Kumekuwa na mijadala mingi sana mitandaoni kuhusu nafasi ya Clatous Chama kwenye timu ya taifa ya Zambia, kwa sasa akiwa Yanga na wakati akiwa Simba.
Wanatakwimu wa mitandaoni wanasema tangu ahamie Yanga kwenye dirisha kubwa la usajili lililopita, Chama amekuwa akipata sana nafasi zaidi kwenye kikosi cha Chipolopolo, kuliko wakati ule akiwa Simba SC.
Ukurasa huu umejaribu kufanya utafiti wa mchezaji huyo kwenye timu ya taifa, katika kipindi hiki yuko Yanga kwa kulinganisha na kipindi kile akiwa Simba.
Utafiti huu umeangalia mechi zote za timu ya taifa ya Zambia za mwaka 2024, ambao umemgawa Chama mara mbili, akiwa Simba na akiwa Yanga.
1. Akiwa Simba
Wakati mwaka 2024 unaanza, Chama alikuwa mchezaji wa Simba, na aliendelea kuwa mchezaji wa Simba hadi Juni 30 mwaka huu mkataba wake ulipoisha.
Katika kipindi hicho, Zambia ilicheza mechi 10, za mashindano rasmi na za kirafiki.
MECHI
MASHINDANO
TAREHE
KUCHEZA
MCHANGO
Zambia 1-1 Cameroon
Kirafiki
09/01/2024
Alikuwa benchi
DR Congo 1-1 Zambia
AFCON
17/01/2024
Alikuwa benchi
Zambia 1-1 Tanzania
AFCON
21/01/2024
Aliingia dk 76
Asisti
Zambia 0-1 Morocco
AFCON
24/01/2024
Aliingia dk 83
Zambia 2-2 Zimbabwe
Kirafiki
23/03/2024
Alicheza dk 90
-Bao 1
Zambia 2-1 Malawi
Kirafiki
26/03/2024
Aliingia dk 64
-Bao 1 na asisti
Morocco 2-1 Zambia
Kufuzu WC
07/06/2024
Hakuitwa
-
Zambia 0-1 Tanzania
Kufuzu WC
11/06/2024
Hakuitwa
-
Zambia 0-2 Kenya
COSAFA
27/06/2024
Hakuitwa
Zambia 0-2 Zimbabwe
COSAFA
30/06/2024
Hakuitwa
NB: Timu alicheza mechi nne na kutumia jumla ya dakika 313 katika sita alizoitwa kati ya 10 ambazo Zambia ilicheza. Katika sita alizoitwa, alifanikiwa kucheza katika mechi nne.
2. Akiwa Yanga
Alfajiri ya Julai mosi, 2024 Yanga waliposti picha ya Clatous Chama akisaini kuitumikia klabu hiyo na kuthibitisha tetesi za muda mrefu.
Mkataba wake ukaanza kuwa rasmi tangu siku hiyo.
Katika kipindi hicho, Zambia imecheza mechi tatu tu, kama ifuatavyo.
MECHI
MASHINDANO
TAREHE
KUCHEZA
MCHANGO
Comoro 1-0 Zambia
COSAFA
02/07/2024
-Hakuitwa
-
Ivory Coast 2-0 Zambia
Kufuzu AFCON
06/09/2024
-Alicheza dk 64
-
Zambia 3-2 Sierra Leone
Kufuzu AFCON
10/09/2024
-Alicheza dk 89
-
NB: Katika kipindi akiwa Yanga, Zambia imecheza mechi tatu tu huku yeye akiitwa katika mechi mbili katika hizo na akicheza jumla ya dakika 153.
Japo dakika zinaweza kuonekana chache akiwa Yanga kuliko alipokuwa Simba, lakini kiuhalisia huku ndiyo amefaidi zaidi kuwepo timu ya taifa kuliko wakati ule.
CH4 CH4
Hii ni kwa sababu wastani wa mechi na dakika ni mzuri zaidi kuliko kule. Hapa ndipo wachambuzi wa Tanzania wanaposhadadia wakisema anapata zaidi muda wakati huu kwa sababu yuko Yanga.
Lakini hiyo siyo kweli, ni mambo tu ya kishabiki, ukweli ni kwamba Chama anapata zaidi muda wakati huu kutokana na kushuka kwa viwango vya watu waliokuwa wakimuweka benchi wakati ule.
Wale wachezaji waliokuwa wanaanza mbele ya Chama wakati ule, sasa hivi hawana kitu kabisa. Wakati ule nafasi ya Chama kwenye kikosi cha Zambia ilikuwa ngumu sana kutokana na watu aliokuwa anashindana nao katika nafasi ambazo yeye anaweza kucheza.
Nafasi zote ambazo Chama anaweza kucheza zilikuwa na wachezaji waliomzidi uwezo. Nitakuchambulia nafasi moja moja.
CH5 CH5
Namba 10
Hii ndiyo nafasi ambayo Chama huwa anaimudu vizuri kuliko zote, na anaifurahia sana kucheza.
Lakini wakati ule kwenye timu ya taifa ya Zambia nafasi hii ilikuwa ikimilikiwa na Fashion Sakala, nyota wa klabu ya Rangers ya Scotland.
Msimu uliopita wakati akimsugulisha benchi Chama kwenye timu ya taifa, Sakala alimaliza akiwa amefunga mabao 10+ na kutoa asisti 10+ za mabao kwenye ligi yao.
Hakuna kocha anayetaka ushindi atamuacha mtu kama huyu nje ilhali ni mzima wa afya, halafu akamuanzisha Chama. Labda kama kuna matatizo ya kiufundi au kinidhamu.
Lakini sasa Sakala siyo yule tena na mara kadhaa nafasi hii imekuwa ikitawaliwa na Edward Chilufya wa klabu ya Midtjylland ya Denmark.
Kwenye mchezo wa kipigo cha 2-0 kutoka Ivory Coast, Chama aliingia dakika ya 26 kuchukua nafasi ya huyu.
Namba 8
Nafasi nyingine ambayo Chama anaweza kucheza, angalau kwa kulazimisha, ni namba nane. Lakini kwa bahati mbaya kwenye kikosi cha Zambia wakati ule nafasi hii ilikuwa mali ya Kings Kangwa anachezea Belgrade Red Star ya Serbia.
Kwenye ligi yao jamaa alifunga mabao 10+ msimu uliopita, wakati akimsugulisha Chama.
Mwezi Machi mwaka jana, Kangwa alimpisha Chama katika dakika ya 81 kwenye mchezo wa kiraki dhidi ya Malawi.
Jamaa bado kaishikilia nafasi hii na Chama hajathubutu kabisa kuchukua nafasi yake hata kwa sekunde.
Winga namba 7
Labda tuseme kocha ajilipue na kumpanga Chama kama winga wa kulia. Lakini hata hivyo, kwa Zambia hilo haliwezekani kwa sasa kama ambavyo lilikuwa haliwezekani wakati ule kwa sababu nafasi hii ni mali ya Emmanuel Banda kutoka Rijeka ya Croatia.
Jamaa ana kasi, nguvu na maarifa yanayoweza kumshawishi kocha yoyote kumpa nafasi.
Winga namba 11
Mara kadhaa klabuni Simba wakati ule Chama alikuwa akicheza kama winga wa kushoto ili kutoa nafasi kwa timu kuanza na washambuliaji pacha (wakati wa Bocco na Kagere) au hata baadaye kuruhusu yeye na Saido Ntibazonkiza kuanza pamoja.
Lakini hilo halikuwezekana wakati ule akiwa Simba hata sasa akiwa Yanga kwa timu ya taifa ya Zambia kwa sababu nafasi hii ni mali ya Lameck Banda wa Lecce ya Italia.
Kwa hiyo licha ya umaarufu wake hapa nyumbani na hata kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, bado Chama aliendelea kuchoma mahindi kwenye timu ya taifa.
Lakini sasa, kuyumba kidogo kwa Fashion Sakala kunaweza kumrahishia kazi Chama na kuendelea kutamba zaidi na timu ya taifa.
Lakini sababu siyo kwamba yuko Yanga, hapana, ni kiushuka kwa viwango kwa wale waliokuwa wakimchomesha mahindi wakati ule pale Chipolopolo.