Watani wa jadi, Simba na Yanga, vita yao kwenye upande wa safu ya ulinzi na ushambuliaji sio kwenye Ligi kuu Bara tu, bali mpaka anga za kimataifa tabu ipo palepale.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Simba inashiriki, rekodi zinaonesha kuwa ipo imara kwenye upande wa kutupia ikiwa imetupia mabao 10, inashika nafasi ya pili kwa timu zenye mabao mengi Kundi C.
Vinara baada ya kucheza mechi sita katika kundi hilo la Ligi ya Mabingwa Afrika ni Raja Casablanca ambao wamefunga mabao 17, katika mabao hayo Simba imetunguliwa mabao sita na imewafunga Raja bao moja kwenye mabao yao 10.
Kwa upande wa ulinzi, Simba imetunguliwa mabao 7 ikiwa nafasi ya pili na ile ya kwanza ambayo haijafungwa mabao mengi ni Raja imetunguliwa mabao matatu, zote mbili zimetinga hatua ya robo fainali.
Yanga ambao wanashiriki Kombe la Shirikisho Afrika, wapo nafasi ya kwanza Kundi D wakiwa na pointi 13, safu ya ushambuliaji imetupia mabao 9 ikiwa inaongoza kundi huku safu ya ulinzi ikiwa imeruhusu mabao manne.
Rekodi ya Yanga ni kushinda dhidi ya TP Mazembe nje ndani kwenye hatua za makundi, huku watani zao wa jadi Simba wakitunguliwa na Raja Casablanca kwenye hatua ya makundi nje ndani ikiwa ni rekodi yao ya maumivu, lakini zote zimetinga robo fainali kwenye mashindano hayo ya kimataifa.