Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sio Freddy na Guede tu, hata hawa jamaa walichemka Bongo!

Sgsg Sio Freddy na Guede tu, hata hawa jamaa walichemka Bongo!

Fri, 22 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Huko mtandaoni na katika vijiwe vya kahawa, kuna mjadala mkubwa juu ya viwango vya nyota wapya wa Simba na Yanga waliosajiliwa kupitia dirisha dogo lililofungwa Januari 15 mwaka huu.

Mjadala huo umechangiwa zaidi na kutofikia haraka matarajio ya mashabiki kwa nyota Michael Freddy Koublan na Pa Omary Jobe wa Simba na Joseph Guede aliyesajiliwa na Yanga kuchukua nafasi ya Hafiz Konkoni aliyechemka awali licha ya kupambwa sana alipotua Jangwani ili kuziba nafasi ya Fiston Mayele aliyepo Pyramids ya Misri.

Wapo wanaoamini wachezaji hao hawakustahili kutua katika timu hizo kwa viwango walivyovionyesha katika hatua hii ya mapema, lakini wakirejea kwenye namba walizokuwa nazo, huko walikotoka wanajikuta wakiungana na wale wanaowatetea na wanaodai soka la Bongo ni pasua kichwa kwa wageni.

Pia kuna wengine wanaoamini wachezaji hao wameshindwa kubamba mapema kwa sababu soka la Ligi Kuu Bara liko juu zaidi ya huko walikotoka na pia wamekutana na mabeki wasiocheka hovyo na washambuliaji, ndio maana Freddy na wenzake bado wanajitafuta licha ya namba alizotoka nazo Zambia zinatisha.

Rekodi zinaonyesha Freddy ametua Simba kutoka Green Eagles ya Zambia akitoka kufunga mabao 14 na asisti 4 katika mechi 16 za Ligi ya Zambia.

Lakini hadi sasa Freddy amefunga mabao matatu katika Ligi Kuu, huku Pa Jobe na Guede wakiwa na bao moja-moja hadi sasa, mbali na kupewa muda wa kuzitumikia timu hiyo katika mechi mbalimbali za ligi hiyo na zile za michuano mingine wakiwa wamefunga kati bao 1-2.

Kasi hiyo ndogo japo ni mapema mno kuwahukumu kwa sasa, imewafanya wachezaji hao kutolewa macho ya kunyooshewa vidole kwa kurejea rekodi za wachezaji wengine wa kigeni waliowahi kutua Simba, Yanga na Azam na kuuwasha moto mapema akiwamo Meddie Kagere, Donald Ngoma na Mayele.

Ni kweli wachezaji hao wanahitaji muda zaidi kama ilivyokuwa kwa Obrey Chirwa aliposajiliwa Yanga mwaka 2016 hakuanza na maajabu kwa kukaa zaidi ya miezi minne bila ya bao katika Ligi, lakini code zilipofunguka, jamaa alitisha na kuanza kumezewa mate hadi na timu wapinzani.

Hata hivyo, ni bahati mbaya kwa Freddy na Guede na nyota wengine ni kwamba klabu zinahitaji matokeo mazuri kuliko huo muda wanaouhitaji na hapo ndipo wanaposakamwa kila kona.

Ila ni kwamba, hao sio nyota wa kwanza kuchemka katika Ligi Kuu Bara, licha ya huko wanakotoka kuwa na namba zinazotosha.

Hapa chini ni baadhi ya wachezaji waliosajiliwa na klabu kubwa nchini za Simba, Yanga na Azam wakibebwa na namba walizotoka nazo mahali walipokuwepo, lakini ghafla wakajikuta wakichemsha kiasi cha kugeuka kituko na mwishowe kutemwa, lakini walipoenda kwingine walitisha kwa kupiga boli.

JUMA BALINYA (YANGA)

Huyu ni mshambuliaji aliyesajiliwa na Yanga kwa mbwembwe za aina yake msimu wa 2019-2020 akitokea Polisi ya Uganda.

Balinya alitua Yanga kininja baada ya mabosi wa klabu hiyo kuwapiku wenzao wa Simba iliyokuwa ikimpigia pia hesabu ya kumbeba kutokana na kutisha kwa namba mahali alipokuwa.

Nyota huyo alitambulishwa kwenye kwenye Mkutano Mkuu wa klabu hiyo na kumwagiwa sifa kemkem kutokana na ukweli alikuwa ametoka Uganda akiwa kama Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na alitazamiwa kuwa mrithi wa Heritier Makambo aliyekuwa ameuzwa AS Horoya ya Guinea.

Wakati Makambo anaondoka Jangwani alikuwa ndiye mfungaji kinara wa Yanga akishika pia nafasi ya tatu ya Wafungaji Bora wa Ligi Kuu akifunga mabao 17 akiwa nyuma ya Meddie Kagere aliyekuwa Simba na Salim Aiyee wa Mwadui waliomaliza na mabao 23 na 18 mtawalia.

Balinya alitoka Uganda akiwa amefunga jumla ya mabao 19, yakiwamo 13 aliyofunga kwenye uwanja wa nyumbani, sita ugenini, akitumia mechi 12 tu kufunga idadi hiyo ya mabao kwa kuzitungua timu nane tofauti huku akiwa amepiga hat-trick moja na asisti tano.

Hata hivyo, mambo yalimgeukia akiwa Yanga kwani jamaa alichemka vibaya na aliondoka katika timu hiyo aliyoichezea kwa nusu msimu tu, akifunga bao moja alilowatungua JKT Tanzania kisha kupishana na Yikpe Gnamian, straika raia wa Ivory Coast aliyetokea Gor Mahia ya Kenya alikoenda Mganda huyo.

Cha ajabu ni kwamba Balinya alitisha Gor Mahia aliyoitumikia kwenye Ligi Kuu ya Kenya, wakati Yikpe aliyeondoka kwa heshima akifunga mabao mawili kwenye Mashemeji Derby dhidi ya AFC Leopards mambo yalimharibia kiasi cha kuacha gumzo nchini alipoondoka na mabao mawili tu.

MICHAEL SARPONG (YANGA)

Mkali huyo kutoka Ghana alisajiliwa na Yanga msimu wa 2020-2021 akitokea Rayon Sport ya Rwanda, akiwa amefunika kwa kufunga jumla ya mabao 23 katika michuano yote, yakiwamo 16 ya Ligi Kuu na kuiwezesha timu hiyo kubeba ubingwa wa tisa nchini humo.

Pia alifunga mabao sita katika michuano ya FA (Rwanda Cup) na kumaliza kama kinara wa mabao wa klabu na kwa kiwango alichokionyesha alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Rayon Sports na hapo ndipo Yanga ikavutiwa naye na kumbeba ikiamini ataleta maajabu yake Jangwani.

Kilichotokea ni kwamba mwamba huyo alichemka mbaya na kufunga mabao manne tu likiwamo lile la penalti lililokuwa bao la kusawazisha katika Kariakoo Derby dhidi ya Simba pambano lililoisha kwa sare ya 1-1. Licha ya kuwa na mkataba wa miaka miwili aliutumikia mmoja tu kabla ya kutemwa.

DAN SSERUNKUMA (SIMBA)

Usajili wa mshambuliaji huyo ndiyo ulionekana kutikisa katika timu hiyo ya Simba msimu wa 2014-2015 alipomchomoa Amissi Tambwe katika dirisha dogo ili alete moto aliouwasha Kenya.

Simba ilimsajili nyota huyo raia wa Uganda kwa kuamini kwamba ni mchezaji imara kutokana na rekodi zake akiwa Gor Mahia ambako alikuwa ni mfungaji bora mara mbili mfululizo katika ligi ya Kenya 2012/13 na 2013/14.

Alikuwa na rekodi ya mabao 49 katika mechi 73 lakini alipofika Simba alicheza mechi 12 na kufunga mabao sita tu, yakiwamo matatu ya Ligi Kuu, huku akikosa namba muda mwingi ndani ya kikosi hicho.

Baada ya kutoka Simba timu ya mwisho kuichezea ilikuwa ni Vipers ya nyumbani kwao Uganda na kumaliza na rekodi ya mabao 23 katika mechi 32.

LAUDIT MAVUGO (SIMBA)

Inafahamika kuwa usajili ni kama mchezo wa kubahatisha na ndicho kilichotokea kwa wekundu hao baada ya kumsajili Mrundi huyo kwa mbwembwe baada ya kumfukizia kwa muda mrefu akiwa Vital’O.

Ingawa alikuwa na rekodi nzuri ya kufunga mabao 62 katika misimu miwili mfululizo wa kwanza akifunga 32 na mwingine 30, lakini alipotua Msimbazi msimu wa 2016-2017 alishindwa kuonyesha makali, licha ya kufunga mabao muhimu ikiwamo dhidi ya Yanga, ila haikuweza kuwa sababu ya yeye kucheza vizuri kama ilivyotarajiwa na mabosi hao kuamua kumpa mkono wa kwaheri.

Maajabu ni kwamba baada kutoka Simba alitimkia Napsa ya Zambia ambako alionyesha soka na kuwa Mfungaji Bora wa Zambia kwa kufunga mabao 10 kisha baadae kuibukia Difaa el Jadida ya Morocco waliyokuwa wakichezea Watanzania Saimon Msuva na Nickson Kibabage.

HAFIZ KONKONI (YANGA)

Mshambuliaji huyu mwenye asili ya Ghana alisajiliwa msimu uliomalizika akiwa kama mbadala wa mshambuliaji Fiston Mayele kutoka Congo.

Alisajiliwa baada ya waliokuwepo kushindwa kuonyesha uwezo nao ni Clement Mzize na Kennedy Musonda.

Mayele aliondoka akiwa na rekodi ya mabao 17 na kuibuka mfungaji bora Ligi Kuu Bara msimu uliopita na baadaye kutimkia Pyramids.

Mrithi huyo wa Mayele naye hakuwa na rekodi mbaya alikotoka katika timu ya Bechem United FC ya Ghana, kwani aliibuka mfungaji bora namba mbili kwa kupachika mabao 15 na asisti tatu katika mechi 26 za Ligi Kuu.

Alifahamika kwa uwezo mkubwa wa kufunga akiwa ndani ya boksi, kwa namna alivyoweza kumiliki mpira, ana uwezo mkubwa wa kupiga mashuti na anajua kupiga pasi.

Lakini hakuweza kuonyesha makali hayo alipokuwa Yanga, kwani alicheza mechi sita tu na kufunga bao moja katika ligi, huku kimataifa alicheza jumla ya dakika 17 tu, akiwa hana bao lolote na katika dirisha dogo akafunguliwa mlango wa kutokea akidaiwa kwenda Cyprus.

YAHYA MOHAMMED (AZAM)

Alitua Azam FC msimu wa 2016-2017 akitokea Ghana alikowaka akiungana na Mzimbabwe Francisco Zukumbawira, akiaminika angekuwa na maajabu akiwa sambamba na nduguye, Yakubu Mohammed anayecheza beki wa kati ambaye alijijengea heshima kubwa kiasi cha kupewa unahodha.

Yahya alijiunga na Azam Juni 2016 akitokea Aduana Stars ya Ghana, aliyoisaidia kushika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Ghana msimu 2015-2016 na mshambuliaji huyo aliiibuka mfungaji bora namba mbili wa ligi hiyo akifunga mabao 15, mawili pungufu na aliyokuwa nayo Latif Blessing wa Liberty Proffesional aliyetupia 17 aliyeibuka kidedea.

Hata hivyo, tofauti na matumaini ya mabosi wa Azam juu ya namba alizotua nazo klabuni, Yahya alichemsha kwani katika msimu mmoja na ushei aliyokuwepo klabuni hapo hakufikia hata robo ya mabao aliyoyafunga katika ligi ya Ghana, zaidi ya kuisaidia Azam kubea Kombe la Mapinduzi tu.

Katika Ligi, Yahya aliishia kufunga mabao matatu, yakiwamo mawili ya msimu wa kwanza na moja la msimu uliofuata kisha kusitishiwa mkataba Novemba 2017 kutokana na kushindwa kuwa na maajabu, hata hivyo alivyorudi kwao Ghana aliendelea kuwa na moto hadi kuuzwa Mexico.

MOZINZI MPIANA (AZAM)

Mshambuliaji huyo raia wa DR Congo aliyezitetemesha Simba na Yanga kuvizia saini yake, alitua Azam FC msimu wa 2020-2021 akiwa na namba zinazotisha katika klabu alizopita akiwa kwao DR Congo.

Azam ilimchukua kutoka Maneama akitarajiwa kuibeba timu hiyo kwa upande wa eneo la ushambuliaji ajiungana na kina Obrey Chirwa, lakini mwamba huyo alishindwa kuwika katika Ligi Kuu Bara na haikuwa ajabu hadi anaondoka Chamazi alikuwa amefunga mabao mawili tu katika mechi alizoichezea timu hiyo ambayo iliamua kumleta Idris Mbombo pia kutoka DR Congo kuziba nafasi yake ambaye naye hakuwa na maajabu sana japo alikuwa na afadhali kuliko nyota huyo.

GNAMIAN YIKPE (YANGA)

Mshambuliaji aliyesubiriwa kwa shauku katika usajili wa mwaka 2020 alitikisa kutokana na rekodi zake nzui alizokuwanazo Gor Mahia na timu nyingine alizopita kabla ya kutua Yanga.

Muivory Coast huyo alipotua Jangwani hakuweza kutisha na hadi mwisho aliondoka akiwa amefunga mabao 2 tu dhidi ya Singida na jingine FA.

Alipewa mkono wa kwaheri na viongozi wa timu hiyo na aliposepa cha ajabu ni kwamba alienda kukiwasha upya na swali likabaki kuwa shida ilikuwa nini alipokuwa Yanga.

GEORGE ODHIAMBO (AZAM)

Mkali huyo aliyefahamika kama Black Berry naye alichemsha kwani alikuwa na rekodi ya mabao 16 katika mechi 48 alipokuwa Gor Mahia ya Kenya.

Mambo yalibadilika alipotua katika kikosi cha Azam, kwani rekodi zake zilipotea na mwisho hakuweza kuendelea na mkataba wake.

Wapo wengi ambao walikuwa na rekodi kubwa lakini walipotua katika timu mpya hasa hizi kubwa hapa nchini walichemka na kuondoka wakiwa wameacha rekodi mbaya, mfano wao ni kama Sidney Urikhob alitoka na bao moja tu, Patrick Sibomana aliyetoka na mabao saba.

Chanzo: Mwanaspoti