Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri iliyojificha Aziz Ki wa Gamondi vs Aziz Ki wa Nabi

Aziz Ki0012 Aziz Ki.

Sat, 26 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiwango anachokionyesha kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki kinatajwa kusababishwa na aina ya uchezaji wa sasa wa timu pamoja na uhuru anaopewa uwanjani na kocha Angel Miguel Gamondi.

Msimu huu umeanza vizuri kwa Aziz Ki, ambaye licha ya msimu uliopita kufunga mabao 10 ya Ligi Kuu, lakini hakuonekana kama mchezaji mwenye ubora katika mechi mfululizo za mashindano yote.

Lakini msimu huu umekuwa na mabadiliko makubwa kwa nyota huyo wa kimataifa wa Burkina Faso, ambaye ameshafunga katika mashindano ya aina tatu tofauti ndani ya mechi tano.

Yanga imecheza Ngao ya Jamii mechi mbili dhidi ya Azam FC na Simba, huku Aziz Ki akifunga dhidi ya matajiri wa Chamazi kwenye ushindi wa 2-0, mechi na Simba ikimalizika kwa suluhu na kuamuliwa kwa penalti.

Katika mechi hizo, Aziz Ki alikuwa anaingia akitokea benchi, lakini kwenye mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ASAS, Kocha wa Yanga, Gamondi aliamua kumwanzisha na kufunga bao la kuongoza katika ushindi wa 2-0. Lingine lilifungwa na Kennedy Musonda.

Kocha huyo aliendelea kumwamini hata kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC, juzi, kwenye Uwanja wa Azam Complex na nyota huyo wa zamani wa ASEC Mimosas aliendeleza ubora kwa kufunga bao moja katika ushindi wa 5-0.

Hofu ya wengi msimu huu juu ya Aziz Ki ilikuwa baada ya kusajiliwa kwa Pacome Zouzoua, ambaye naye kwa asili anacheza nyuma ya mshambuliaji wa kati (namba 10), lakini kwa mshangao zaidi, Gamondi aliwaanzisha wote wawili juzi.

Akionekana kucheza kama winga wa kushoto, Aziz Ki alikuwa akiwazunguka Zouzoua na winga mwenzake, Jesus Moloko, akionyesha jinsi gani ubora wake umeimarika katika kuichezesha Yanga.

Tofauti na msimu uliopita, mchezaji huyo anayetumia mguu wa kushoto anaonekana kuanza kukabia juu, huku pia akichangia kwa kiasi kikubwa kusaka mabao katika kila shambulizi la Yanga msimu huu.

Ubora wa kipa wa KMC, Wilbol Maseke ulipunguza idadi ya mabao ya Aziz Ki kwenye mchezo wa juzi, kwani shuti lake la dakika ya 11 na lile la adhabu ndogo kipindi cha pili ni miongoni mwa kazi nzuri za nyota huyo uwanjani.

Akimzungumzia mchezaji huyo na maendeleo yake, Gamondi alisema anapenda kutoa nafasi kwa kila mchezaji kumwonyesha alichonacho kabla hajaamua vinginevyo.

"Wakati tunaanza kambi, Aziz Ki alikuwa miongoni mwa wachezaji waliochelewa kurudi, nikapata nafasi ya kuwaona wote kabla ya mechi dhidi ya Kaizer Chiefs, nikawaona tena kwenye Ngao ya Jamii.

"Hivyo nikipanga mchezaji kwa sasa inatokana na kile ambacho tunafanya mazoezini, nafurahi kuona kila mchezaji ananipa ambacho nakitarajia, ukiachana na makosa machache," alisema kocha huyo raia wa Argentina.

Mshambuliaji wa zamani Tanzania Prisons na Yanga, Hery Morris alisema anamuona Aziz Ki akizidi kuwa bora msimu huu kwa sababu ameachwa acheze akiwa huru.

Morris alisema nyota huyo anavyocheza ni tofauti na msimu uliopita, kwani alikuwa anatakiwa achezeshe timu wakati huo huo akabe, hivyo kuna uwezekano mkubwa chini ya Gamondi nyota yake ikang'aa zaidi.

"Hata kule ASEC Mimosas alionekana bora kwa sababu alikuwa huru hasa kwenye kutembea na mpira, nadhani kocha ameona kitu kwa Aziz Ki, ndiyo maana amemuachia awe huru," alisema Morris.

Mshambuliaji wa zamani Moro United na Ashanti, Benedict Ngassa alisema msimu huu Aziz Ki anaweza kuwa tegemeo kwa sababu Gamondi amempa uhuru wa kufanya chochote.

Ngassa alisema katika timu yoyote haiwezekani wachezaji wote wakabe, lazima kuwe na mmoja ambaye atakuwa huru kuangalia wapi mpira unatakiwa kwenda na kwa wakati gani.

Aziz Ki alisajiliwa akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwa mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: