Wawakilishi pekee wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Singida Big Stars inatarajiwa kushuka Uwanja wa Al Salaam katika mchezo wa marudiano dhidi ya Future ya Misri kusaka tiketi ya makundi ya michuano inayoishiriki kwa mara ya kwanza tangu ipande Ligi Kuu.
Mchezo huo umepangwa kupigwa saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, huku Singida iliyobeba matumaini zaidi kwa Watanzania katika michuano hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi ya kwanza bao 1-0, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Misri, kocha msaidizi wa timu hiyo, Thabo Senong alisema hamasa imekuwa kubwa kwao huku akiweka wazi kila mchezaji ameonyesha utayari wa kupambana katika mchezo huo.
"Kila mmoja wetu anajua umuhimu na ugumu wa mchezo huu lakini sapoti ambayo tumepata hapa tangu tumewasili imetupa morali kubwa ambayo tunaamini kwa utimamu na utayari wa wachezaji tutapata matokeo chanya," alisema.
Kwa upande wa nyota wa timu hiyo, Nicholas Gyan alisema wao kama wachezaji wamejiandaa ipasavyo na licha tu ya uwepo wao ugenini na ugumu wa mchezo huo ila watapambana kuhakikisha wanafuzu makundi na kuandika rekodi.
Senong ambaye ni raia wa Afrika Kusini anaiongoza timu hiyo kwa sasa baada ya Kocha Mkuu Mjerumani, Ernst Middendorp kutimka Septemba 19 ikiwa ni muda mchache tu tangu ajiunge nao akichukua nafasi ya Hans Van de Pluijm.
Middendorp ndiye aliyeiongoza timu hiyo katika mchezo wao kwanza na Future uliopigwa Uwanja wa Azam Complex na kuiwezesha kushinda 1-0 hivyo kuiacha Singida ikihitaji ushindi au sare tu ili kutinga hatua ya makundi.
Hans aliiongoza Singida kufuzu hatua hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3, dhidi ya JKU ya Zanzibar huku akiiongoza katika mchezo mmoja tu wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons ulioisha 0-0, Agosti 22, 2023.