Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sio matokeo mazuri, lakini sio matokeo mabaya

Kibu Vs Ahly.jpeg Sio matokeo mazuri, lakini sio matokeo mabaya

Mon, 23 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hakuna siku ambayo Simba imepelekewa moto katika Uwanja wa Benjamini Mkapa kama mechi ya juzi na Mafarao wa Kaskazini katika dakika 45 za kwanza.

Al Ahly walikuwa kwenye ubora wao. Walifanya kila walichotaka kwa Simba. Sio kwamba walipata tu bao, walikuwa burudani. Kuna muda unaweza kudhani wachezaji wa Al Ahly walizidi kwa idadi uwanjani.

Wakienda mbele unaona wako wengi. Wakirudi nyuma unaona wako wengi. Simba imekuwa na rekodi nzuri dhidi ya wageni pale kwa Mkapa hakuna kukata tamaa.

Walinzi wa Simba walikatika sana dakika 45 za kwanza lakini hawakukata tamaa. Kama sio uzumbe wa Ahly, Simba ingefungwa kipindi cha kwanza hata mabao matatu. Bado Simba ni timu bora kimataifa hapa nchini.

Simba ni wanaume waliokamilika. Bado wanaweza kufanya kitu mechi ya pili. Bado wana uwezo wa kuishangaza Afrika na dunia. Uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wa Al Ahly ulikuwa unaleta utofauti mkubwa sana uwanjani. Bado Simba ina nafasi ya kufanya vizuri mechi ya pili ingawa historia ya Misri na rekodi hazipo upande wa Simba.

Ukitazama uteuzi wa kikosi cha kwanza utagundua kuwa kocha alitaka zaidi kutumia uzoefu na historia kuwafunga Ahly. Mtu kama Jose Luis Miquessone imebaki stori. Miquissone bado hajajipata. Ana kazi kubwa sana ya kurudi kwenye ubora wake.

Mara ya mwisho Al Ahly walipokuja nchini kucheza na Simba, Miquissone alikuwa kwenye ubora wake. Fundi kwelikweli. Mfalme wa nyika aliwalaza kichwa chini Waarabu hao lakini sio juzi. Alikuwa anaruka ruka tu uwanjani. Baada ya kwenda mapumziko, Mnyama mkali alirejea kamili gado. Alimleta Sadio Kanoute na Jean Baleke uwanjani. Mambo yalibadilika.

Mnyama alitumia dakika saba tu kufunga mabao mawili na kuongoza mbele ya mbabe wa Afrika. Mnyama hajawahi kuwa mnyonge kwa Mkapa. Anaweza asishinde lakini atakupa tuvitu vitu. Simba ni kama walijiamini zaidi na kusahau kujilinda. Al Ahly wakasawazisha tena. Uzuri wa kocha Robertinho kwenye mchezo wa juzi ni kufanya mabadiliko mapema. Kanoute na Baleke walibadili sana mchezo kipindi cha pili.

Hakuna mchezaji yupo kwenye kiwango bora kama Kibu Dennis pale Msimbazi. Ni kwa sababu tu baadhi ya mashabiki wamekariri. Wameamua tu kwa roho mbaya kutomkubali.

Kibu ni mchezaji mwenye kila kitu uwanjani. Ukileta mchezo wa kibabe yupo. Ukileta ustaarabu nao atakupatia. Achana na bao alilofunga, Kibu ana uronadinho flani hivi siku hizi. Anastahili sana maua yake. Mapafu ya mbwa. Yuko kwenye kila eneo. Wachezaji wa mtindo huu wako wachache sana.

Hakuna kitu huwa nashangaa kama kumuona Kibu anapelekwa benchi kirahisi. Willy Onana ana kazi kubwa sana ya kurudisha imani kwa kocha na mashabiki. Alikuwa na mwanzo mzuri, lakini kadiri siku zinavyosonga anazidi kuwa wa kawaida. Juzi alikuwa anaruka ruka tu uwanjani.

Katika usajili wa msimu huu, Che Malone na Fabrice Ngoma ndiyo wachezaji wa uhakika pale Simba. Mechi kama hizi ndiyo msingi wa kuwa na wachezaji wengi wa kigeni ili kuleta utofauti. Wageni wengi wa Simba msimu huu ni watumishi hewa.

Hapa nyumbani pamoja na Simba kuwa timu pekee iliyoshinda mechi zote tano za ligi msimu huu, pamoja na kuongoza ligi, lakini kuna propaganda nyingi juu yao. Simba haipaswi kuzisikiliza kelele za watu.

Timu yao inaimarika kila kukicha na ubora wao kimataifa ni uleule. Simba ni nembo ya soka la Tanzania kimataifa. Wanapaswa kupewa maua yao. Rekodi na historia haiwabebi sana Simba ugenini dhidi ya Al Ahly, lakini mechi bado haijaisha. Bado kuna dakika 90 nyingine kule Cairo.

Mnyama bado ana nafasi ya kuipigania bendera ya taifa letu. Dakika 25 za mwisho ni kama Al Ahly waliamua kupoozesha mchezo ili waupeleke kwao. Bado mechi inabaki kuwa wazi kwa pande zote mbili. Simba watabaki kuwa Simba tu. Hawapo kwenye ubora wao ule tuliouzoea, lakini hatoki mtu mwa Mkapa. Kuizuia Al Ahly haijawahi kuwa shughuli ndogo. Ndiyo timu bora Afrika.

Ndiyo wafalme wa soka letu lakini hawajawahi kupata mechi rahisi dhidi ya Simba. Hii ni mechi ya saba timu hizo zinakutana na hakuna mbabe dhidi ya mwenzie. Kila mtu ameshinda mata tatu na sare moja. Sio matokeo mazuri kwa Simba lakini sio mabaya.

Chanzo: Mwanaspoti