Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida vs Simba; tuwafunge ngapi leo?

Singida Simba Pic Data Singida vs Simba; tuwafunge ngapi leo?

Wed, 9 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ni zamu ya mashabiki 10,000 na ushee wa Mkoa wa Singida kushuhudia live boli likitembea kwenye mechi dhidi ya Singida na Simba.

Mashabiki wa Simba jana walikuwa wakiwatambia wenyeji nje ya Uwanja wa mazoezi wakiwauliza; “Tuwafunge ngapi?” Haswa wakitambia kipigo cha mabao 5-0 kwenye mechi ya Mtibwa. Lakini Meddie Kagere wa Singida amesisitiza kwamba leo ni kazi kazi na hakuna kuangaliana usoni na waajiri wake wa zamani kwani walishamalizana na sasa anapambana na malengo ya Singida kwenye Uwanja wa Liti.

Nahodha wa Simba, Mohammed Hussein alisema jana kwamba ukubwa na uzoefu wa wachezaji wa Simba utaamua mchezo huo.

Singida inaingia ikiwa imetoka kushinda bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania lililofungwa na Meddie Kagere Jumapili iliyopita mjini Karatu.

Singida Big Stars ilirudi Singida juzi na jana ilifanya mazoezi mepesi na kutokana na ukaribu wa kucheza mechi haitashangaza kama miili ya wachezaji wa Singida ikiwa na uchovu tofauti na Simba ambao hawajacheza mechi yoyote tangu Oktoba 30 walipoishinda Mtibwa Sugar mabao 5-0.

MECHI TANO

Singida ni ya nne ikiwa imecheza mechi tisa, imeshinda tano, sare na kufungwa miwili, ikifunga mabao manane na kufungwa matano ina pointi 17.

Simba ipo nafasi ya pili imecheza mechi nane, imeshinda tano, sare mbili, imefungwa moja, imefunga mabao 17, imefungwa manne pointi sawa na Singida Big Stars. Singida ikipata ushindi itakwenda nafasi ya pili ikiwa na pointi 20 sawa na ilizo nazo kinara Yanga, lakini Simba ikishinda itakwenda hadi kileleni mwa msimamo itakuwa na pointi sawa na Yanga, ila itakuwa imefunga mabao mengi.

Katika michezo mitano iliyopita Simba imeshinda mabao 5-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, ilifungwa 1-0 na Azam, suluhu na Yanga, ilishinda 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji na kushinda 1-0 ugenini kwa Tanzania Prisons. Matokeo ya michezo yote mitano iliyopita Simba ilikuwa chini ya kocha Juma Mgunda.

Michezo mitano iliyopita Singida ilishinda bao 1-0 dhidi ya Polisi, ilishinda 1-0 kwa Ihefu, ilishinda 2-1 kwa Kagera Sugar na kupoteza miwili mfululizo yote ikifungwa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa na Azam.

HAWATAKUWEPO

Simba huenda ikawakosa nyota wanne huku watatu ni majeruhi Israel Mwenda, Jimsony Mwanuke na Nelson Okwa, ilhali Clatous Chama atakosekana kutokana na kufungiwa mechi tatu.

Singida itawakosa makipa wawili chaguo la kwanza Metacha Mnata aliyefungiwa na chaguo la pili Benedict Haule aliyepata kadi nyekundu dhidi ya Polisi Tanzania.

Nafasi ya kucheza inabaki kwa Abubakar Khomeny aliyecheza mechi ya kwanza ya ligi msimu huu dhidi ya Polisi Tanzania.

VIKOSI HIVI HAPA

Kikosi cha Simba huenda kisiwe na mabadiliko makubwa;

SIMBA: Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Henock Inonga, Joash Onyango, Mzamiru Yassin, Pape Sakho, Sadio Kanoute, Moses Phiri, Kibu Denis na Augustine Okrah.

SINGIDA: Khomen, Paul Godfrey, Shafiq Batambuze, Abdulamajid Mangalo, Biernes Carno, Aziz Andambwile, Nicholas Gyan, Bruno Gomes, Meddie Kagere, Dario Fredirico na Rodrigo Fegu.

MECHI ITAAMULIWA

Kulingana na ubora wa makocha Hans Van Pluijm (Singida) na Juma Mgunda wawili hao ni waumini wa soka la chini yaani ‘boli litembee’.

Simba silaha yake inaweza kuwa ni ubora wa viungo Mzamiru, Kanoute na Sakho wenye uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga kwa Phiri na Okwa ingawa muda mwingine hufunga wenyewe.

Eneo hilo Singida kuna Andambwile ambaye hufanya kazi nzuri ya kukaba huku Bruno, Ndemla na Dario wakitengeneza nafasi za kufunga kwa washambuliaji. Kutokana na uimara na ubora wa viungo wa timu zote mechi inaweza kuamuliwa katikati.

WALIOPITA SIMBA

Kikosi cha Singida ni kipya kwenye ligi, lakini wachezaji wengi wamepita timu kubwa nchini - Simba na Yanga na watacheza wakitaka kuonyesha wana viwango bora.

Ukiachana na hilo kuna waliopita Simba kila kama Pascal Wawa, Ndemla, Gyan, Kagere na Amiss Tambwe. Kutokana na uwepo wa wachezaji hao huenda wakaongeza ugumu wa mchezo pande zote mbili.

AZAM FC vs DODOMA JIJI

Mechi nyingine itakayochezwa leo, Azam itaikaribisha Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 1:00 usiku.

Kaimu kocha mkuu wa Azam, Kally Ongala alisema: “Kila timu inayokuja kwenye uwanja wa Chamazi huwa inakamia kuhakikisha inapata matokeo. Kwa hiyo tunajua tuna mechi ngumu lakini tutapambana kuhakikisha tunapata pointi tatu.

Naye kocha wa Dodoma Jiji, Melis Medo alisema kikosi chake kimebadilika, akisisitiza: “Dodoma Jiji tumebadilika kwa asilimia kubwa na sasa tupo kwenye asilimia 70 ya ubora, mchezo utakuwa mgumu lakini sote tunahitaji matokeo na ndani ya dakika 90 ndizo zitaamua.”

Chanzo: Mwanaspoti