Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida yatinga 16 bora ASFC

Wachezaji Singida FG.jpeg Singida yatinga 16 bora Shirikisho

Tue, 20 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Singida Fountain Gate, imesonga mbele katika hatua ya 16 bora michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), baada ya kuifunga FGA Talents mabao 2-0.

Timu hiyo imepata ushindi huo jana Februari 19, 2024 mbele ya FGA Talents ya mkoani Morogoro, inayoshiriki Ligi ya Championship, katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza katika mchezo wa raundi ya tatu (32 bora), ambao umeanza saa 10:00 jioni.

Singida ambayo imehamishia mechi zake za nyumbani Uwanja wa CCM Kirumba, imepata mabao yake kupitia kwa Mkongomani, Francy Kazadi dakika ya 11 akimalizia vyema pasi ya Dickson Ambundo.

Matajiri hao wa alizeti walienda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0 baada ya Dickson Ambundo, kuifungia bao la pili dakika ya 45 kwa mkwaju mkali akiwatambuka mabeki wa FGA Talents.

Dakika ya 88, FGA Talents wamekosa nafasi muhimu ya kusawazisha bao, baada ya mshambuliaji wa timu hiyo, Zamfuko Elias, kukosa mkwaju wa penalti.

Baada ya ushindi huo na kutinga hatua ya 16 bora ya michuano hiyo, Singida Fountain Gate, sasa itasubiri kufahamu mpinzani katika hatua inayofuata ya michuano ya Kombe la Shirikisho ikisaka tiketi ya kucheza michuano ya kimataifa barani Afrika baada ya mambo kuwawia magumu kwenye Ligi Kuu.

Ushindi huo ni ishara njema kwa Singida Fountain Gate ambayo imehamishia mechi zake za nyumbani katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, kufuatia Uwanja wa Liti mkoani Singida kufungiwa, ambapo Februari 28 itaikaribisha Azam FC dimbani hapo katika mchezo wa Ligi Kuu.

Ushindi huo ni wa kwanza kwa Singida tangu Desemba 15, 2023, ilipoichapa Arusha City FC kwenye raundi ya nne ya Kombe la Shirikisho, ambapo baada ya hapo imecheza michezo mitatu ya ligi na kupoteza yote ikifungwa 1-0 na Geita Gold, ikafungwa 1-0 na Kagera Sugar na wiki iliyopita imechapwa 3-1 na Tanzania Prisons.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live