Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri ya kikosi kipya Yanga inakwama hapa tu!

77938 Yanga+pic

Tue, 1 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania kwa sasa kwenye michuano ya kimataifa, Yanga imehama siti, imetoka Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kunyooshwa na Zesco United ya Zambia mabao 2-1 juzi Jumamosi.

Katika mchezo huo wa marudiano uliopigwa mjini Ndola licha ya Yanga kucheza vyema dakika 90 ilijifunga bao kupitia kiungo wake fundi wa mpira, Abdulaziz Makame lililowasaidia kuwavusha wenyeji kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Kipigo hicho kiliifanya Yanga kutolewa kwa ujumla ya mabao 3-2 baada ya mchezo wa kwanza kutoshana nguvu ya sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam na sasa inasubiri kujua itacheza na nani kwenye hatua ya play-off ya Kombe la Shirikisho.

Tuangalie sasa kwa kina kwani Yanga inakwama wapi mpaka inakutana na wakati mgumu wa kurejea kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya pili?

YANGA BADO HAIJAIVA

Kinachoitafuna Yanga ni kuchelewa kuanza maandalizi ya msimu mpya, kazi ambayo iliifanya kambini Morogoro haikukamilika kama ilivyotakiwa. Na matatizo haya yanatokana na ujio wa haraka wa mashindano ya Afrika, pia kuchelewa kwa Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera, sasa timu hiyo inamalizia kazi ya kuundwa ikiwa katika mashindano.

Pia Soma

Advertisement
Hatua ya kwanza Yanga itajiulaumu kwa jinsi inavyocheza nyumbani, kwani mara nyingi matokeo ya kuitoa au kufuzu huyapatia ugenini na sio nyumbani.

Hivi karibuni tu, Yanga ilikutana na timu mbili za Zambia ikitangulia kukutana na Zanaco ikatoka nayo sare nyumbani ya bao 1-1 wageni wakichomoa, ilipoenda Zambia ikatoa suluhu na Zanaco ikafuzu hatua ya makundi kwa faida ya bao la ugenini katika mchezo ambao Yanga ilicheza vyema sana ugenini.

Historia hiyo ikajirudia tena ilipoitoa Township Rollers ya Botswana, hapa nyumbani Uwanja wa Taifa, Yanga haikucheza vizuri na kulazimisha sare ya bao 1-1, ugenini ilishinda bao 1-0 jijini Gaborone na kufuzu.

Wiki mbili zilizopita tena hilo ikashindwa kushinda nyumbani dhidi ya Zesco, ikipata sare ya bao 1-1 tena ikicheza soka la kawaida lakini ilipokwenda ugenini ikachezwa soka zuri lakini ikang’oka.

Yanga lazima itafute tiba ya mechi za nyumbani kwa kuwatengeneza kisaikolojia wachezaji wake lakini pia mashabiki wao nao huwapa presha wachezaji wao na kushindwa kuonyesha soka la ushindi.

MAKOCHA WANA KAZI

Benchi la ufundi la Yanga sasa linatakiwa kutulia zaidi kuthibitisha ubora wake kutokana na kuwa na kazi kubwa katika kujenga timu yao.

Yanga msimu huu ina kikosi kipya ambacho kupata sayansi ya haraka bado inawapa shida makocha na hili linachangiwa na kushindwa kutumia vyema suala la muda katika kujiandaa na msimu mpya.

Kinachowapa mzigo mzito ni makocha hawa waliosajili wachezaji hao, wanachosubiri watu wa mpira ni kuona kazi ya kuwaunganisha inafanyika kwa haraka ingawa pia haiwezi kuwa ya haraka sana kutokana na mpira kupata timu kamili linahitaji muda zaidi.

MASTRAIKA WAJIPANGE

Ushindi unahitaji mabao hatua ambayo inaikwamisha Yanga kutokana na kupata ushindi mwembamba tofauti na nafasi wanazozitengeneza. Angalia msimu huu Yanga imefunga mabao manne katika mechi nne lakini kati ya hayo ni bao moja tu limefungwa na shambulizi mengine yote yamefungwa kwa adhabu ndogo na kubwa.

Hii ni changamoto kwani ugumu kwa wachezaji unaanzia hapa ni lazima makocha watulize akili kuhakikisha wanawapa mbinu zaidi wachezaji wao, lakini wachezaji pia wanatakiwa kutambua thamani yao kwa kutumia nafasi.

ZAHERA PRESHA NYINGI

Timu inapokosa matokeo mazuri mtu wa kwanza anayekuwa katika wakati mgumu ni kocha mkuu, hali hiyo inawezekana ipo kwa Zahera ambaye anapaswa kuwa hivyo kutokana na kuwa ndiye aliyesimamia mchakato wa usajili.

Aliwaaminisha watu mambo makubwa mengi yanakuja. Kitu kibaya zaidi Zahera i alijua ahadi hiyo anawapa watu wa Ulaya anakoishi, hakujua hapa ni Tanzania na hasa Yanga ambako hakuna uvumilivu wa mambo ya soka, hata kama wanakupenda wakichoka watakulaumu na kukukimbiza.

Kinachohitajika kwa Zahera ni kuongeza utulivu katika majukumu yake na katika kuondoa hilo Yanga inapaswa kushinda bila mateso.

WASIKIE WADAU

Mchambuzi na Mjumbe wa Kamati Mpya ya Ufundi ya Yanga, Ally Mayay alisema shida ya Yanga msimu huu ni kushindwa kuwa na maandalizi bora ya mwanzo wa msimu.

Mayay alisema hatua ya Zahera kuchelewa kujiunga na timu hiyo ilimnyima nafasi ya kuweza kuwasoma wachezaji wake na sasa kazi ya kumalizia kuunda timu inafanyika wakati wa mashindano.

“Msingi mkubwa wa anguko la Yanga upo hapo, kama mnakumbuka timu ilikuwa chini ya kocha msaidizi kule Mwandila (Noel) kuna kazi nzuri alifanya lakini bado haikutosha, timu ilimhitaji zaidi Zahera,” alisema Mayay.

“Bahati mbaya Zahera akachelewa, kinachomtesa sasa ni kuwaunganisha baadhi ya wachezaji wakati wa mashindano, muunganiko wa timu unafanyika wakati wa mashindano kitu ambacho kinawaumiza.”

Mayay alisema shida nyingine ni kukosa utulivu kwa washambulaiji na viungo kuziba nafasi ya Ibrahim Ajibu aliyetimkia Simba bada ya kumalizika kwa mkatba wake na Heritier Makambo aliyeuzwa Guinea.

“Kule mbele na viungo wao bado hakujatulia kuna changamoto kubwa kitu kibaya zaidi hakuna ambaye ameweza kuthibitisha nani anaweza kuwa na ubora wa kuziba pengo la Ajibu pia hata Makambo.

“Hili hata Simba lilitokea angalia baada ya kuondoka kwa Okwi (Emmanuel), kuna wakati wanaona kama pale angekuwepo mambo yangekuwa mazuri sasa na Yanga nako linatokea, hakuna ambaye ameweza kuwa na ubora wa kupiga pasi kama Ajibu lakini pia nani ana jicho la mabao kama Makambo kwasasa? Kule nyuma hakuna shida wako sawa.”

Aidha Mayay alisema wachezaji wa Yanga wanatakiwa kubadilika kiakili wanakosa matokeo nyumbani wataenda kufanya kweli ugenini.

“Kuna akili kama ile ya Simba kwamba hawataafuti ushindi ugenini wakidhani watashinda nyumbani, kuna wakati mambo yanakuwa magumu, Yanga nako linatokea hili, wachezaji hawajitumi wanapokuwa nyumbani wanadai watashinda ugenini, hii linatakiwa kufanyiwa kazi kisaikolojia sasa.”

Chanzo: mwananchi.co.tz