Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri ushindi wa Yanga hii hapa

31104 Pic+yanga TanzaniaWeb

Wed, 12 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kocha Mwinyi Zahera anabaki kuwa nguzo kuu ya mafanikio ya Yanga katika mashindamo ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Uwezo wa kuwajenga kisaikolojia wachezaji, msingi wa nidhamu aliotengeneza kikosini, ujanja wa kung’amua kwa haraka ubora na udhaifu wa kikosi chake na wapinzani kisha kufanyia kazi ndani ya muda mfupi na mbinu za kiufundi vimeifanya Yanga kuwa tishio.

Kabla ya msimu kuanza, Yanga haikuwa miongoni mwa timu bora zilizokuwa zikipewa nafasi ya kutwaa ubingwa kutokana na aina ya usajili iliyofanya, hali ngumu ya kiuchumi inayopitia na kutopata muda wa kutosha wa maandalizi.

Timu zilizokuwa zinapewa nafasi kubwa ni mabingwa watetezi Simba na matajiri wa Azam FC ambazo zilionekana zina vikosi bora na nguvu ya kiuchumi kuzidi Yanga.

Hata hivyo, mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa wametwaa mara 26, wamebadili upepo kwa kupata matokeo mazuri hasa ya ushindi ambayo yamewafanya wakae kileleni mwa msimamo wa ligi na sasa wanapewa nafasi ya kutwaa ubingwa.

Tofauti na matarajio ya wengi, Yanga iliyocheza michezo 15 hadi sasa, haijaonja ladha ya kupoteza mechi kwenye ligi, ikishinda michezo 13 na kutoka sare mara mbili.

Wakati Yanga ikionekana kuwa na kundi kubwa la wachezaji wa kawaida, Zahera amefanikiwa kucheza na saikolojia yao, kuwajengea morali na hamasa ya kuipigania timu jambo ambalo limewasaidia.

Moja ya mbinu ambazo Zahera amekuwa akizitumia ni kuwataja na kuwakosoa bila kificho nyota wake ambao wamekuwa wakicheza chini ya kiwango au wale wasiokuwa na ufanisi wa kutosha mazoezini.

Mbinu hiyo imesaidia kuwafanya wachezaji kujituma uwanjani licha ya changamoto za kiuchumi wanazopitia ili waepuke kuanikwa na Zahera.

Lakini kama hiyo haitoshi kocha huyo mara kadhaa amekuwa akitoa fedha zake za mfukoni kuwapa wachezaji wagawane ili kupoza machungu ya ukata unaowakabili hasa mishahara na posho inapochelewa.

Kocha huyo pia amefanikiwa kuwajenga kinidhamu wachezaji wa Yanga ambao licha ya madai yao ya fedha yanayoibuka kila wakati, wengi wao wamekuwa wakihudhuria na kufanya mazoezi kwa bidii jambo linalowafanya kuwa fiti.

Pia Zahera anasifika kwa uwezo mkubwa wa kubadilika kwa haraka kimbinu pindi Yanga inapofanya maandalizi ya mchezo au inapokuwa uwanjani inacheza kulingana na ubora na udhaifu wa timu yake na upinzani.

Yanga imekuwa ikibadilika kila wakati na imekuwa ikilazimika kucheza soka la kuvutia ikijilinda na kushambulia kwa kushtukiza, pasi fupifupi au ndefu kulingana na jinsi wapinzani wao walivyo.

Hilo limechangia Yanga kuwa na uwezo wa kudhibiti timu pinzani hata pale inapoanza kuzidiwa kwani amekuwa akifanya mabadiliko ya haraka ambayo husaidia timu kurudi mchezoni na kupata matokeo mazuri.

Mbali na Zahera kingine ambacho kinaonekana kuwabeba ni udhaifu wa timu pinzani kutoipa heshima pindi wanapokutana nayo wakihisi sio tishio ndani ya uwanja jambo linalowapa faida Yanga kutokamiwa na kupata matokeo ya ushindi tofauti na Simba na Azam ambazo zinafanya timu pinzani kujipanga vilivyo pindi wanapokabiliana nazo.

Mchambuzi wa soka nchini Ally Mayay alisema Zahera ana mchango mkubwa katika mafanikio ya timu hiyo kuvuna pointi 41 katika mechi 15 walizocheza bila kupoteza mchezo katika mashindano hayo msimu huu.

“Kile wanachokifanya wachezaji wa Yanga uwanjani kinaonyesha namna kocha Zahera alivyokuwa mzuri wa saikolojia, siyo kazi rahisi kumuelekeza mchezaji ajitume angali hajapokea mshahara, kwa maoni yangu amefanya kitu kikubwa sana kwa Yanga,”alisema nahodha huyo wa zamani wa timu hiyo.

Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua, alisema kuwa Zahera ana mchango mkubwa na maendeleo ya klabu hiyo kwa kuwa ndiye mtu wa mwisho wa benchi la ufundi na wachezaji wanatekeleza wanachoambiwa.

Wakati huo huo, Azam jana ilishindwa kuing’oa Yanga kileleni baada ya kutoka sare mabao 2-2 na KMC. Lipuli iliicharaza mabao 2-1 timu ya Ruvu Shooting.



Chanzo: mwananchi.co.tz