic' licha ya nyota huyo kupendwa na mashabiki wa timu.
Bezinski amekuwa akiwapenda sana wachezaji hao mazoezini na wakati mwingine amekuwa akibaki nao uwanjani baada ya mazoezi ili kuwapa mbinu zaidi za kufunga mabao jambo ambalo kipindi hicho lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Akizungumza jijini Dar es Salaam, Bezinski alisema wachezaji hao wanahitaji vitu vichache ili kucheza soka la Ulaya na inawezekana wakafanya hivyo iwapo watapata timu za kuichezea hata kwa msimu ujao. "Nimecheza soka la Ulaya kwa kipindi kirefu," alisema Bezinski ambaye alicheza katika ligi ya Bulgaria mechi 363 akiwa na klabu ya CSKA Sofia kabla ya kucheza ligi ya Ureno michezo 79 akiwa na timu ya Portimonense.
"Najua ili mchezaji acheze ligi ya Ulaya anatakiwa kucheza kwa uhakika katika nchi yoyote barani humo, hawa wangu wanaweza kwa asilimia kubwa kwa sababu hata umri pia unawaruhusu," alisema Bezinski raia wa Bulgaria.
Aliongeza baada ya kipindi cha miezi sita kutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake na anaamini idadi ya wachezaji wake kuwa na uwezo wa kwenda kucheza sehemu yoyote Duniani itaongezeka kwa kiasi kikubwa.
"Kocha lazima awe na malengo na wachezaji wake, sio kucheza ligi pekee lakini je una wachezaji wanaoweza kupiga hatua zaidi na kwenda kwingine, hiyo ni sehemu ya kocha kujivunia," alisema.
Wachezaji wa Simba kipindi hicho walikuwa wakimwagia sifa kocha huyo kutokana na uwezo wake wa ufundishaji hasa kutoa mifano mingi kwa vitendo kama kuuchezea mpira, kukimbia na kupiga krosi au mipira ya adhabu.
Bezinski wakati huo alitua nchini kuchukua nafasi ya Mserbia, Milovan Cirkoviv aliyeondoka na kurejea kwao na baadae kujiunga na Fanja ya Oman.