Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri ya Aziz Ki yafichuka, Fei Toto atajwa

Aziz Ki Pic Siri ya Aziz Ki yafichuka, Fei Toto atajwa

Tue, 3 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa Yanga wameanza kumuelewa sana, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Stephane Aziz KI hasa katika kufunga mabao yatokanayo na mashuti au friikikii, lakini kocha msaidizi wa timu hiyo, Cedric Kaze amefichua siri za mabao ya nyota huyo kutoka Burkina Faso.

Aziz KI katika mechi mbili mfululizo zilizopita amefunga mabao ya kutokea mbali likiwamo shuti dhidi ya Azam na lile la juzi dhidi ya Mtibwa Sugar akipiga friikikii iliyomshinda kipa Razack Shekimweri na kutinga wavuni na kuendeleza rekodi ya kuitungua Mtibwa kwani alifunga pia Dar.

Bao la juzi Aziz KI alipiga friikikii ambayo ilimshinda kudaka kipa Shekimweri na kumgonga gotini na kuingia wavuni, likiwa bao la nne msimu huu, ila alifunga pia bao la friikikii dhidi ya Simba akimtungia kipa Aishi Manula na katika mechi ya Azam alisababisha bao la tatu kwa kupiga mkwaju kama huo ukamshinda kipa Ali Ahamada na kumfanya Farid Mussa kukwamisha bao la ushindi.

Juzi kwenye Uwanja wa Manungu, alipiga friikikii nyingine kali katika kipindi cha pili, lakini safari hii Shekimweri aliiokoa na kufanya hadi mwisho wa mchezo matokeo kuwa bao 1-0 na Yanga kuendeleza rekodi ya kushinda mechi ya sita mfululizi dhidi ya Mtibwa katika ligi.

Hata hivyo, Kocha Kaze amefichua kuwa, mishuti anayoipiga Aziz Ki sambamba na zile friikikii sio kama anabahatisha.

Akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya mechi ya Manungu, Kaze alisema ni mchezaji ambaye hupenda kujiongeza baada ya mazoezi akitumia kati ya dakika 15 hadi 20 kufanya mazoezi binafsi ya kupiga mipira ya aina hiyo.

"Sio jambo geni kwake, kwani huwa analifanya mazoezi kila siku tukimaliza mazoezi ya pamoja, tunachomsaidia ni kumpa muda na maelekezo tu ambayo huyafanyia kazi," alifichua Kaze na kuongeza;

"Unapocheza na Mtibwa kwao unatakiwa kuwa na njia mbadala ya kupata ushindi, ni timu ambayo haifungiki kirahisi hapa kwao ndio maana tuliwaelekeza wachezaji wetu wacheze kwa kutulia ili kupata njia ya kuwafunga," alisema Kaze.

Kaze alisema kwa aina ya mipira ambayo nyota huyo amekuwa akiipiga huenda akaendelea kuwatesa sana makipa, kwani wakati mwingine huonekana kama haina madhara kwani anaipiga kiwepesi lakini huwa na kasi inayowachanganya makipa wengi.

"Ufundi huu wa kupiga mipira hiyo na mashuti mengine akiwa mbali hajaanza hata, amekuwa akifanya tangu akiwa Asec Mimosas, ila kwa hapa amekuwa akijitengenea muda na kuzidi kuimarika na kama ataendelea hivi atatisha zaidi," alisema Kaze aliyewahi kuwa kocha mkuu wa Yanga kabla ya kufurushwa mwaka 2021 na kurudishwa mwaka jana kumsaidia Nasreddine Nabi.

Kuhusu michuano ya Kombe la Mapinduzi, Kaze alisema; "Hakuna michuano tunayodharau, tunaenda kushindana ingawa baadhi ya wachezaji wetu tutawapumzisha hawataenda kabisa. Ni wale ambao wametumika sana katika mechi za ligi na michuano ya kimataifa, wanapaswa kupumzika maana tuna jukumu zito siku zijazo."

Alisema wanaenda Zanzibar kwa malengo yaleyale ya kushinda na kutwaa ubingwa huo baada ya msimu uliopita kuteleza na kuliteja taji ililokuwa ikilishikilia kwa kulitwaa mwaka 2021.

Baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo kupitia mitandao ya kijamii na wale waliokuwa uwanjani juzi, walikaririwa wakitamba kwamba wataanza kumsahau Feisal Salum 'Fei Toto' aliyevunja mkataba na kuondoka klabuni kwao na sasa akila bata Dubai.

"Kwa migoli kama hii, tutamsahau tu Fei, ni kweli alikuwa kipenzi chetu, lakini Aziz KI anatupa raha...mwamba anajua sana, halafu hana makeke mengi," alikaririwa shabiki aliyekuwa Uwanja wa Manungu wakati akishangilia ushindi wa timu hiyo dhidi ya Mtibwa.

Yanga inaenda Zanzibar ikiwa inaongoza ligi kwa pointi 50, huku watani zao Simba wakishika nafasi ya pili na pointi 44, nne zaidi na ilizonazo Azam iliyopo ya tatu na pointi 40.

Chanzo: Mwanaspoti