Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri yafichuka rundo la kesi za Yanga FIFA

Hersi Zqew.jpeg Eng. Hersi Said

Fri, 21 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dirisha jipya la usajili kwa ajili ya msimu ujao wa mwaka 2024-2025 limefunguliwa tangu Juni 15, huku kukiwa na sintofahamu kwa timu tano ikiwamo mabingwa wa Tanzania, Yanga.

Timu za Yanga, FGA Talents, Tabora United, Singida Fountain Gate na Biashara United zimejikuta matatani kwa kufungiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kufanya usajili wa nje na ndani kutokana na kushindwa kutimiza malipo ya baadhi ya wachezaji walioachana nao.

Hii ni mara ya kwanza kwa soka la Tanzania kutokea timu nyingi kwa kiwango hicho, kufungiwa kwa wakati mmoja na shirikisho hilo.

Hata hivyo, hali hii inatokea wakati ambapo wachezaji wengi wamekuwa wakivutiwa kuja kucheza soka Tanzania kutokana na umaarufu wa ligi na ushiriki wa klabu zake kwenye michuano ya kimataifa.

Yanga ndio timu pekee imetoka hadharani na kutoa taarifa kuwa ilishawalipa wachezaji walioishtaki Fifa akiwamo Lazarous Kambole  na Mamadou  Doumbia ambao walijiunga na timu hiyo msimu uliopita.

Hata hivyo, misimu miwili mfululizo tatizo la timu kufungiwa na Fifa limekuwa kubwa zaidi hapa nchini kutokana na baadhi ya wachezaji kutolipwa mahitaji yao huku sababu kadhaa zikionekana kuchangia.

WACHEZAJI KUCHEMSHA

Wachezaji wengi ambao wamekuwa wakiizishtaki klabu Fifa ni wale ambao hawakupata nafasi ya kutosha klabuni, lakini wengi umri unakuwa umekwenda.

Hii inatokea baada ya mchezaji kushindwa kutimiza malengo ambayo anakuwa anapewa na klabu yake ikiwa ni pamoja na kupata nafasi lakini akiwa amekula nusu tu ya hela ya usajili anayokuwa wamekubaliana.

Iko hivi! Wachezaji wengi wanaosumbua kwa sasa ni wale ambao walisajiliwa wakiwa huru, hivyo makubaliano ya fedha ya usajili hufanya wenyewe na klabu zao na mara nyingi hulipwa mara mbili au tatu kulingana na jinsi ambavyo wamezungumza.

Kama mchezaji atatakiwa kulipwa 50 milioni kwa miaka miwili, mara nyingi fedha hizi hugawanywa mara mbili, anaposaini hupewa 25 milioni na zinazobaki anatakiwa kupewa mwaka wa mwisho wa mkataba wake.

Kinachotokea ni kwamba mchezaji husika kutokana na kiwango chake kushindwa kuiridhisha klabu, anaachwa kabla ya kumaliza mkataba wake akiwa bado anaidai klabu nusu ya fedha zake za usajili. Hapa danadana huwa zinaanza kati ya mchezaji na klabu na mwisho anakimbilia Fifa kushtaki.

Hii inatokea baada ya klabu kusajili mchezaji bila kufuatilia anachofanya kwa wakati husika au anapewa historia yake ya nyuma.

Mchezaji huyo anapotua kwenye timu huanza kwa kasi ya chini na baada ya miezi miwili au mitatu hukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza au anakuwa na majeraha ya kudumu.

Hii mara nyingi hawalazimisha mabosi wa klabu kuachana naye baada tu ya dirisha la usajili kufunguliwa bila kujali ametumika kwa muda gani.

SKAUTI MBOVU

Timu nyingi zimekuwa zikisajili wachezaji wa kimataifa kwa rekodi za nyuma kwa kuwa hazina watu wazuri wa kuwafuatilia wachezaji na bajeti ndogo.

Mara nyingi timu zimekuwa zikifanya usajili kwa kukumbuka mchezaji flani alifanya nini misimu mitatu nyuma, badala ya wakati husika au anaweza kuwa na uwezo lakini klabu hazina muda wa kusubiri awe bora.

Kwa kuwa wachezaji wengi ambao wanasajiliwa wengi wanakuwa ni wale ambao wanatoka kwenye baadhi ya timu kubwa Afrika ni wale ambao wanakuwa wamekaa nje muda mrefu hivyo kushindwa kuendana na kasi ya wakati husika.

DHARAU:

Baadhi ya wachezaji wamekuwa wakilalamika kuwa baada ya kuachwa na klabu husika huamua kukimbilia Fifa baada ya mabosi kugoma tena kupokea simu zao ili kuwaeleza watalipwa vipi fedha zao zilizobaki.

Hii imekuwa ikichangia hata wakati mwingine wachezaji wale kurudi kwenye klabu zile kwa gia ya kujiweka fiti lakini ni njia ya kuhakikisha wanawapata mabosi wa timu hizo ili kuzungumzia kuhusu fedha zao, kulazimisha kubaki hapo ili walipwe, jambo ambalo wakati mwingine limekuwa likifanyika na wakati mwingine kushindikana.

MICHONGO YA WATU

Hawa ni wale wachezaji ambao wakati mwingine wanakuwa na uwezo mkubwa lakini wanakuwa wamesajiliwa na baadhi ya marafiki wa klabu au baadhi ya viongozi wa timu bila kufuata utaratibu mzuri wa klabu.

Sasa mara nyingi, aidha mchezaji anashindwa kufanya vizuri yule bosi anakasirika na kugoma kumlipa fedha zake au, huyu mtu anashindwana na baadhi ya viongozi na kuamua kususa suala la kumlipa mchezaji huyo.

Hapa mchezaji akienda kwa viongozi anaambiwa amtafute jamaa aliyemleta klabuni na akimpigia au akimpata jamaa anamwambia waambie klabuni wakulipe, mwisho wanashindwana anakimbilia Fifa.

“Sisi msimu huu tumepata tatizo la barua kwa wachezaji watatu, lakini hawa wawili walisajiliwa na watu walitaka kutusaidia baada ya kuona timu haifanyi vizuri wakaamua kugoma kuwalipa.

“Ukweli hatukuwa na bajeti nao hivyo tuliamua kuachana nao wakaenda kutushtaki ndiyo shida ambayo tunakutana nayo, nafikiri tumejifunza msimu ujao tutasajili kulingana na kila tulichonacho,” alisema kiongozi mmoja wa klabu.

KUSHTUKIZWA NA WALIOPO

Klabu nyingi zimekuwa zikiona kama ni fasheni kusajili wachezaji  12 wa kigeni ambao wanatakiwa na kanuni jambo ambalo limekuwa likiwapa mzigo mzito.

Lakini wachezaji hawa wengine wanapokuja hukuta baadhi ya wazawa kwenye nafasi zao ambao ni bora zaidi kuliko wao, hilo limekuwa wakati mwingine likiwafanya wakae benchi na mwisho klabuni kuona ugumu wa kuwalipa kile ambacho walikubaliana na kuwaacha, baada ya hapo wachezaji hao hukimbilia Fifa kudai haki yao.

Mfano mkubwa ni Doumbia katika kikosi cha Yanga, alisajiliwa Yanga na kukutana Ibrahim Bacca, Dickson Job na Bakar Mwamnyeto wana ubora wa juu zaidi yake na anakosa nafasi ya kucheza.

TFF YAKOMAA

Mara baada ya taarifa ya TFF juu ya kufungiwa kwa klabu hiyo, uongozi wa Yanga ulijitokeza na kudai ilishamalizana na wachezaji hao na kwamba hawadaiwi, lakini muda mchache baadaye shirikisho hilo liliweka wazi ikizikomaliza klabu hizo zijue zipo kifungo hadi Fifa ikakapozifungulia.

Katika taarifa ya ya juzi jioni, TFF ilisema Fifa ndio pekee wenye uwezo wa kuzifungulia klabu hizo na baada ya walioshtakia kuwathibitishia kwamba wameshamalizana na klabu husika.

"Kwa mujibu wa utaratibu wa Fifa mdai anatakiwa kuthibitisha kupokea malipo ndani ya siku tangu baada ya mdaiwa kufanya malipo husika," ilisomeka taarifa hiyo ya TFF iliyosainiwa na Ofisa Habari, Cliford Ndimbo na kuongeza;

"Iwapo mdai atathibitisha  kupokea malipo yake, ndipo Fifa itaiondolea klabu husika adhabu ya kufungiwa kusajili. TFF itaendelea kutoa taarifa klabu zote zilizofungiwa na zile zitakazokuwa tayari zimefunguliwa na Fifa baada ya kuwalipa wahusika."

WASIKIE WADAU

Beki wa zamani wa Yanga na Stars, Bakari Malima 'Jembe Ulaya' alilishauri TFF, kutoa semina elekezi kwa timu nje na Simba, Yanga na Azam FC ili kujua madhara ya kudaiwa na wachezaji wazawa na wageni.

"TFF wamefanya kazi kubwa ya kuifanya Ligi ya Tanzania kuwa bora Afrika, hiyo tabia iliyoanza ya kudai wachezaji mara kwa mara ni mbaya, inachafua taswira ya soka letu, nimeshangaa kuona timu nje ya Simba, Yanga na Azam nazo zimeingia kwenye mkumbo huo wa kusajili wachezaji wa kigeni, halafu wanashindwa kuwalipa," alisema Malima na kuongeza;

"TFF lisipotolea macho jambo hilo, wachezaji wazuri kutoka nchi mbalimbali watakuwa wanaogopa kuja kucheza Tanzania, wataona viongozi wa timu wamejaa utapeli, hivyo siyo jambo la kulichekelea hata kidogo."

Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema, suala kubwa analoliona kwa klabu zetu kudaiwa ni kushindwa kuzingatia mikataba wanayoingia na wachezaji husika jambo ambalo linawaletea taswira mbaya na kujikuta zikifungiwa.

"Kwa mtazamo wangu naona shida ni kutozingatia zaidi suala la mkataba kwa sababu kuna vipengele vingi ambavyo vinaweza kukulinda wewe kama kiongozi ili mwisho wa siku usiingie matatizoni na wachezaji na hata kuisababishia klabu kufungiwa."

Chambua aliongeza, hata kama mchezaji ana kiwango kizuri na una imani kwake unaweza ukaingia mkataba wa muda mfupi ambao hauwezi kukufunga kutokana na kipato kinachoingia kuliko kujiweka matatizoni unaposhindwa kumlipa stahiki zake zote.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live