Singida Fountain Gate FC imeshindwa kutamba nyumbani mbele ya watoto wa Kinondoni timu ya KMC FC baada ya kulazimishwa suluhu.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara umepigwa jana Jumatatu Desemba 11 kwenye Uwanja wa Black Rhino uliopo mjini Karatu mkoani hapa ambao timu ya Singida Fountain Gate umeichagua kama uwanja wake wa nyumbani baada ya Liti uliopo mjini Singida kufungiwa na Bodi ya Ligi.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilianza kwa kasi huku kila timu ikihitaji kupata bao la mapema na kujitengenezea mazingira mazuri ya kuondoka na pointi zote tatu lakini kukosa umakini na utulivu kwa safu zao za ushambuliaji ilifanya dakika hizo kukamilika bila kushuhudiwa goli.
Licha ya mabadiliko kadhaa za kiufundi ambazo zilifanywa na walimu wa timu zote Heron Ricardo upande wa wenyeji Singida Fountain Gate na Abdihamid Moalin wa KMC kila mmoja akiutaka zaidi mchezo lakini pia ilishuhudiwa ngoma ikizidi kuwa ngumu na kufanya dakika 90 kukamilika bila bao lolote.
Matokeo hayo yanazifanya timu hizo mbili kuishusha Simba SC mpaka nafasi ya tano ambapo Singida sasa ndio inashika nafasi ya tatu kwa alama 20 sawa na KMC ambayo ipo nafasi ya nne zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa huku zikiwa zimecheza mechi 13.
Simba SC inashika nafasi ya tano kwa alama zake 19 baada ya mechi nane, imeshinda sita, sare moja sawa na iliyopoteza huku ikifunga mabao 18 na kufungwa 11.
Baada ya mchezo wa jana wa Ligi Kuu Bara, Singida Fountain Gate inageukia mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports ambapo itacheza Desemba 15 mwaka huu dhidi ya mabingwa wa Mkoa wa Arusha timu ya Arusha City katika uwanja wa Black Rhino.
KMC nayo inarudi Dar kwenda kuisubiri bingwa wa Mkoa wa Manyara timu ya Aca Eagle kutoka mjini Babati ambapo itacheza nayo Desemba 17 katika uwanja wa Uhuru.
Mechi nyingine iliyopigwa leo ni Azam FC ikiichapa JKT Tanzania mabao 2-1. Mabao ya Azam yamefungwa na Sospeter Bajana na Idd Nado huku la JKT Tanzania likifungwa na Najimu Magulu.