Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida yaipora Simba beki kimafia

Yahaya Mbegu To Simba Singida yaipora Simba beki kimafia

Fri, 26 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa Simba walishaanza kuhesabu saa kabla ya kumuona beki mpya wa makrosi akitua katika timu hiyo ili kuimarisha kikosi hicho kwa msimu ujao, lakini ghafla mambo yametibuka baada ya matajiri wa Singida Big Stars kumpora kimafia na kuwaachia Msimbazi wakibaki na mkataba tu.

Ipo hivi. Simba ilishamalizana na Yahya Mbegu anayekipiga Ihefu kwa kumpa mkataba wa awali ili atue kikosini na Mwanaspoti lilishawajulisha mapema, lakini dili hilo limetibuka baada ya mabosi wa Msimbazi kushindwa kumpa kishika uchumba, kitu kilichomfanya Singida kumbeba kirahisi.

Mwanaspoti linafahamu kuwa, beki huyo wa kushoto anayesifika kwa kupiga krosi za mabao, alishamalizana na mabosi wa Simba baada ya klabu hiyo kuwa ya kwanza kumfuata na kuzungumza naye kiasi cha kumsainisha mkataba wa awali, lakini aliwaomba wamwekea Sh 5 Milioni amalize ishu zake binafsi, lakini mabosi wa Msimbazi wakasikilia fedha na fasta Singida wakawatibulia.

Mtu wa karibu na mchezaji huyo alilidokeza Mwanaspoti kuwa, Mbegu alisaini mkataba huo wa awali lakini bado ana mkataba na Ihefu japo walishazungumza na viomgozi wenzao wa Ihefu, lakini kitendo cha kumcheleweshewa kishika uchumba kimechangia kubadili akili na kutua Singida.

“Kweli alikuwa na dili ya kwenda Simba na walikubaliana kila kitu, ila sasa huyu kijana akabadili upepo baada ya kucheleweshewa kutimiziwa ahadi kwa vile aliomba kiasi flani cha fedha," kilisema chanoz hicho na kuongeza;

“Hata hivyo wakati akiendelea kuwasikilizia Simba, mabosi wa Singida wakapata taarifa na fasta wakamfuata na kumalizikana naye sambamba na klabu yake ya Ihefu na kwa sasa anasubiri msimu uishe ajiunge na wawakilishi hao wa michuano ya kimataifa kwa msimu ujao."

Mwanaspoti limedokezwa kuwa mkataba huo wa Mbegu na Singida ni wa miaka miwili na kwamba benchi la ufundi lilikuwa linamhitaji mno beki huyo ili kuongeza ushindi kwa mabeki waliopo kwa sasa akiwamo Mganda Shafik Batambuze na Yassin Mustafa.

Uwepo kwa Mustafa na Batambuze ulichangia kumfanya beki chipukizi Nickson Kibabage kuhamisihiwa eneo la mbele akicheza kama winga ambaye kwa sasa anatajwa yupo mbioni kusajiliwa na Yanga kwa ajili ya msimu ujao.

Inaelezwa benchi na mabosi wa Singida wamemsajili haraka Mbegu kwa lengo la kuhakikisha wanakuwa na beki wa kuaminika kwa zipo tetesi kwamba Batambuze kama ilivyo kwa Kibabage huenda akaondoka kikosini, hivyo kusaliwa na beki mmoja tu wa kushoto.

Ndani ya Ihefu, Mbegu amekuwa chaguo la kwanza la timu hiyo na mchango wake umeifanya timu hiyo kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuepuka kushuka daraja tofauti na ilivyokuwa mwishoni mwa duru la kwanza la msimu huu ilipokuwa ikiburuza mkia.

Habari kutoka ndani ya klabu ya Singida ni kwamba beki huyo na nyota wengine wanasajiliwa kwa sasa kwa ajili ya michuano ya CAF ya msimu ujao baada ya timu hiyo kujihakikisha kutaka tiketi kwa kuwa ndani ya Nne Bora ya Ligi Kuu, huku ikiwa pia imefika nusu fainali ya Kombe la ASFC.

Chanzo: Mwanaspoti