Klabu ya Yanga imesema kuwa iwapo watani zao Simba wanapanga kwenda mahakamani kushitaki kuhusu logo yao kutumika kwenye mabango ya 5-1 ya Yanga yaliyowekwa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, basi wasisahau kuwa hata zile 5 ni mali yao.
Hayo yamesemwa na Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe wakati akizungumza na chombo kimoja cha habari nchini baada ya kuweka mabango hayo kuwakera watani zao kufuatia ushindi huo wa kihistoria.
“Uongozi siku zote huwa unapanda lifti, lakini ukweli unapanda ngazi, waliwadanganya watu kwamba wao ndio klabu kubwa Tanzania lakini sasa hivi Afrika nzima inajua ni timu gani kubwa hapa Tanzania.
“Binadamu tumeumbwa kusahau, ndiyo maana tumekuja na mabango maalum ili mtu akitoka kazini anakwenda nyumbani ana-stress zake akipita pale anapata faraja.
“Leo tunamalizia utaratibu wa kuweka bango roundabout ya Bunju, tumefika FIFA tushindwe kufika Bunju? Tunataka kila mtu mwenye stress akipita pale apate furaha. Tukimaliza mabango tunahamia kwenye video za highlight za mabao yetu kwa sababu kuna mashabiki hawakufaidi vizuri haya mabao.
“Tutaweka video hizo kwenye maeneo ya matangazo barabarani, tembelea pale Morocco, Magomeni na Kilwa Road. Wanetu wa Mbagala wakipita Kilwa Road wanamwambia dereva wa daladala simamisha tutazame mabao ya Maxi, Aziz Ki na Pacome halafu mkaendelea na safari yenu.
“Trending haziendi bure, tumepata trending, tumetengeneza mabango, sponsor ameingia na pesa tumetengeneza, mashabiki wana enjoy lakini Makolo wanaumia. Hata kilio cha mtu sisi ni furaha kwetu.
“Nimeona mjadala kwamba sijui wametumia logo ya Makolo, sisi sio logo tu, pale vya kwao ni logo na zile bao tano, vyote ni mali yao. Wanapotaka kufikiria sheria waunganishe vyote logo na lile 5 kubwa waende nalo, wasilalamike nusunusu,” amesema Kamwe.