Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri za Ferguson kutafuna bazoka uwanjani

Ferguson Pic Siri za Ferguson kutafuna bazoka uwanjani

Fri, 30 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Michezo na hasa kandanda ina kila aina ya wazimu na baadhi yao hata mabingwa wa ugonjwa wa akili wa hospitali kama ya Mirembe Dodoma, watashangaa wakisikia simulizi za wazimu huo.

Hivi karibuni nilipofuatilia uhifadhi mazingira uliosababisha Singapore kuwa mfano mzuri wa nchi isiyofanya mzaha na usafi, nilifurahishwa na Manchester United ilipopata kikwazo ilipotaka kutembelea nchi hiyo miaka 15 iliyopita.

Kikwazo hicho kilichotokana na sheria iliyopitishwa Januari 3, 1992 kiliathiri wachezaji zaidi na kocha wa wakati huo, Sir Alex Ferguson, nacho ni kukuta ukiwa unatafuna ubani (bazoka), kuchoma ovyo maua, kutema mate na kutupa vishina vya sigara njiani ni marufuku kwao.

Baada ya mazungumzo Manchester United walikubaliwa kutafuna bazoka, lakini wahakikishe wanahifadhi mabaki na kurudi nayo kwao Uingereza.

Sir Fergeson alikuwa maarufu kwa kutafuna ubani akiwa na timu yake mwanzo mpaka mwisho wa mchezo na kuna wakati alitafuna chembe zaidi ya 20.

Sasa nigusie wazimu mpya wa ubani na kandanda. Hivi karibuni palizuka mjadala katika klabu ya Manchester United kutaka kunadi upya mabaki ya mwisho ya bazoka aliyotupa Sir Ferguson katika mchezo wa kumuaga baada ya kuwa kocha kwa miaka 27 tangu 1986 hadi 2013.

Mchezo huo ulikuwa kati ya Manchester United na West Bromwich Albion na kumalizika kwa sare ya mabao 5-5 katika Uwanja wa Hawthorns.

Mchezo ulipomalizika kijana mmoja aliokota mabaki ya mwisho ya bazoka aliyokuwa anatafuna kocha huyo. Baadaye alionyesha kwenye mitandao bazoka aliyohifadhi na kuiweka mnadani. Hapo ndipo ukaanza wazimu wa kununua na matokeo yake mshindi alikuwa yule aliyetoa Pauni 390,000 za Kiingereza kununua mabaki hayo.

Fedha zilizopatikana ziliingizwa katika mfuko wa kusaidia jamii na sasa kidonge hicho cha bazoka knachohifadhiwa kama almasi kinataka kunadiwa tena ili kupata fedha zaidi. Huu sio wazimu mdogo.

Ukiangalia kwa umakini kandanda iwe uwanjani au kupitia runinga utaona wachezaji, makocha, waamuzi na watazamaji ambao tangu mwanzo hadi mwisho wa mchezo wanatafuna bazoka.

Zipo dhana tofauti za wataalamu wa soka na afya za wachezaji juu ya tabia hii na kwa miaka mingi imekuwa na mjadala ambao haujapatiwa jibu la uhakika.

Katika baadhi ya viwanja ni marufuku wachezaji kutafuna bazoka, lakini sheria haisimamiwi vikali na kwingine watazamaji wanapoingia uwanjani hunyang’angwa paketi za bazoka na wanaotafuna hutakiwa waziteme na kutupwa katika vyombo vya kuhifadhi taka.

Kwa kuwa Watanzania wengi wanafuatilia michezo ya Ligi Kuu England nianze kwa kueleza machache juu ya watafunaji bazoka maarufu wa ligi hiyo. Anayetajwa kama mtafunaji bazoka namba moja hadi sasa ni Sir Ferguson kwani uchunguzi umeonyesha wakati akiwa na Manchester United alitumia paketi za bazoka zaidi ya sita kila moja ikiwa na vipisi sita kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.

Hii ni mbali na zile alizotafuna alipoambatana na timu kwenda uwanjani au katika mazoezi. Mara nyingi Manchester United ilipokuwa karibu kufanya safari ya kwenda uwanjani wapo wachezaji hasa David Beckham waliomkumbusha asisahau paketi zake za bazoka.

Wachezaji wengine wa Uingereza waliosifika kwa kutafuna bazoka uwanjani ni Paul Scholes na Wayne Rooney ambaye pia kama Lionel Messi alipata umaarufu wa kutema mate uwanjani kila mara.

Zipo taarifa kuwa kocha wa zamani wa Brazil, Mario Zagalo alipowataka wachezaji miaka ya 1970 waache kutafuna bazoka waliomba kama ni hivyo waruhusiwe kutokuwemo katika kikosi chake na Zagalo ilibidi asalimu amri.

Watu wengi hujiuliza kutafuna bazoka katika mchezo kuna siri au faida gani? Wapo wataalamu wa afya na michezo wanaosema husaidia kuchangamsha mwili, akili na damu ya mchezaji kutembea vizuri na kupunguza wasiwasi kwenye mchezo.

Tafiti zinaonyesha uwezekano wa anayetafuna bazoka kusinzia uwanjani ni mdogo kuliko yule asiyetafuna kwa vile mwili huwa kazini na haujatulia kama wa asiyetafuna bazoka.

Nilipokuwa mdogo na wenzangu tulihakikisha tunatafuna bazoka tulipokuwa na mchezo wenye ushindani mkubwa. Tulifanya hivyo kwa kuiga wakubwa zetu au kufuata msemo wa “Kiingiacho mjini sio haramu”.

Wapo wanamichezo maarufu wa kandanda, riadha, mpira wa kikapu, kriketi na magongo ambao hutafuna bazoka nusu saa kabla ya kuanza mchezo. Wengine ukitaka kugombana nao ni kuwaomba wateme.

Wapo wanaotumia vitu vyenye kuchangamsha mwili. Kwa mfano, wachezaji wengi wa zamani wa Newcastle United walipendelea kutafuna karatasi za kusafisha mwili baada ya kwenda haja maarufu kama tishu.

Katika picha moja niliyoiona zamani wachezaji wa Newcastle walipokuwa katika chumba cha kubadilishia nguo, meza yao iliwekwa bazoka, juisi na mabunda ya tishu. Nilipouliza kuhusu tishu hizo niliambiwa ni moja ya zana inayotumiwa na wachezaji wanapokuwa uwanjani.

Maelezo yale yalinikumbusha uzoefu nilioupata nilipofuatana na wachezaji wa timu yetu ya taifa. Kwa mfano beki mashuhuri wa Taifa Stars miaka ya nyuma, Mohamed Chuma wa Mtwara alipendelea kula mapera kama saa mbilii kabla ya mchezo.

Siku moja tukiwa Sudan nilimuuliza kama alipata mapera na aliniambia wakati baadhi ya wachezaji wenzake walichukua visheti, keki na vitafunio vingine katika safari yao, yeye alichukua mapera.

Nilipomuuliza kwa nini alipenda kula mapera kabla ya mchezo alicheka na kuniambia:”Sheikh, kwani wewe si mtu wa Pwani, hujui kama mapera yanasaidia kuziba choo.”

Mchezaji mwingine aliyependelea kitafunio cha ajabu ni kipa wa zamani wa timu ya taifa, Juma Pondamali. Huyu ana siri yake katika soka. Nilichogundua siku zote aliingia uwanjani na vipande vya karatasi za gazeti alivyovitafuna mwanzo wa mchezo hadi mwisho.

Anayetaka maelezo zaidi ya mwenedo huu wa Pondamali wakati akiwa kipa makini wa timu ya taifa amulize mwenyewe, lakini naamini atachopata ni Pondamali kuangua kicheko tu kwa vile hapendi kuzungumzia hili. Nichukue nafasi hii kuwaomba waandishi wa habari na mashabiki wa kandanda wachunguze - wapo wachezaji wangapi katika kila mchezo wanaotafuna ubani.

Chanzo: Mwanaspoti