Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri ya makali ya Azizi KI

Aziz KI Mpira Siri ya makali ya Azizi KI

Wed, 25 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mpaka mseme, bado hamjasema. Moja kati ya wachezaji bora wa ligi yetu kwa sasa ni Stephen Aziz KI. Karibu kila kitu anachofanya uwanjani kinageuka kuwa madini.

Karibu kila kitu anachofanya uwanjani kinageuka kuwa dhahabu. Tangu kuondoka kwa Fiston Mayele na Feisal Salum ni kama Yanga ilikuwa haina mfalme. Ni kama kiti cha ufalme wa Jangwani kilibaki wazi.

Kuna uwezekano mkubwa ujio wa Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua kumemuamsha Aziz KI. Wakati mwingine kwenye maisha unahitaji kumpata mtu anayekukimbiza. Inapendeza maishani kuwa na mtu anayekupa presha nyuma yako. Nzengeli alianza kuimbwa kuanzia tu mechi yake ya kwanza Siku ya Wananchi.

Pacome alichelewa, lakini alipokuja aliingia na taji lake la ufalme. Miguu yake ni burudani tosha. Akili yake ni Zidane kabisa wa Ivory Coast. Ni mchezaji mwenye kila kitu uwanjani.

Aziz KI ameamka tena. Anajaribu kuwaonyesha Wananchi ni kwanini usajili wake ulikuwa gumzo nchini.

Anajaribu kuwakumbusha watu ni kwa nini alitambulishwa saa tisa alfajiri. Hakuna ubishi, Stephen Aziz KI ni mmoja wa wachezaji bora kwenye ligi yetu msimu huu. Ni mchezaji aliyezaliwa upya. Mabao yapo. Udambwidambwi upo. Matobo yapo.

Nadhani anatakiwa kutambulishwa tena. Nadhani anatakiwa kupokewa upya pale Julius Nyerere International Airport. Aziz KI atambulishwe upya au inatosha? Usinipe jibu.

Tayari anaongoza kwenye orodha ya wafungaji bora mpaka sasa. Mabao sita tayari yameshatinga kambani kutoka kwenye miguu yake.

Huyu ndiye kiungo mshambuliaji aliyetambulishwa saa tisa alfajiri. Kuondoka kwa Mayele na Feisal pia kuna namna kumefanya Yanga kila mtu ajione mfalme.

Feisal ni kama alikuwa mfalme wa wachezaji wazawa huku Mayele akiwa mfalme wa wote.

Yanga msimu huu kila mtu staa. Kila mtu mfalme. Kuna namna ambavyo karibu kila mchezaji amebadilika.

Ni wakati sasa wa Stephen Aziz KI kugeuka na kuwa mfalme mpya wa Jangwani.

Nadhani ameona akichelewa tu kidogo Yao Yao, Nzengeli na Pacome watamuacha mbali. Kwa sasa pale Jangwani kuna vita ya ufalme wa boma.

Kwa namna unavyowatazama pale unadhani nani anakwenda kuwa mfalme mpya wa Jangwani? Naomba maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu pale juu.

Kwa zaidi ya miaka 10 Shomary Kapombe wa Simba amekuwa akilinganishwa na mabeki wote wa kigeni wanaokuja nchini, lakini hajawahi kushindwa. Kapombe ameendelea kuwa beki bora kwa zaidi ya miaka 10 hapa nchini, lakini nadhani safari hii amekuja mtu sahihi wa kushindanishwa naye.

Yule Yao pale Yanga sio poa. Ni mtu na nusu. Ana uwezo wa kufanya kila kitu uwanjani. Ni mchezaji mwenye kasi, nguvu, ufundi, uwezo wa kupanda na kushuka. Nadhani huyu anaweza kuja kuwa mfalme mwingine wa mabeki wa pembeni hapa nchini. Sio mchezaji wa kawaida. Ana kitu cha ziada.

Ni aina ya wachezaji wanaowania taji la ufalme pale Jangwani sema tu nafasi anayocheza ni ngumu kuwapita watu kama Aziz KI, Pacome na Nzengeli lakini anastahili kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowania ufalme pale Yanga.

Naitazama Yanga inavyocheza napata ugumu wa moja kwa moja kumtambua mfalme wao.

Najua na wewe unawafuatilia na huenda tayari umemuona mfalme mpya wa Jangwani.

Kama tayari unamjua tafadhali naomba usisite kunijuza kwa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Ushindani ni mkubwa sana ndani ya Yanga wenyewe pengine kuliko hata nje. Hata orodha ya wafungaji bora inakuonyesha hilo kwenye wachezaji watano wenye mabao mengi, Yanga ina wachezaji watatu. Ukiondoa Jean Baleke wa Simba mwenye mabao matano na Feisal Salum mwenye mabao manne, pale Yanga yupo Aziz KI mwenye mabao sita, Pacome matatu na Nzengeli matatu. Yanga kumekucha.

Nimetazama mechi yao dhidi ya Azam FC. Ilikuwa dume sana. Ilikuwa ni mechi ya kibabe sana. Ilihitaji wachezaji wakubwa kuiamua. Feisal Salum aliupiga mwingi sana. Nimerudia tena kuitazama, Aziz KI aliupiga mwingi sana. Mechi kubwa wakati mwingine inahitaji wachezaji wakubwa.

Bado napata kizunguzungu kumpata mfalme wa Jangwani. Najua na wewe unafuatilia. nani anastahili kuwa mfame mpya wa Yanga? Naomba maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi wa Maandishi kupitia namba Yangu ya simu hapo juu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: