Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri imefichuka! Aliyekwamisha mchakato wa mabadiliko Simba Sc atajwa

Mo Dewji: Tunahitaji Golikipa Mwingine Simba Mo Dewji.

Sat, 2 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Huko Simba mambo bado, juu ya ile ishu ya mabadiliko ya klabu hiyo ili iendeshwe kwa mfumo wa hisa ambao mchakato wake ulianza tangu mwaka 2017 umekwama ikielezwa tatizo likiwa ni katiba ya klabu hiyo, kiasi cha Ofisi ya Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kurudisha mpira Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Simba inapambana kutaka klabu hiyo iendeshwe kisasa kwa hisa na tayari imekuwa ikimtangaza Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohammed ‘Mo’ Dewji kuwa ni mwekezaji wake akidaiwa kumiliki asilimia 49 ya hisa, huku 51 zilizobakia zikiwa ni za klabu.

Mchakato unaelezwa ulishapata ruksa kwa Tume ya Ushindani nchini (FCC) kisha Ofisi ya Wakala na Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na sasa ilitua RITA ambako maofisa wake walijifungia kufanya uchambuzi wa kina na kubaini kuna tatizo katika katiba ya klabu hiyo.

Rita wala hawakutaka mambo mengi inaelezwa baada ya kuangalia katiba ikionyesha mwekezaji mwenye asilimia 49 ana mamlaka makubwa kuliko wenye asilimia 51 ikashtuka na kuamua kurudisha jambo hilo ofisi za BMT wakitoa maelekezo kwa Simba ifanye kitu mambo yawe sawa.

Karibu mwaka wa tano tangu mchakato huo uanze, lakini ukiwa umeshindwa kukamilika baada ya kupita sehemu mbalimbali, hali iliyoibua sintofahamu huku mwekezaji huyo mara kadhaa akilalamika katika mitandao ya kijamii akidai kuonewa kutokana na jambo hilo kutofikia tamati.

Hata hivyo, juzi mmoja wa vigogo wa Simba aliliambia Mwanaspoti mchakato huo umekwama RITA ambao ndio wenye mamlaka ya kupitisha Bodi ya Wadhamini ya klabu hiyo kwa mujibu wa katiba ya Simba.

Alisema RITA imebaini kuwepo na upungufu kwenye katiba hiyo baada ya kupitia suala hilo na kulazimika kuirejesha katiba hiyo BMT ambao ndio waliwasilisha RITA jambo hilo.

“Tumetakiwa kumaliza sintofahamu iliyopo kwenye katiba yetu, hivyo RITA imeirudisha BMT na tayari baraza nalo limeirudisha Simba,” alisema kigogo huyo aliyeomba hifadhi ya jina.

Japo mabosi wa RITA walikataa kuzungumzia suala hilo walipoulizwa, lakini Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha alikiri kuipokea katiba hiyo kutoka RITA.

“Ni kweli imerudishwa kwetu, na kilichobaki ni sisi kuwasiliana na Simba kuwajulisha hilo, sikuwepo ofisini, kwa ajili kujadili hilo ndio nimerudi, lakini suala lao limerudishwa kwetu, nilipokuwa nje ya ofisi nililiacha kwa msajili (Evodius Kyando),” alisema Neema na kuongeza;

“Kuna some issue (baadhi ya mambo) katika katiba yao ndio inapaswa kurekebishwa, hivyo wasiliana na msajili atakuwa na majibu mazuri kuhusu jambo hilo.”

Kwa upande wa msajili huyo alipoulizwa  alisema; “Kimsingi kuna mambo mengi pale Simba, hili suala lilifika kwetu na tukawarudia kuwaelekeza wanachotakiwa kuboresha. Mwanasheria wa Simba, ndiye anayepaswa kulizungumzia zaidi hilo, kwa vile maelekezo yote tumeshapeana na tunasubiri feedback (mrejesho) kama tulivyokubaliana.”

Mwanasheria wa klabu, Hosea Chamba alipotafutwa alisema jambo hilo ni pana na hakuwa kwenye mazingira ya mazuri ya kulizungumzia.

“Niko bize kidogo na suala hili ni pana, nipe muda wa saa mbili (kuanzia saa 4:13 asubuhi juzi) kisha nipigie,” alisema Hosea na kukata simu.

Hata hivyo, baada ya muda huo alipigiwa simu hakupokea, hata jana asubuhi alitafutwa tena, simu yake iliita bila kupokelewa, ila kiongozi wa Simba aliyeomba hifadhi ya jina alisema kinachotakiwa kwa sasa kuboreshwa kwa baadhi ya vipengele vingi ndani ya katiba ya klabu hiyo ambavyo haviko sawa.

“Wanadai kuna vitu vingi havipo sawa, mfano mwekezaji ana hisa 49 halafu ndiye mwenye mamlaka makubwa kuliko mwenye hisa 51, wanasema sio sawa, lazima klabu itendewe haki na kulindwa,” alisema.

Awali Simba ilitaka kumpa mwekezaji asilimia 51 na klabu kubaki na 49, kabla ya serikali iliingilia kati  na Mo inadaiwa alishatoa Sh20 bilioni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live