Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri ya Maradona kuvaa saa mbili

Maradona Saa Siri ya Maradona kuvaa saa mbili

Sat, 23 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Diego Maradona. Jina mashuhuri kwenye soka. Ni miongoni mwa majina yanayotajwa kwenye orodha ya wanasoka bora wa muda wote. Soka lilitendewa haki na staa huyo wa Kiargentina.

Nje ya uwanja, Maradona alipata umaarufu mkubwa kwa kuvaa saa mbili, jambo ambalo liliibua maswali mengi. Kwanini avae saa mbili?

Saa zake mbili, moja alivaa mkono wa kulia na nyingine mkono wa kushoto. Kulikuwa na maelezo kwamba, Maradona anavaa saa mbili kwa wakati mmoja anapokuwapo safarini.

Lakini, swahiba wake, supastaa wa Kibrazili, Ronaldo de Lima anafichua ukweli wa jambo hilo, kwanini Maradona alikuwa akivaa saa mbili. Maradona alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 60, Novemba 2020. Watu wa mpira duniani kote waliungana kutoa salamu za mwisho kwa kipenzi chao huyo, ambaye aliandika historia kubwa kwenye mchezo huo wa mpira wa miguu. Pele, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo walikuwa miongoni mwa mastaa walioguswa na kifo cha shujaa huyo wa Argentina, aliyeipa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 1986.

Maradona alikuwa na makosa yake kama mwanadamu, lakini hakuna ubishi alipendwa na kundi kubwa sana la watu – hasa huko kwao Argentina na wale waliobahatika kucheza naye.

Lakini, hata Wabrazili, wenye upinzani na Waargentina, walimpenda Maradona, akiwamo supasaa Ronaldo de Lima, ambaye pia ni mshindani mwingine kwenye hadhi ya kutambuliwa kama mchezaji bora wa soka wa nyakati zote.

Ronaldo, mshindi mara mbili wa Kombe la Dunia, alifuchua urafiki wake na Maradona baada ya Muargentina huyo kufariki.

Kama ilivyokuwa kwa wapenda soka wengine, straika huyo wa zamani wa Real Madrid, Barcelona, PSV, Inter Milan na AC Milan, alikuwa mwenye huzuni kubwa baada ya kupata taarifa za kifo cha Maradona.

“Diego ameacha heshima kubwa kwenye soka. Kifo chake ni kigumu kwangu kukubaliana nacho,” alisema Ronaldo.

“Taarifa zile zilinishtua sana na kuniacha mwenye huzuni. Maradona amebadili maisha ya watu wengi sana, mimi ni mmoja wa watu waliopata hamasa kupitia yeye.”

Maradona kuvaa saa mbili

Ronaldo alifichua nyuma ya pazia ya Maradona kuvaa saa mbili. Iliwahi kuripotiwa huko nyuma kwamba Maradona alikuwa akivaa saa mbili kila alipokuwa safarini: saa moja ilikuwa inasema muda wa jiji alilikuwapo na nyingine ilikuwa inasema muda wa Argentina.

Lakini, Ronaldo anafichua ukweli wa jambo hilo. Haikuwa kama watu walivyokuwa wakidhani, akisema: “Kuna kipindi Maradona alikuja kunitembelea Madrid na tulikwenda kupata mlo wa jioni pamoja.

“Diego alikuja na saa zake mbili na kusema hakuwa akienda kokote bila ya kuwa na saa hizo mbili.

“Nilimuuliza kwanini anavaa saa mbili na alinijibu, binti yake alimnunulia saa hizo kama zawadi, hivyo hajawahi kuzivua tangu alipozivaa. Tulipomaliza kula, alivua saa moja na kunipa zawadi. Nilikataa, lakini alisisitiza na kuonyesha kukasirika, hivyo sikuwa na namna. Nitaitunza ile saa kwa siku zote za uhai wangu kama kumbukumbu ya urafiki wangu na yeye.”

Hakika saa hiyo ni zawadi yenye thamani kubwa kwa Ronaldo, ambaye kwa sasa ni rais wa klabu ya Real Valladolid.

Chanzo: Mwanaspoti