Singida Big Stars jana iliondoka nchini kwenda Misri kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Future FC, huku ikiahidi makubwa.
Singida na Future zitacheza Oktoba Mosi, saa 12:00 jioni katika Uwanja wa Al-Salam jijini Cairo.
Timu hiyo iliondoka ikiwa na mtaji wa ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Septemba 17. Singid iliondoka mapema kwa nchini ili kuzoea mazingira ya Misri na kuepuka figisu za Future kwani itakuwa na siku nne za kukaa kabla ya mchezo.
Katika mchezo wa Ligi Kuu uliopita, timu hiyo ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC ambao ulikuwa mkali, lakini ulilipa kipimo tosha benchi la ufundi linaloongozwa na Mathias Lule na Ramadhan Nswazurimo.
Mshambuliaji wa Singida Big Stars, Thomas Ulimwengu akizungumzia mchezo wa marudiano alisema licha ya kuwamba wanacheza ugenini, bado wana nafasi ya kusonga mbele.
Ulimwengu alisema wanacheza na timu ngumu ikiwa nyumbani, lakini hiyo sio sababu kubwa ya kuwafanya washindwe kupata ushindi.
“Sikuhizi mpira umebadilika sio kama zamani. Anayecheza kwa nidhamu ndiye atakayeshinda kwa hiyo tukienda vizuri na kwa kufuata maelekezo ya makocha tutapata ushindi na kutimiza malengo yetu,” alisema Ulimwengu.
Wachezaji walioondoka ni Beno Kakolanya, Benedict Haule, Ibrahim Rashid, Laurian Makame, Biemes Carno, Hamad Waziri, Kelvin Kijiri na Yahya Mbegu.
Wengine ni Gadiel Michael, Morice Chukwu, Azizi Andambwile, Yusuph Kagoma, Deus Kaseke, Dickson Ambundo, Duke Abuya, Bruno Gomes na Marouf Tchakei, Meddie Kagere, Elvis Rupia, Francy Kazadi na Thomas Ulimwengu.