Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sioni shida ya kanuni ya bao la ugenini Afrika

Simba Vs Ahly Cairo Misri.jpeg Sioni shida ya kanuni ya bao la ugenini Afrika

Mon, 30 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kumekuwa na mijadala na mitazamo tofauti juu ya kuendelea kutumika kwa kanuni ya bao au mabao ya ugenini katika kuamua mshindi kwenye mashindano mbalimbali yanayochezwa kwa mtindo wa mtoano hapa Afrika.

Kwa hapa nchini, jambo hilo lilionekana kuibuka na kuteka hisia msimu uliopita baada ya Yanga kukosa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika mbele ya USM Alger ya Algeria katika fainali baada ya mechi mbili kumalizika kwa sare ya mabao 2-2. Mchezo wa kwanza ambao ulichezwa hapa Dar es Salaam, Yanga ikiwa mwenyeji ilipoteza kwa mabao 2-1 lakini katika mechi ya ugenini huko Algeria ikaibuka na ushindi wa bao 1-0.

Hata hivyo ushindi huo haukutosha kuipa Yanga taji kwani wapinzani wao walinufaika kwa kufunga idadi kubwa ya mabao ugenini kulinganisha na wao.

Kabla hata nusu mwaka haujatimia baada ya Yanga kukosa taji, Simba wamejikuta wakiumizwa na kanuni ya bao la ugenini katika mashindano mapya yaliyozinduliwa nchini Oktoba 20 ya African Football League (AFL). Katika mashindano hayo ambayo yalianzia robo fainali, Simba ilikwama mbele ya miamba ya Afrika Al Ahly licha ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Sare ya mabao 2-2 katika mechi ya kwanza iliyozikutanisha timu hizo Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam iliwavusha Al Ahly kwenda nusu fainali wakinufaika kwa kufunga idadi kubwa ya mabao ugenini tofauti na Simba iliyolazimisha sare ya bao 1-1 huko Misri.

Wengi ambao wanalia na kanuni hiyo wanaona na kuamini kwamba Simba na Yanga zilikuwa na fursa ya kutamba dhidi ya timu hizo kutoka Kaskazini mwa Afrika ikiwa isingekuwepo na badala yake mechi hizo zingeamriwa kwa mikwaju ya penalti ili kusaka mshindi.

Hata hivyo kwa mtazamo wangu, sioni tatizo wala shida yoyote ya uwepo wa kanuni ya bao la ugenini katika kuamua mshindi hapa Afrika kwenye mashindano ya mtoano ikiwa mechi mbili za timu zinazoshindana zimehitimishwa kwa matokeo ya sare ya mabao.

Uwepo wa kanuni hii naamini unaongeza umakini na tahadhari zaidi kwa timu lakini ushindani mkubwa kwenye mechi pindi inapokuwa nyumbani au ugenini, ili iweze kupata matokeo mazuri ambayo yatakuwa chachu ya kuiwezesha kusonga mbele katika mashindano husika.

Timu inapokuwa katika uwanja wa nyumbani, hapana shaka italazimika kucheza kwa nidhamu kubwa ya kujilinda ili isifungwe mabao ambayo yanaweza kumnufaisha mpinzani lakini itajitahidi kuhakikisha inapata ushindi mnono wa mabao ili ijiweke katika mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mechi ya marudiano.

Kwa ile ambayo itakuwa ugenini ni wazi kwamba itahakikisha ina sanaa nzuri ya kujilinda na kushambulia iweze kupata mabao ya ugenini ambayo yatapunguza kazi katika mechi ya marudiano pale itakapokuwa nyumbani.

Lakini pia badala ya kupaza sauti kanuni hiyo isiwepo, pengine ingekuwa vyema nguvu inayotumika kupigania hilo lifanyiwe kazi, ingetumika katika kuzishawishi na kuzisaidia timu zetu zifanye usajili wa wachezaji bora na ziandaliwe vizuri ili ziweze kuwa na uimara na kiwango cha juu cha kupambana na timu ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika mashindano ya klabu Afrika na hata timu za taifa.

Ubora wa timu na maandalizi utaziwezesha timu zetu kupata ushindi popote pale pasipo kuangalia zimecheza na nani na hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kufanya vizuri bila hofu ya kucheza ugenini au nyumbani.

Ukiwa na timu bora na imara, unaweza kufunga idadi kubwa ya mabao ugenini na ukayalinda yakakubeba kama unavyoweza kufanya katika mechi za nyumbani. Mfano mzuri ni msimu uliopita ambapo Yanga ilipata ushindi katika mechi nne tofauti za kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ugenini na timu hizo ambazo ilizifunga hazikuweza kufua dafu mbele yake pindi zilipokuja hapa Dar es Salaam.

Kama timu zetu hazitokuwa bora na imara, hazitoweza kufanikiwa hata kama ikitokea kanuni hiyo ya bao la ugenini itaondolewa kama ambavyo mara kadhaa imewahi kuzikumba pindi zilipokuwa zikishiriki mashindano tofauti Afrika.

Mbali na hayo, tunapaswa kukumbuka kwamba zipo nyakati ambazo timu zetu zimewahi kunufaika na kanuni hiyo ya bao la ugenini leo hakuna haja ya kuona ubaya wake kisa tu imetuumiza.

Mfano mzuri tu ni katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambapo Simba licha ya kutokuwa na kiwango bora katika mechi mbili dhidi ya Power Dynamos ya Zambia, ilisonga mbele ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka sare ya mabao 3-3 katika mechi mbili baina yao, ikilazimisha sare ya mabao 2-2 ugenini na nyumbani ikitoka sare ya bao 1-1.

Chanzo: Mwanaspoti