Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri ya Azam FC na Wacolombia hii hapa

Azam Wacolombiaz Siri ya Azam FC na Wacolombia hii hapa

Thu, 6 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Azam imefikisha wachezaji wanne raia wa Colombia hadi sasa ila moja ya jambo usilolijua ni kwamba, mshambuliaji wa timu hiyo, Franklin Navarro aliyesajiliwa Januari mwaka huu ndiye aliyechora ramani ya nyota wengine kusajiliwa.

Iko hivi. Baada ya mabosi wa Azam kukamilisha usajili wa Navarro kutokea Cortulua FC ya kwao Colombia, walimtumia nyota huyo kama skauti ya wachezaji wengine na ndipo wakaanza kuwafuatilia mmoja baada ya mwingine na kukamilisa sajili zao.

Mmoja wa viongozi wa Azam, aliliambia Mwanaspoti, awali hawakuwa na mpango wa kusajili kutoa Amerika ya Kusini ila ujio wa Navarro ulitoa mwanga huo kwani ndipo walipata nafasi ya kuskauti nyota wengine ambao wamekuwa na tija kikosini.

"Kulikuwa na meneja mmoja ambaye alipendekeza jina la Navarro tumsajili na tulikuwa na mashaka naye mwanzoni ila baada ya kumwangalia tukagundua ni mchezaji mzuri, tulipomsajili tukaamua kumtumia kupata wengine," alisema kiongozi mmoja.

Kwa upande wa Kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo alisema, usajili uliofanyika hadi sasa unaonyesha ni kwa jinsi gani timu hiyo inataka kufanya vizuri zaidi msimu ujao hususani ikichagizwa na ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Moja ya sajili ambazo mshambuliaji huyo alipendekeza ni za beki wa kati, Yeison Fuentes aliyetokea Leones FC ikiwa ni moja ya usajili bora kufanyika kwani tangu nyota huyo ametua nchini amekuwa ni panga pangua katika kikosi cha kwanza.

Wengine ni kiungo, Ever Meza aliyetokea klabu ya Leonnes na mshambuliaji, Jhonier Blanco kutoka klabu ya Aguilas Doradas ambaye msimu uliopita alikuwa mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza (Categoria Primera B) akifunga mabao 13 na timu ya Fortaleza CEIF.

Pia, Jhonier aliisaidia Fortaleza kupanda daraja na kuchukua ubingwa, huku akifunga jumla ya mabao 18 katika mechi 26 za mashindano yote.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live