Singida Fountain Gate imewapiga mkwara JKU ikitamba imepanga kupata matokeo mazuri watakapovaana raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Singida na JKU zitacheza mchezo wa kwanza leo Ijumaa kwenye Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 1:30 usiku, na akizungumza jana, mtendaji mkuu wa timu hiyo, Olebile Sikwane alisema lengo lao ni kufanya mashindano ya kimataifa na Ligi Kuu na ndio maana wamefanya usajili mkubwa.
“Tumesajili wachezaji wakubwa na uzoefu wa soka hapa nchini na Afrika, na lengo likiwa ni kuhakikisha timu inafanya vizuri ndani na nje,” alisema Sikwane.
“Kimataifa lengo letu kubwa ni kufika hatua ya makundi na ndio maana tunahakikisha timu inakuwa bora kila idara kuanzia kwenye uongozi hadi wachezaji.”
Sikwane alisema wanakabiliwa na ratiba ngumu kimataifa na Ligi Kuu, lakini ujio wa meneja wa oparesheni, Jonathan Kasano utasaidia
Naye Kasano alisema hana maneno mengi badala yake ni kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri kwanza kwa ajili ya mchezo dhidi ya JKU.
“Viongozi wote wa CAF wameshaingia (nchini). Wageni wetu (JKU) nao wapo na wale waamuzi watafika usiku wa leo (jana),” alisema.
Kasano ana uzoefu wa takriban miaka sita katika soka nchini akifanya kazi kama meneja wa Bodi ya Ligi.