Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sio sifa kuingia uwanjani saa 4 asubuhi, tumepitwa na wakati

Mashabiki Wa Simba V Yanga Sio sifa kuingia uwanjani saa 4 asubuhi, tumepitwa na wakati

Sun, 30 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Zamani, zaidi ya miaka 30 iliyopita ungeweza kumsikia Charles Hillary au Ahmed Jongo kama sio Sekioni Kitojo au Salim Mbonde au Aboubakari Liongo, akitangaza mechi kupitia Redio Tanzania. Pambano ni Simba na Yanga na kitu cha kwanza ambacho angesifia kabla ya kutaja vikosi ni namna uwanja ulivyofurika.

Baada ya hapo angeelezea uwanja umefurikaje. Angekwambia mashabiki walianza kuingia uwanjani tangu saa nne asubuhi. Kuzungumza mashabiki walikuwa wameingia uwanjani tangu saa nne asubuhi lilikuwa jambo la sifa.

Zaidi ya miaka mingi baadaye, Baraka Mpenja wa Azam TV naye anatuambia jambo hili hili. Kwamba mashabiki walianza kuingia uwanjani tangu saa nne asubuhi. Wakati mwingine inanikera kwa sababu linazungumzwa kama sifa hivi.

Inaonekana kama vile moja kati ya ushabiki mkubwa wa pambano la Simba na Yanga ni mashabiki kujitokeza uwanjani kuanzia asubuhi na kuingia moja kwa moja uwanjani. Tujitahidi kutofautisha kati ya dhiki na upenzi wa soka. Ni vitu viwili tofauti.

Ukweli ni kwamba mashabiki kuingia uwanjani saa nne asubuhi sio sifa. Kufika uwanjani saa nne asubuhi, hakuna tatizo lakini kuingia ndani ya uwanja sio sifa. Unaweza kufika uwanjani saa nne asubuhi na kufurahia mazingira ya mechi, jinsi watu wanavyoimba na kutambiana. Lakini kuingia uwanjani saa nne asubuhi ni mateso.

Wengine huwa wanaingia na watoto uwanjani. Ni mateso. Kinachosababisha watu waingie uwanjani mapema ni kujihami tu. kuwa wana uhakika akisubiri hadi wakati tunakaribia kuanza kwa mechi basi ataingia uwanjani kwa mateso makubwa.

Shabiki akishangia uwanjani anakumbana na adha ya jua. Chakula sio cha uhakika. Vinywaji sio vya uhakika. Ni mateso kwake yeye na mtoto aliyeambatana naye. Kinachonikera bado tunaishi katika dhiki hizi miaka mingi baada ya kuzinduliwa kwa Uwanja wa Taifa.

Uwanja huu ulipaswa kuendana na viwanja ambavyo binafsi nimewahi kuhudhuria mechi za soka barani Ulaya.

Santiago Bernabeu, Camp Nou, San Siro na vinginevyo ni miongoni mwa viwanja ambavyo nimewahi kutazama soka barani Ulaya. Vilinisisimua.

Uwanja wa Genk ambao vijana wetu Mbwana Samatta na Kelvin John wanacheza ni miongoni mwa viwanja ambavyo vilinisisimua. Hata mechi iwe kali kiasi gani, shabiki wa soka ataamua mwenyewe ni muda gani wa kuingia uwanjani.

Mashabiki tunajikusanya nje tukiwa tumeshikilia glasi za vinywaji, wengine wakiwa katika foleni za nyama za kuchoma na vitafunwa vingine. Kila mmoja ana tiketi yake mkononi. Mazingira ni mazuri na mechi inaweza kuwa ya watani wa jadi.

Nimetazama Lazio dhidi ya Inter, nimetazama El Clasico kati ya Barcelona dhidi ya Real Madrid. Nimetazama Real Madrid dhidi ya Atletico Madrid, nimetazama Chelsea dhidi ya Real Madrid, nimetazama Manchester City dhidi ya Atletico Madrid.

Nimetazama Kombe la Dunia, nimetazama mechi nyingi za soka la hali ya juu.

Utaratibu wa maisha ni rahisi tu. Timu zinapasha moto misuli huku unapata glasi yako ya kinywaji nje ya uwanja. Hauna hofu. Muda unaojisikia kuingia unakwenda na tiketi yako hadi katika mlango husika. Unabonyeza mahala geti linafunguka. Waliopo pale wamesimama tu kwa ajili ya kukusaidia kama haujui sehemu ya kugandamiza tiketi yako.

Kazi yao sio kukagua uhalali wa tiketi yako. Kila anayekwenda pale ana tiketi halali. Huenda ameinunua mitandaoni au katika ofisi husika za klabu ya nyumbani. Hauwezi kwenda mpaka getini kama hauna tiketi halali. Lakini mageti yako mengi na ukiingia tiketi inakupeleka katika siti yako. Hakai mtu mwingine.

Ningeweza kusema hatuwezi kuwafikia Wazungu, lakini ukweli ni kwamba nauzungumzia Uwanja wa Taifa ambao Mzee wetu Hayati Mkapa aliujenga katika zama mpya. kwanini ninachozungumzia kinawezekana katika Uwanja wa Emirates wa Arsenal uliojengwa mwaka 2006 halafu inashindikana katika Uwanja wa Mkapa ambao umejengwa mwaka 2007.

Ukweli ni hatukuamua kutumia teknolojia kwa sababu kama tungetumia basi kuna watu wangekosa mianya ya kuiba. Na kuna watu wale wanaoingia bure kama VIP nao wangeshindwa kuingia uwanjani. Katika uwanja ambao tiketi yako inakufungulia geti la kuingilia ni nguvu kwa waheshimiwa feki kuingia bure.

Tunaweza kuvisamehe baadhi ya viwanja vya zamani kama Nangwanda Sijaona, Majimaji, Ali Hassan Mwinyi na vinginevyo lakini kinachoendelea katika uwanja mpya wa Taifa nadhani ni ukosefu wa mipango na ustaarabu.

Ni hiki hiki ndicho ambacho kimeendelea kuwatesa watu wawe wanaingia uwanjani saa nne asubuhi na bado huwa tunazungumzia jambo hilo kama sifa fulani hivi ya unazi wetu mkubwa katika soka. Ukubwa wa mechi huwa hautoi mateso kwa wenzetu.

Kuna pambano kubwa la soka duniani kuliko pambano la fainali za Kombe la Dunia? Na bado shabiki mwenye tiketi halali anaamua muda wowote wa kuingia uwanjani hata kama ni bado dakika tano pambano lenyewe kuanza.

Kitu kibaya zaidi ni kwamba uwanja wetu huu mkubwa hauna matumizi makubwa zaidi ya mchezo wa soka. Majirani wa uwanja, namaanisha wakazi wa Temeke walipaswa kuwa na matumizi mengine na uwanja huu kando ya mechi. Kulipaswa kuwa na maduka mazuri, baa, na sehemu za chakula. Hata hivyo kwa sasa tunacheza mechi, mpira ukiisha Polisi wanawafukuza watu mpaka litakapofika pambano jingine.

Katika hili hili la kuingia uwanjani kwa urahisi, hasa mechi za Simba na Yanga dhidi ya wengine zinapohusika mikoani, nadhani mashabiki wengi wameamua kukacha kwenda viwanjani, hasa katika mechi zao. watu wamekuwa wakijiuliza kwanini mashabiki wanapungua lakini ukweli ni rahisi kukaa baa ukatazama soka kuliko kwenda uwanjani.

Unafikiria adha za mbwa wa Polisi na kusukumwa ingawa una tiketi yako mkononi.

Wakati huo huo ungeweza kukaa baa ukiwa na glasi yako ya kinywaji na una uwezekano mkubwa wa kutazama mechi mbili hadi tatu kwa wakati mmoja.

Unaweza kutazama Simba dhidi ya Polisi Tanzania pale Arusha na wakati huo huo TV nyingine ikawa inaonyesha pambano la Chelsea dhidi ya Manchester United pale Stamford Bridge huku TV nyingine ikionyesha pambano la Arsenal na Southampton.

Chanzo: Mwanaspoti