Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri ya ushindi Yanga ipo hapa

Ben Morisson Al Winga Bernard Morisson akiwatoka wachezaji wa Al Hilal

Fri, 14 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Japokuwa kuna baadhi ya mashabiki wa Yanga wanaonekana kuikatia tamaa timu yao juu ya kupindua meza mbele ya Al Hilal katika mechi ya marudiano ugenini, lakini benchi la ufundi na nyota wa zamani wa klabu hiyo wamesema lazima kieleweke, huku nyota wa timu wakipewa kazi maalumu kuivusha .

Yanga ina mlima mrefu ugenini dhidi ya Al Hilal baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani, huku rekodi zikionyesha Wasudan wanapokuwa nyumbani kwao huwa wagumu kufungika, pia, vibe la mashabiki wao uwanjani mwanzo mwisho huchangia kuwaangusha wapinzani wao uwanjani.

Hata hivyo, Kocha Nasreddine Nabi ambaye si mgeni Sudan baada ya kuwahi kuifundisha timu Al Merrikh, alisema anajua ana kazi kubwa ugenini, lakini anaamini vijana wake watapambana kadri ya uwezo wao na kupindua meza kwenda makundi.

“Ni kazi ngumu, lakini liwalo na liwe, lazima tusonge mbele kwani kama wao waliweza kupata sare kwetu, hata sisi tunaweza kushinda ugenini kwa sababu tuna timu imara na bora,” alisema Nabi.

Wakati Nabi akiyasema hayo, nyota wa kikosi hicho akiwamo Fiston Mayele, Bernard Morrison, Feisal Salum na Stephane Aziz KI wamepewa kazi maalum ili kuibeba timu kwenye mechi hiyo ya ugenini itakayoamua hatma ya Yanga kutinga makundi ama kwenda Kombe la Shirikisho Afrika.

Mayele mwenye mabao saba ya Ligi ya Mabingwa Afrika, akifunga hat-trick mbili dhidi ya Zalan kabla ya kufunga jingine moja katika sare ya 1-1 na Al Hilal, anatazamwa kama nyota aliyeibeba Yanga mabegani kwenye mechi hiyo ya ugenini, kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao katika mazingira magumu.

Mbali na Mayele, pia Aziz KI aliyesajiliwa kutoka ASEC Mimosas ilipokuwa imecheza dhidi ya Simba, Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo wasifu (CV) wake unawafanya wadau kuamini atakuwa msaada mkubwa kwa timu yake ikiikabili Al Hilal huko Sudan.

Pia, kiwango cha Bernard Morrison kwenye michuano ya CAF, kinatajwa kama mchezaji muhimu zaidi ndani ya kikosi hicho, akitarajiwa atakuwa chachu ya kuibeba Yanga, wengine ni Khalid Aucho, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Djigui Diarra na Geal Bigirimana wote wamepewa kazi maalumu kuivusha Yanga.

Ingawa Kocha wa Al Hilal, Florent Ibenge jicho lake ameliona kwa Mayele na kusema ni mchezaji hatari zaidi kwenye kikosi cha Yanga na alikiri kumhofia, kutokana na uhodari wake wa kucheka na nyavu.

WASIKIE WADAU

Mshambuliaji wa zamani Yanga na Timu ya Taifa, Taifa Stars, Herry Morris alisema hata ikitokea Mayele amekabwa vilivyo bado Yanga ina wachezaji watakaoamua mechi.

Morris alisema Yanga ina Fei Toto (Feisal Salum) na KI (Aziz) ambao wote wanaweza kuipa matokeo timu.

“Kikubwa utulivu tu unahitajika na kupeana pasi za maana, Mayele ni mchezaji mzuri na anafunga ila muda mwingine anapoteza utulivu na kushindwa kutumia nafasi nyingi anapokuwa uwanjani,” alisema Morris aliyewahi kutamba na Tanzania Prisons.

Kocha wa zamani Biashara United, Aman Josiah alisema Feisal Salum na Aziz KI wote ni wazuri ambao wanaweza kuibeba Yanga.

Josiah alisema KI haya ndio mashindano yake licha ya kwamba hakuwa katika kiwango kizuri katika mchezo uliopita.

“Hata kama hakuwa kwenye kiwango kizuri haimaanishi KI ni mchezaji mbaya, ni mchezaji mzuri na haya ni mashindano yake,” alisema Josiah na kuongeza;

“Yanga kwasasa inahitaji iwape hamasa wachezaji wake tu, uwanjani wapo vizuri na hawana majeruhi.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live